NCAA yatoa angalizo

Mtanzania - - kanda Ya Ziwa - Na ELIYA MBONEA

MAMLAKA ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), imezitaka Halmashauri za wilaya ya Karatu na Ngorongoro, kutumia Sh bilioni moja ilizozitoa kwa malengo yaliyokusudiwa.

NCAA ilitoa Sh milioni 500 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya huku Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ikipewa Sh milioni 500 za ujenzi wa vituo viwili vya afya.

Akikabidhi msaada huo jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NCAA, Profesa Abiud Kaswamila, alisema anaamini fedha hizo zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Kwa bahati nzuri, mamlaka kwa sasa tunao utaratibu wa kufuatilia fedha zinazotolewa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nje na ndani ya mamlaka.

“Katika suala la maendeleo, NCAA huchangia asilimia 15 ya pato ghafi katika mfuko wa Serikali na fedha hizo husaidia mipango ya maendeleo nchini ikiwa ni sehemu ya chachu ya kukuza uchumi.

“Pamoja na kuendelea kuchangia mfuko mkuu wa Serikali, NCAA itaendeleza utaratibu wa kufadhili miradi ya maendeleo ya jamii ndani na nje ya hifadhi ili wananchi waone umuhimu wa kuhifadhi rasilimali adimu.

“Jamii inayozunguka Hifadhi ya Ngorongoro, ni wadau muhimu wa uhifadhi endelevu na kwa kutambua hilo, NCAA imekuwa ikifadhili miradi ya maendeleo kupitia utaratibu wa ujirani mwema.

“Kwa mfano, mwaka 2016/17, tulitumia shilingi milioni 359.1, mwaka 2017/18 tulitumia shilingi milioni 295 na mwaka 2018/19 tulitenga shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya shughuli za maendeleo za ujirani mwema.

“Kwa ujumla, michango inayotolewa kusaidia miradi ya maendeleo, imekuwa chachu kwa wananchi kufichua watu wanaohujumu maliasili zetu wakiwamo majangili,” alisema Profesa Kaswamila.

Akipokea mchango huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, aliishukuru NCAA kwa kuendelea kutambua juhudi za Serikali za kuwaletea wananchi maendeleo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Theresia Mahongo na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Rashid Taka, waliishukuru NCAA kwa kuwapatia mchango huo huku wakiahidi kwenda kusimamia shughuli za ujenzi wa majengo yaliyokusudiwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.