Wavuta sigara kwenye mikusanyiko wameshindwa kudhibitiwa?

Rai - - MAKALA - NA HASSAN DAUDI

KWAKWELI ni tabia inayokera, ukiacha ukweli kwamba ni hatari kwa afya za watu wanaomzunguka mtu huyo, yaani mvutaji sigara.

Nikitolea mfano katika vituo vya daladala ambako tabia hii imetamalaki, ni kawaida mtu kuwasha sigara yake bila kujali afya za waliopo mbele, nyuma, au pembeni yake.

Aidha, utaushuhudia utamaduni huo wa ajabu katika sherehe, misiba, viwanja vya michezo, mikutano ya hadhara, ikiwamo ya siasa, na mikusanyiko mingine. Hakika inashangaza kuona hakuna anayejali.

Ukiweka kando madhara ya sigara kwa mtumiaji, ikiwa ni pamoja na kumsababishia ugonjwa hatari wa kansa, huenda wanaomzunguka wakati anavuta aidha hawajui au wanapuuzia namna ambayo nao wamekuwa wakiumia.

Mfano, tafiti mbalimbali zimeonesha mtu aliye karibu na mvutaji, hufikiwa na kemikali 70,000 zitokanazo na sigara, huku nyingine zikiwa ni zinazosababisha kansa.

Wataalamu wa afya wamebaini kuwa uwezo wa kusikia wa mtoto unaweza kuathiriwa na moshi wa sigara uliokuwa ukimfikia akiwa tumboni.

Hiyo ni mbali ya tafiti nyingie kudai kuna uwezekano mkubwa wa mtoto huyo kuwa mvutaji hapo baadaye endapo atakapozaliwa atakuwa anamuona baba yake akifanya hivyo.

Je, ukiacha waliopo katika familia yake, mvutaji amekuwa akiwadhuru watoto wangapi anapowasha sigara yake kituo cha daladala? Hakika ni wengi ingawa imekuwa likichukuliwa kuwa ni jambo la kawaida.

Ukifuatilia kwa makini, utagundua kuwa suala hilo la uvutaji sigara kwenye mikusanyiko wa watu linawakera wengi lakini tatizo ni kwamba kumekuwa na kawaida ya kuoneana aibu.

Mfano; katika msiba, kama anayevuta ni baba, mjomba au kaka, aghalabu huwa ngumu kumzuia kwa maneno au vitendo kwani kunaweza kuonekana ni kumvunjia heshima.

Kama haitoshi, hebu jiulize, ni marafiki zetu wangapi wanaoweza kuwasha na kuvuta sigara mbele yetu na tunashindwa kuwaambia kwa kuwa tutapishana nao kauli na mwishowe kugombana?

Kwamba tupo tayari kuumizwa na kemikali zilizotakiwa kuwadhuru kwa uzembe wao, kisa tu kuilinda heshima au urafiki ambao kwa mazingira hayo hauna tija yoyote? Haika ni upuuzi.

Pia, lipo suala la woga, kwamba anayefanya upuuzi huo ni mtumiaji wa dawa za kulevya, au mwenye tabia zingine za kihuni, yaani zisizo kubalika katika jamii, ikihofiwa kuwa kumzuia ni kumkorofisha na kutafuta tatizo.

Kwa mazingira hayo basi, mkono wa sheria uko wapi kukabiliana na tabia hiyo sugu na yenye madhara makubwa si tu kwa mvutaji bali pia kwa wanaomzunguka?

Katika hilo, safu hii ya ‘Macho Yameona’ inashauri hatua ya kwanza iwe ni kukomesha biashara ya sigara katika vituo vya daladala ambavyo kila uchwao havikaukiwi umati wa watu.

Aidha, iwe hivyo pia katika viwanja vya michezo, vituo vya treni, katika mikutano ya hadhara, na maeneo mengine yanayoikutanisha idadi kubwa ya watu.

Kuonesha kuwa ni juhudi ndogo tu zinazoweza kulimaliza tatizo hilo, mbona katika baadhi ya ofisi onyo la uvutaji sigara limefanikiwa? Kwanini ishindikane katika vituo vya daladala, ikizingatiwa kuwa onyo litasimamiwa na sheria?

Pia, kuna hili la kuona maeneo hayo yakitengewa vyumba maalumu kwa ajili ya uvutaji sigara na si kokote kama inavyofanyika sasa.

Ni kweli sigara ni moja kati ya mazao yanayoipatia Serikali fedha nyingi, lakini hiyo inaweza kuwa na faida yoyote ikiwa mamilioni ya watu wake wanateketea?

Hivyo, ufike wakati kama ilivyo katika kukabiliana na majanga mengine, zikiwamo ajali za barabarani na utumizi wa dawa za kulevya, sheria kali zipambane na hili la sigara zinazovutwa ovyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.