Waziri ahimiza wanawake kliniki

Mtanzania - - kanda Ya Ziwa - Na OSCAR ASSENGA

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema asilimia 24 ya wajawazito nchini, ndiyo wanaohudhuria kliniki wakati wa wiki 12 za mwanzo.

Kutokana na hali hiyo, Mwalimu amewataka wajawazito wahakikishe wanahudhuria kliniki mapema pindi wanapogundua kuwa ni wajawazito.

Kwa mujibu wa Mwalimu, kipindi hicho ambacho mjamzito anaweza kujua kama ana magonjwa ikiwamo kisukari na kuweza kuchukua hatua ya kuzuia mapema maradhi hayo.

Waziri huyo aliyasema hayo juzi wakati akipokea mashine mbili za ultrasoud na mashuka 150 ya hospitali yaliyotolewa na mdau wa maendeleo mkoani Tanga, Habibu Nuru, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za kuboresha huduma za afya hasa za mama na mtoto nchini.

Mwalimu ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CCM, alisema msaada huo utasaidia kuokoa maisha ya wajawazito jijini Tanga pamoja na watoto wachanga.

“Ndugu zangu wajawazito nchini, ni lazima mhakikishe mnahudhuria kliniki mapema pindi mnapogundua ni wajawazito.

“Nasisitiza mahudhurio hayo kwa sababu kwa nchi nzima, asilimia 24 ya wajawazito ndiyo wanaohudhuria kliniki katika wiki 12 za mwanzo.

“Idadi hiyo inatakiwa kuongezeka kwa sababu hapo ndipo unapojua kama una ugonjwa wa sukari au una magonjwa mengine yanayoweza kudhibitiwa haraka.

Naye Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Daudi Mayeji, alimshukuru mdau huyo wa maendeleo pamoja na familia yake kwa sababu msaada alioutoa utasaidia kuokoa maisha ya wananchi.

Pia, Mayeji alimshukuru Waziri Mwalimu kwa kile alichosema kuwa amekuwa mstari wa mbele kusaidia maendeleo mkoani Tanga.

“Tunakushuru wewe mdau wa maendeleo pamoja na Waziri Ummy kwa sababu msaada huu utakuwa ni mkubwa katika afya za wananchi,” alisema Mayeji.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.