Shule ya msingi yakabidhiwa choo cha kisasa

Mtanzania - - Mkoa Kwa Mkoa - Na JANETH MUSHI

SHULE ya Msingi Selian iliyopo Wilaya ya Arumeru, mkoani hapa, imekabidhiwa jengo la choo cha kisasa kilichogharimu zaidi ya Sh milioni 28 baada ya kile kilichokuwa kikitumika awali kutitia mwishoni mwa mwaka jana.

Msaada wa choo hicho ulitolewa juzi na shirika lisilo la kiserikali la Kilimanjaro Technology, ambapo kina jumla ya matundu 10.

Oktoba mwaka jana, taharuki iliibuka shuleni hapo baada ya mwanafunzi wa darasa la kwanza shuleni hapo, Emanuel Ephraim (7), kunusurika kufa baada ya choo kuzama wakati akijisaidia.

Shirika hilo linalofanya kazi zake jijini hapa na lenye makao yake makuu nchini Marekani, lilikubali kujenga vyoo vya kisasa shuleni hapo wakati wanafunzi wakitumia vyoo vya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Selian.

Akizungumza wakati wa kukabidhiwa jengo hilo la choo, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro, aliwashukuru wadau hao wa elimu kwa msaada huo ambao alisema utasaidia wanafunzi hao kusoma katika mazingira salama.

Alisema kwamba, choo ni moja ya miundombinu muhimu kwa wanafunzi wawapo shuleni, hivyo akawataka walimu kuwasimamia wanafunzi hao ili kukakikisha kinatunzwa vizuri.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.