Wananchi Mvomero wamlalamikia DC

Mtanzania - - Habari - Na ANDREW MSECHU - DAR ES SALAAM

WANANCHI wa vijiji vitano katika kata mbili za Wilaya ya Mvomero, wanalalamikia kunyang’anywa ardhi yao ya asili waliyoishi kwa zaidi ya miaka 65 sasa.

Wakizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam, wawakilishi wa wananchi hao walisema wameamua kuomba msaada kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Rais Dk. John Magufuli baada ya kubaini kuwapo mchezo mchafu unaomhusisha Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mohamed Utali na baadhi ya viongozi wa Serikali katika suala hilo.

Wawakilishi hao (majina yanahifadhiwa) walisema wamekuwa wakitishiwa na kuhamisha kwa nguvu katika maeneo yao ambayo yalithibitishwa kuwa ardhi za vijiji kisheria tangu mwaka 2004, kwa madai kuwa ni sehemu ya hifadhi za taifa lakini wamebaini kuwa maeneo hayo yameanza kupewa mwekezaji.

“Maeneo haya yapo katika Kata za Mtibwa na Kata ya Kanga katika vijiji vitano na kwa miaka yote yalikuwa yakitumika kwa kilimo na makazi.

“Tumebaini upo mpango wa kuwapa wawekezaji wa Mtibwa Forest Plantation kwa hila,” alisema mmoja wa wawakilishi hao.

Alisema pamoja na malalamiko yao kufika ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma ambayo iliuagiza uongozi wa Mkoa kupitia barua Na BD.214/282/01/01 iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa Waziri Mkuu Agosti 8 mwaka huu kumtaka Mkuu wa Mkoa wa Wilaya, Utali kushughulikia suala hilo na kurejesha majibu, bado hakuna hatua zilizochukuliwa.

Alivitaja vijiji vitano ambavyo eneo lao la zaidi ya kilometa za mraba 2500 limeporwa kuwa ni Kijiji cha Kanga, Kaole na Dihinda katiuka Kata ya Kanga na vijiji vya Kunke na Mlumbilo katika Kata ya Mtibwa.

Alisema kutokana na hali hiyo kaya 715 zenye zaidi ya watu 4516 kwenye vijiji vitatu wamekwisha kuathirika na tathmini inaendelea katika vijiji viwili, ambako pia makazi, makanisa, misikiti, vituo vya afya na shule vimebomolewa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.