RC apiga marufuku TRA kufunga maduka ya wafanyabiashara

Mtanzania - - kanda Ya Ziwa - Na RENATHA KIPAKA

MKUU wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali, Marco Gaguti amewataka watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani kuacha mara moja tabia za kufunga biashara za wananchi kwa sababu ya kodi.

Amesema badala yake wajikite katika kuwaelimisha ili kulipa kodi kwa utashi bila kushurutishwa.

Pia aliwataka kuweka mkakati wa kuwapata walipakodi wapya na kuwaelimisha namna ya kufanya biashara zao na kulipa kodi.

Maagizo ya RC Gaguti aliyatoa juzi katika kikao cha baraza la wafanyabiashara katika Manispaa ya Bukoba. Katika kikao hicho aliwaita wafanyabiashara hao kuwasikikiliza kero zao lengo likiwa ni kuboresha ulipaji wa kodi katika Mkoa wa Kagera ikiwamo kufikia malengo ya ukusanyaji wa kodi kwa mwaka 2018/2019 kwa asilimia 100.

Kabla ya RC kutoa maagizo hayo, aliwapa nafasi wafanyabiashara kuchangia namna bora ya kuhakikisha kodi inakusanywa kwa asilimia 100 mkoani humo na kuhakikisha wafanyabiashara wote wanafikiwa ili kodi katika mazingira mazuri ya kufanya biashara bila bughudha.

Wafanyabiashara walilalamika utendaji kazi wa TRA kuwa inakusanya kodi bila kutoa elimu na haijengi mazingira mazuri ya kuwasikiliza wafanyabiashara walipe kodi kwa utashi. Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao mfumo unaotumiwa na TRA unasababisha wafanayabisahara wengi kufunga biashara zao.

Baada ya kuwasikiliza RC alisema anataka katika Mkoa wa Kagera kuwe na mazingira mazuri ya wafanyabiashara kufanya biashara zao na kulipa kodi bila kushurutishwa.

Alisema ni muhimu kila mfanyabiashara atambuliwe ili kuwa na takwimu sahihi za wananchi wote wanaojishughulisha nabiashara.

Gaguti alitoa siku 14 kwa Serikali za mitaa kuwatumia viongozi na watendaji katika ngazi za kata hadi vijiji kuwatambua wafanyabiashara wote wakubwa au wadogo ili kuwe na takwimu sahihi ya mkoa kuhusu wananchi wanaojishughulisha na biashara.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.