‘First lady’ wa kwanza kwa nani?

Rai - - MAKALA -

Kuanzia katikati ya karne ya kumi na tisa baada ya Kristo [BK], msamiati mpya wa “First Lady”, yaani, “Mama wa Kwanza” ulimea na kujichimbia mizizi katika “Kamusi” ya tawala za nchi za Kiafrika na dunia ya tatu kwa ujumla. Dhana hii ya “Mama wa Kwanza”, kwa maana ya mke wa kiongozi wa nchi, sasa imeingia kwa kishindo kikubwa kiasi cha kuzoeleka na kuonekana kama sehemu ya utawala wa nchi ambapo wake za Viongozi wanaweza kuzungumzia au kutoa kauli elekezi kwa masuala ya kitaifa.

Katika nchi zingine, kina mama hawa wana nguvu kubwa kuweza kusababisha Maofisa wa ngazi za juu Serikalini kama Mawaziri, Makatibu Wakuu wa Wizara na Wakuu wengine wa asasi mbali mbali nchini, kumwaga unga.Kwa mfano, nchini Kenya enzi za utawala wa Rais wa kwanza wa nchi hiyo, hayati Jomo Kenyatta, mke wa Rais, Mama Ngina, aliogopewa na Baraza lote la Mawaziri kuliko lilivyomwogopa Rais mwenyewe.

Nchini Malawi, enzi za utawala wa hayati Rais Dk. Hastings Kamuzu Banda, ingawa hakuwa na mke rasmi, kazi ya kuchunguza mienendo ya Mawaziri na Watendaji wakuu wengine wa Serikali ilifanywa na Mama Kazimiri, mwanamke aliyekuwa na nguvu na kuogopewa pengine kuliko Banda mwenyewe.

Huko Ufilipino, wakati wa utawala wa hayati Rais Ferdinand Macros, mke wa Rais huyo, Mama Imelda Marcos [ aliyewahi kuwa “Miss” Ufilipino wakati fulani], kwa “nguvu” alizokuwa nazo, alikuwa ni kama Msaidizi wa Rais huyo katika kuitawala nchi, asiyetambuliwa na Katiba.

Kina mama hawa, wakati mwingine na mahali pengi, wamekuwa na ushawishi mkubwa kwa waume zao katika uteuzi wa Mawaziri na Watendaji Wakuu Serikalini, hata bila kujali uwezo wa wanaoteuliwa, mradi tu wako karibu na “first lady” wa nchi husika.

Licha ya kujipenyeza katika utawala wa nchi kinyume cha Katiba, kina mama hawa pia waliwekewa kasma maalum kutoka mafungu ya serikali kugharamia shughuli zao zisizo rasmi wala za kiserikali, kama wake za Marais. Mara nyingi, nchi zinazopenyeza wake za Wakuu wa nchi kuwa na kauli turufu katika mambo ya utawala na Serikali, zinatawaliwa kwa aina fulani ya udikteta, maana kwa watawala wengi, “kitanda” kina nguvu kubwa kuliko kauli ya “mlala hoi”.

Katika nchi zinazozingatia Katiba na majukumu ya uongozi, kutambulika kwa dhana ya “First Lady” inakuwapo kwa jina tu kama heshima ya mke wa mtawala wa nchi, basi. Kwa mfano, hatukusikia mama Keneth Kaunda [Zambia], Mama Nyerere au mama Sekou Toure [Guinea], wakijaza kwa pupa kurasa za mbele za magazeti kwa kujikweza au kujipa utukufu katika masuala ya nchi kama Ma “First Lady”.

Vivyo hivyo, hatukusikia mama Kwame Nkrumah, Mama Murtala Mohammed [Nireria] au Mama Dauda Jawara [Gambia] wakiitwa na kufurahia jina hilo kwa sababu walielewa ubatili wake kwa misingi ya utamaduni wa Kiafrika na dhana sahihi ya Katiba na utawala wa nchi.

Cha kushangaza kwa dhana hii ni kwamba inapokuwa Mkuu wa nchi ni mwanamke, mumewe haitwi “Mwanaume wa Kwanza – “First Man”. Hatukuwahi kusikia “First Man” baba Corazon Aquino, “First Man” baba Golda Meir, “First Man” baba Bandaranaike, au “First Man” baba Hellen Sirleaf Johnson, na kadhalika. Kwa nini?.

Ndipo tunapojiuliza: First Lady kwa maana ya “Mama wa Kwanza” au “Mama Nambari Wani” katika mpangilio wa hadhi au sifa za wanawake; wa kwanza kwa nani? Na sifa hizo ni zipi?

Kama “First Lady” ina misingi ya utawala wa nchi, kwa nini kusiwe na “First Man” kwa maana ya “Mwanaume wa Kwanza” – mume wa Kiongozi wa nchi mwanamke?.

Hakuna kinachoitwa “Mama wa Kwanza” katika jadi za Kiafrika, wala hakuna neno linalofanana nalo kuweza kuelezea hilo. Ni kwa sababu Afrika asilia haijawahi kuwa na mama wa aina hiyo.

Kwa Afrika, wanawake wote wako sawa na wake za watawala ambao nao ni wanawake tu miongoni mwa wanawake. Tofauti ndogo iliyopo kati ya wake za watawala na wanawake wengine ni ya hadhi tu ya kimazingira zaidi kuliko hadhi ya kijinsia na kijamii.

Kama ilivyosemwa kwa usahihi, kwamba mke ni “Waziri” mfawidhi wa mambo ya ndani katika familia, ndivyo ilivyo kwamba, wake za watawala ni viongozi wa familia na wafawidhi wa masuala ya makazi ya waume zao, yasiyohusiana na mambo ya kiserikali. Na ndivyo ilivyo kwa mke yeyote katika makazi na familia ya mumewe.

Kwa hiyo, tofauti iliyopo kati ya mke wa mtawala na mke wa raia wa kawaida, si katika nafasi na wajibu wao katika familia, bali ni hadhi ya mahali na mazingira wanapotekelezea wajibu huo.

Mke wa mtawala si sehemu ya mamlaka ya utawala wa nchi na kamwe hapashwi kutekeleza majukumu ya utawala wa nchi kama mke wa Mtawala. Ingawa imeandikwa katika misahafu ya dini kwamba, “Mume na mke ni mwili mmoja”, lakini kwa mujibu wa misingi ya mamlaka ya utawala wa nchi, mume na mke ni watu wawili tofauti inapokuwa katika kutekeleza majukumu ya nchi na uwajibikaji. Wala Katiba za nchi haziwatambui wake za Viongozi, na familia zao kuhusiana na mambo ya nchi na Taifa.

Hii ni kwa sababu taifa halimchagulii mtawala mke, wala mke wa mtawala hapashwi kuapa kwa Katiba ya nchi jinsi ya kutekeleza majukumu yake ya kifamilia katika makazi ya mtawala - Ikulu

Ni kwa sababu hii kwamba, wake za watawala duniani kote ni wake au ni wanawake sawa tu na wake za wananchi wengine wenye majukumu sawa katika familia zao; wote wanaheshimika na kuwajibika kwa majukumu katika maeneo yao tofauti.

Kwa Afrika asilia ya kale, Wafalme walitawala; lakini kamwe mke wa Mfalme hakuruhusiwa kutenda wala kuzungumzia majukumu ya utawala ya mume wake kwa sababu hawakuwa sehemu ya utawala wa nchi.

Ipo mifano tele ya Wafalme walioondolewa madarakani kwa sababu ya kudhalilisha nafasi zao kwa kuruhusu siri na mambo ya utawala kuingiliwa na familia zao. Katika jadi na utamaduni wa Afrika, watawala waliteuliwa ili watawale kwa haki, hekima na usawa kwa kutumia vipaji vyao bila kushirikisha familia zao katika masuala ya kitaifa.

Wapo Viongozi wa kale waliojutia kuchanganya siri za utawala na mambo ya kifamilia kwa wake zao: Samson alitoa siri juu ya nguvu zake za kutawala na vita kwa Delilah akaangamia.

Mwenyekiti Mao Tse Tung wa China alijiachia, mke wake akaweza kujiunga na kundi la maadui wa ustawi wa Taifa la China [The Gang of Four], na alipobaini hilo, akalazimika kuwaangamiza kwa kuwapiga risasi, akiwamo mke wake.

Ni Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius K. Nyerere aliyeonya kwa kusema: “Ikulu ni mahali patakatifu”. Kwa hiyo, dhamana anayopewa Kiongozi wa nchi kwa nchi ni kubwa na nyeti, isiyopaswa kutekenywa na wanafamilia wa mtawala wasiotambuliwa na Katiba, wakiwamo Ma-“First Lady”.

Kwa kusema haya, hatuna maana ya kuwabagua au kuzionea gere “mbavu” za Wakuu hao wa nchi kwa ushiriki wao katika masuala ya kitaifa ya waume zao.

Tunachosema ni kwamba, mambo ya kitaifa yanapaswa kushughulikiwa na mtawala mwenyewe ambaye ndiye mwenye Mkataba wa kutawala, kati yake na watawaliwa. Kina mama hao wanaweza kuupata utukufu wanaotamani kwa kujitosa moja kwa moja katika uongozi wa nchi, baadala ya kutaka kuupata kwa migongo ya “waume” zao waliofungwa mikono na Katiba.

Itaendelea wiki ijayo.

Mke wa Rais Janeth Magufuli na mke wa Waziri Mkuu Mary Majaliwa wakielekezana jambo

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.