Sakata la Makonda, polisi ukweli waanikwa

Rai - - MBELE - NA LEONARD MANG’OHA

KAMANDA wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ameuanika ukweli halisi wa

sakata la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwapongeza askari polisi, akidai kuwa halikukiuka sheria wala maadili ya jeshi hilo. RAI linaripoti.

Makonda alifanya hivyo mwishoni mwa wiki iliyopita kwa kile alichokiita kuwa ni kufanya kazi nzuri wakati wa zoezi zima la uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Ukonga na udiwani kata ya Vingunguti.

Kamanda Mambosasa alisema kitendo cha askari wa jeshi hilo kusherehekea kazi waliyoifanya hakijakiuka maadili ya jeshi hilo.

Alisema askari hao walikuwa wakifurahia kutokana kukamilisha kazi ya kusimamia uchaguzi huo bila kulazimika kutumia nguvu.

Katika kufafanua zaidi alisema kwa kawaida huwa wanafanya tathmini kabla na baada ya operesheni yoyote, hivyo baada ya kumaliza uchaguzi huo bila askari kulazimika kutumia nguvu na mabomu kukabiliana na wananchi waliamua kujipongeza kwa vinywaji.

“Baada ya kukamilisha ile kazi tulikuwa tunawatawanya wale askari kwenye vituo vyao, kwa sababu kulikuwa na askari kutoka Pwani na Tanga. Sasa kwa sababu walikuwa na njaa wakawa wanapata vinywaji vilivyokuwa pale.

“Wakati tunaendelea kuburudika akaja Mkuu wa Mkoa (Paul Makonda) akawa anasherehekea nao, hakuna maadili yaliyokiukwa pale, na kwa sababu yeye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa lingetokea jambo la tofauti angeitwa kuulizwa kwa sababu halijatokea jambo baya si vibaya kupongezwa” alisema Mambosasa.

MAKONDA HAPOI

Uamuzi huo wa Makonda umeibua mjadala wenye pande mbili tofauti ukiwahusisha wasomi na wanasiasa.

Makonda ambaye tangu ateuliwa kwake kuwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Machi 2016, amekuwa haishi kuibua mijadala kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kutokana na kauli ama matendo yake.

Miongoni mwa matukio ya Makonda yaliyoibua mijadala ni hatua yake ya kuwatangaza hadharani baadhi ya wafanyabiashara, wasanii na wanasiasa aliowahusisha na dawa za kulevya.

Mbali na hilo pia akiwa katika ziara zake za Dar Mpya alipata kutoa kauli kadha wa kadha pamoja na kuwasema hadharani baadhi ya watumishi wa Serikali wa mkoa wa Dar es Salaam ambao mara nyingi amekuwa akiutaja kama mkoa wake.

Ukiachilia mbali hayo, mwishoni mwa mwezi uliopita jina jina la Makonda lilichomoza upya na kuibua mjadala mzito uliohusisha Makontena 20 yaliyopachikwa jina la ‘Makontena ya Makonda’.

Hatua ya kuwapongeza askari hao kutoka Dar es Salaam, Tanga na Pwani imewaibua wasomi na wanasiasa ambao wameonesha kuipinga hatua hiyo.

Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR Mageuzi) amesema kuwa kitendo cha Makonda kuwaandalia polisi hafla ya kuwapongeza kufanikisha chaguzi ndogo kwa amani, kimedhihirisha namna jeshi hilo linavyotumika kisiasa.

Akizungumza na RAI, Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi alisema uamuzi huo ni maangamizi kwa Taifa.

“Umeona polisi wanambeba Makonda, wanamshangilia, hivi ni vielelezo vya wazi, vitendo vinavyofanyika sasa ni maangamizi kwa taifa letu. Hakuna mahali popote duniani vyombo vya dola vimewahi kuzidi nguvu ya umma,” alisema.

Hoja hiyo ya Mbatia pia imeungwa mkono na Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu kishiriki cha Ruaha (RUCU), Profesa Gaudence Mpangala ambaye pamoja na mambo mengine alisema hali hiyo sasa imedhihirisha wazi bila kificho tena kuwa jeshi la polisi linatumika kisiasa.

Alisema awali vilionekana kutumika kwa njia za kujificha, lakini sasa hali imekuwa tofauti kwani vinatumika wazi wazi.

Alisema hali hiyo inaibua utata hasa ikizingatiwa kazi ya polisi ni kulinda raia na mali zao.

“Ila kitendo cha kuonesha furaha na kumshangilia Makonda ambaye pia ni kada wa CCM, kimeonesha wazi kuwa namna gani Jeshi hilo linatumika kisiasa,” alisema

Kama ilivyo kwa Mbatia na Profesa Mpangala, hali imekuwa hivyo pia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, ambaye amesema wazi kuwa Makonda hakupaswa kufanya sherehe na polisi kwa sababu kuna mahali hali haikuwa shwari na wao walikaa kimya.

Polepole aliyasema hayo mwanzoni mwa wiki hii, alipozungumza na waandishi wa habari ndani ya ofisi ndogo za CCM Lumumba, jijini Dar es Salaam.

Alisema Chadema imekuwa ikisema kuwa jeshi la Polisi linawasaidia wakati aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Ukonga kwa tiketi ya chama hicho cha upinzani Asia Msangi alimkwida msimamizi wa uchaguzi mbele ya polisi na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.

“Makonda hakupaswa kufanya sherehe nao kwa sababu kuna mahali sheria ya tume ilikiukwa na ilikiukwa huku polisi wakiwepo na wametulia,”alisema Polepole.

RAI lilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Barnabaa Mwakalukwa ili kuzungumzia suala hilo lililohusisha askari wa Tanga na Pwani, hata hivyo alisema kuwa hilo si suala la kitaifa.

“Mimi ni professional, nenda kaulize kwa Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Mambosasa, mimi ni msemaji wa polisi Tanzania nzima. Hilo si jambo la kitaifa,” alisema.

Paul Makonda

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.