Ziwa Kitangiri lafungwa hadi Aprili

Mtanzania - - Mkoa Kwa Mkoa - Na SEIF TAKAZA

HALMASHAURI za Wilaya ya Iramba Mkoa wa Singida na Meatu, Mkoa wa Simiyu, zimekubaliana kwa pamoja kufunga Ziwa Kitangiri hadi Aprili 17, mwaka huu.

Makubaliano hayo yalifikiwa juzi katika kikao cha pamoja cha ujirani mwema kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Mkoa wa Simiyu.

Katika kikao hicho, kamati za ulinzi na usalama za wilaya hizo zikiongozwa na wakuu wa wilaya ambao pia ni wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama za wilaya, zilishiriki.

Akifungua kikao hicho cha ujirani mwema, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dk. Joseph Chilongani, alisema limekuwa jambo jema kwa kamati za ulinzi na usalama pamoja na wenyeviti wa halmashauri zote mbili na baadhi ya madiwani wa halmashauri hizo, kuwa na kikao cha pamoja cha kuhakikisha wanalinda Ziwa Kitangiri kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa halmashauri hizo.

“Ni jukumu letu sisi viongozi wa wilaya hizi kuhakikisha tunatunza na kuhifadhi mazingira ya Ziwa Kitangiri ili kutoa fursa ya samaki wazaliane kwa wingi.

“Jambo la msingi hapa kwa Halmashauri za Wilaya za Iramba, Meatu, Igunga na Wilaya ya Kishapu ni kwamba, tulikuwa na utaratibu wa pamoja wa kufunga Ziwa Kitangiri kila mwaka lakini hatukuwa na mpango mkakati wa pamoja kuamua ni lini ziwa hili litakuwa linafungwa kila mwaka.

“Hata hivyo, katika kikao cha ujirani mwema tulichofanya mjini Shinyanga mwaka juzi, tulikubaliana kuhifadhi Ziwa Kitangiri na kupiga vita kwa nguvu uvuvi haramu huku tukihakikisha mazingira ya ziwa yanakuwa mazuri ili samaki wazaliane kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho,’’ alisema Dk. Chilongani.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula, alisema ziwa hilo limeshafungwa kwa upande wa Wilaya ya Iramba kuanzia Januari mosi, mwaka huu.

“Ndugu mkuu wa Wilaya ya Meatu, kwa upande wetu tulishafunga Ziwa Kitangiri kama kawaida yetu ya kila mwaka ila mwaka huu tumeona tuje kujiridhisha katika Wilaya ya Meatu maana miaka yote sisi tulipokuwa tukifunga kwa upande wetu, huku Meatu walikuwa wanavua,” alisema Luhahura.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.