Mgombea udiwani CCM aahidi kujenga barabara

Mtanzania - - Habari - Na MWANDISHI WETU - DAR ES SALAAM

MGOMBEA udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Magomeni, Shaweji Kumbula, amesema ili kumuenzi mtangulizi wake marehemu Julian Bujugo, atahakikisha anasimamia ndoto yake kwa kujenga barabara ya lami katika mitaa ya Uwazani na Mkadini.

Pia ameahidi kutoa mikopo kwa wanawake na vijana na kuhakikisha miradi yote ya maendeleo iliyoahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM inatekelezwa kabla ya hajamaliza kipindi chake cha uongozi.

Hayo aliyasema juzi alipokuwa akiomba kura kwenye mkutano wa kampeni ya kuwania udiwani uliofanyika Mtaa wa Dosi.

Alisema kazi ya CCM ni kuhakikisha inatenda kwa ajili ya watu na si maneno kama ilivyo kwa vyama vingine.

Mkumbula alisema ana matumani atachaguliwa kuongoza kata hiyo Januari 19 mwaka huu na katika uongozi wake hatakuwa na ubaguzi kwa wananchi wote ikiwamo wa vyama vya upinzani.

“Marehemu Bujugo (Julian) alikuwa rafiki yangu sana na moto ya ndoto yake kabla ya mwaka 2020 ilikuwa ni kuhakikisha barabara ya Mkadini na Uwazani inawekwa lami nami nitalifanya hivyo kama njia ya kumuenzi, ninawaomba sana wanamagomeni.

“Na leo hii (juzi) ninamuona Songoro Mnyonge hapa naye ni diwani (Mwananyamala) alikuwa rafiki mkubwa wa Bujugo.

“…hata ndani ya ukumbi pale manispaa walikuwa wakikaa viti jirani, ninaomba ili kuenzi urafiki ule kile kiti kisitolewe Songoro awe ananikumbusha kila alichokuwa akisistiza marehemu.

“Msiwasikilize wale wengine (wapinzani), mimi ndiye diwani wenu kura zote nipeni miye Januari 19 nami sitawaangusha, nitaleta maendeleo kwa kasi ndani ya kata yetu,” alisema Mkumbula

Aliahidi kuendelea kutoa mikopo kwa vijana na wanawake ambako hadi sasa zimekwisha kutolewa zaidi ya Sh milioni 100 na bado kuna mahitaji.

“Mimi nitafanya mara mbili yake kwenye suala la mikopo, ninachowaomba endeleni kujenga imani kwa CCM na Rais Magufuli ambaye amekuwa akitekeleza ilani kwa vitendo,” alisema.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Mkoa wa Dar es Salaam, Yussuf Nassoro, alisema vyama vya upinzani vimekwisha kupoteza mweelekeo kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Rais Dk. John Magufuli.

“Rais Magufuli amekuwa na kazi kubwa ya kuleta maendeleo kwa kasi katika taifa letu, kila Mtanzania anaona.

“Ndani ya miaka mitatu barabara, reli, madaraja na hata ununuzi wa ndege kila mmoja anaona. Sasa mchagueni Shaweji awe diwani, kazi hii izidi kufanyika zaidi katika Kata ya Magomeni,” alisema Nassoro

NAKAGUA: Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, akikagua daftari la mmoja wa wanafunzi wa Chuo cha Utumishi alipowatembelea katika Kampasi ya Dar es Salaam jana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.