JOKATE: Aliyefanikiwa amekaa kwenye mabega ya wakubwa

Rai - - MAONI/KATUNI - NA SIDI MGUMIA, ALIYEKUWA KISARAWE

UKIONA mtu amefanikiwa ujue amekaa kwenye mabega ya watu wakuu (giants) ambao wametengeneza ile njia ya yeye kuweza kufanikiwa…” Hii ni kauli ya mkuu wa wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo, aliyoitoa wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la kituo cha mafunzo cha kilimo cha muhogo cha mradi wa Green Voices katika kijiji cha Kitanga wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.

Katika hafla hiyo Jokate alisema yeye kama binti, kama mama, kama kiongozi wa Serikali anasikia faraja na furaha kusema mafanikio yao yanatokana na akina mama kama Getrude Mongela, ambao wamesaidia kutengeneza njia anayoipita leo.

“Isingekuwa hawa kuthubutu na kujitoa tusingefika hapa, kwasababu kuna kipindi akina mama walikuwa wanadharaulika, wanaonekana hawawezi, hasa ukiwa na umri mdogo, lakini kupitia kwao dhana ile imefutika, hawajatuangusha.

“Wamefanya kazi nzuri na kazi zao zimeonekana na wanazidi kupata sifa ndani na nje ya nchi, na kwa kazi nzuri walizozifanya sisi kama wanawake tunatembea vifua mbele, kwa kujiamini kwamba tunaweza bila hata kuwezeshwa kwasababu najua hata nyinyi mlivyoanza hizi harakati mlikutana na changamoto.

“Mama Mongela ana historia ndefu sana ndani na hata nje ya nchi, na hata ulipoenda Beijing, kupigania haki, tayari mlishaanza bila hata ya kuwezeshwa na huo ndio uthubutu tunaoutaka hata kwa watoto wetu.”

Jokate amesema kwakupitia wakina mama hawa ndio wao wamepata ujasiri wa kusema kuwa tuna mama zetu wamethubutu na wameweza na wametengeneza njia, kwahiyo na sisi tunajukumu la kuendeleza hayo mazuri na makubwa waliyoyafanya na waliyoyapigania kwa ajili ya nchi yetu.

Alisema akina mama ni mfano bora hata katika familia kwani watoto wanapata faraja kuona mama akichakarika kutafuta chakula.

“Nimefika hapa kama Serikali kuwapongeza, nawapongeza kwa hatua hizi mlizofikia. Wilaya ya Kisarawe iko mkoa wa Pwani, ambako sasa kuna viwanda vingi na sasa wanasema Pwani yetu ni Pwani ya Viwanda.

Alisema katika eneo la kilimo wameweka kipaumbele kwenye muhogo na korosho na tayari yeye ameshaanza kuyafanyia kazi mazao hayo.

“Nilikutana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Benki ya NMB, katika mambo mengi tuliyoyagusia ilikuwa ni pamoja na jinsi yakuwawezesha wakulima wetu katika mazao ya korosho na muhogo.

“Tumetoa milioni 112.3 katika awamu ya kwanza, tutakua na awamu mbili za kutoa mikopo ambayo sasa hivi itakuwa ikitoka bila riba, tunamshukuru sana Waziri Selemani Jaffo (TAMISEMI), yeye ndiye alisimamia hili, hela hizi za Halmashauri zinatoka kwa wananchi, sasa kwanini zitoke kwa wananchi halafu watoe tena riba, na ikapitishwa.”

Katika kuhakikisha Kisarawe inakuwa kibiashara alisema hayuko tayari kuona watu wa wilaya hiyo wanafanya kazi ndogo ndogo badala yake anatamani kuona kila mmoja wao anafanikisha malengo yake.

Alisema uanzishwaji wa kiwanda kwenye kijiji cha Kitanga ni fursa kubwa kwao na atakachokifanya ni kuwasisitiza TARURA waharakishe ujenzi wa barabara ya kwenda kwenye kiwanda hicho.

Alisema lengo la Serikali ni kuwawezesha wananchi ili kutekeleza kazi waliyotumwa na Rais na kwamba ameahidi kupima viwanja kupitia wataalamu wa wilaya yake.

TATIZO LA MAJI

“Kuna suala la uhaba wa maji, na hii ni moja ya changamoto ambayo nilikuwa nikiisikia kabla hata sijafika Kisarawe. Nilipoapishwa tu nikaanza kuuliza hivi Kisarawe ninakoenda kuna changamoto zipi, Kwasababu Rais anavyokuteua anataka ushughulike na changamoto zile muhimu zinazogusa wananchi na uzifanyie kazi, na mimi nikauliza na nadhani asilimia 99.9 wakawa wanasema kuna tatizo kubwa la maji, na nimefika kweli hilo tatizo nimelikuta.

“Kwa bahati nzuri nimefika wakati hilo tatizo limeanza kuwa historia kwa maana ulisainiwa mkataba Mei 27, mwaka huu wa mradi wa maji kutoka Ruvu Juu kupitia Kibamba, kilometa 17 mpaka Mnarani, na pale tunajenga kisima na mimi nimeshatembelea lile eneo la mradi, wameanza kufanya kazi Agosti na kwa bahati nzuri sasa lile tenki linajengwa tenki lenye uwezo wa kujaza maji lita milioni sita kwa siku na sisi tulivyofika pale tulikuta mchakato umeshaanza.

“DAWASA tumekutana na Mkandarasi ofisini kwetu, wameniahidi kulitatua tatizo hilo kwa haraka.

“Niwatie moyo, Serikali chini ya Jemedari wetu Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk. John Joseph Pombe Magufuli , inafanya kazi.

“Sisi ni wateule wake, sisi ni watumishi wenu, sisi tumekuja kuwatumikia, hatujaja hapa kukaa kwenye magari, kuchekacheka na kula, kunywa siku imeisha, sisi tunafanya kazi ,kwahiyo ninaomba sana tushirikiane.

“Nikiona wananchi wanafanya jitihada kama hizi, hata sisi tunahamasika kwamba kazi tunayoenda kuifanya inabadilisha maisha ya watu na inathaminiwa, kwahiyo naomba sana tushikamane,tupendane, tushirikishane kwa masuala ya maendeleo ya wananchi wetu.

“Sisi ni viongozi vijana, Rais ametuamini na tunapenda tupokee changamoto zenu na tunapenda pia ninyi wazee wetu mtuambie kwa jinsi tunavyoishi kwamba hapa tukienda hivi, tutafanikiwa zaidi na sisi tutasikiliza kwasababu kiongozi mzuri ni yule ambaye ni msikivu. Kwahiyo tunawakaribisha sana, tushirikiane, tunaenda kujenga Kisarawe mpya na Kisarawe mpya itajengwa na sisi wenyewe.

KAULI YA BALOZI MONGELA

Balozi Mongela ambaye pia ni mlezi wa mradi wa Green Voices alisema anafuraha kuendesha mradi huo wilayani Kisarawe.

Alisema Green Voices imetokana na taasisi ya Women for Africa ambayo ilianzishwa na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Spain Maria Teresa De la Vegas ambaye baada ya kustaafu, aliamua kusaka ushirikiano na wanawake wa Afrika.

“Nakumbuka hata mkutano wake wa kwanza Niger, tulikuwa pamoja na bahati nzuri nikateuliwa kuwa kwenye bodi ya taasisi hii ambayo tumefanya nayo kazi na tumepata fursa hapa Tanzania kupitia mradi huu ambao unaongozwa na Secelela Balisidya akiwa pamoja na wenzake.

“Green Voices ni jina letu, tumeanzisha miradi mbalimbali Tanzania ambako wakina mama wanafanya shughuli zao za kuleta maendeleo.

“Tulifanya uzinduzi wa mradi huu hapa nchini na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alishiriki akiwa na Maria Tereza De La Vegas.

“Miradi 10 katika mikoa sita ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Kigoma Morogoro na Pwani imeingia awamu ya pili sasa na tunategemea tutapanuka katika mikoa mingine mingi Tanzania.

MRATIBU WA MRADI

Mratibu wa mradi huo Balisidya aliyataja mafanikio ya akina mama hao kuwa wamenunua mashamba kwa ajili ya kuendeleza kilimo, kununua mashine mbalimbali za kuboresha mnyororo wa thamani wa mazao yao ya kilimo na kujenga majengo ya kudumu (training centres) ikiwa ni sehemu ya mafunzo kwa wananchi wote wanaopenda kujifunza kutoka Green Voices.

“Kupitia ofisi ya uratibu wa mradi, Green Voices tumeweza kusajili jina letu la Green Voices Women kama jina la biashara ili lebo zetu zitutambulishe sokoni. Hivyo napenda kuchukua fursa hii kuwahimiza Watanzania kununua bidhaa zenye nembo yetu ili kuunga mkono juhudi zetu.

“Katika kipindi hiki, licha ya akinamama zaidi ya mia tatu kushiriki moja kwa moja katika miradi, lakini pia tumetoa mafunzo kwa wanawake na wanaume wapato 235 na tayari baadhi yao wameenda kuanzisha katika maeneo yao.

KAULI YA ABIAH

Mtekelezaji wa mradi huo Abiah Majura Magembe ambaye ni afisa kilimo na lishe mstaafu alisema mradi wake ulianza na kikundi cha Wakinamama wapatao 64 lakini kutokana na sababu ambazo hazikuweza kuzuilika walibakia wakinamama 34 tu.

Alitoa mafunzo yenye lengo la kuwajengea uwezo Wakinamama kujua jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na changamoto zake kama wazalishaji wakuu wa mazao ya chakula katika kaya.

“Masomo yalifundishwa kwa nadharia na vitendo, upande wa nadharia walifundishwa kanuni bora za kilimo katika kuzalisha zao la muhogo, kwa upande wa vitendo walifundishwa Teknolojia sahihi za kisasa ambazo ni pamoja na usindikaji, hifadhi na matumizi bora ya zao la muhogo ikiwa ni upangaji, utayarishaji na mapishi mbalimbali ya matumizi ya unga wa muhogo.

“Kupitia ufadhili wa ‘’Women For Africa Foundation’’, Serikali na mtekelezaji wa mradi yafutayo yametekelezwa:Serikali imechangia Tshs. za Kitanzania Million moja (1,000,000/=) kupitia ofisi ya mkurugenzi wa wilaya ya kisarawe kama mkopo kwa kikundi cha kina mama Green Voices (Cassava Women Group Kitanga) pesa hizi zilitumika kuanzisha shamba la kikundi lenye ukubwa wa nusu ekari lililopandwa muhogo.

CHANGAMOTO

Pamoja na mafanikio hayo, lakini hawana soko la uhakika la bidhaa zao badala yake wanatembeza vichwani na mkononi hali inayowakatisha tamaa wakinamama.

Sehemu kubwa ya eneo la mradi halijapimwa na ni gharama kubwa kupima, tatizo la maji nalo ni sehemu ya changamoto inayowakumbwa, barabara za kuelekea ulipo mradi si nzuri, kipndi cha mvua haipitiki kabisa, hawana vitendea kazi vya kisasa vya kutosha kukidhi mahitaji yao ya kuchakata na kusindika unga wa muhogo safi na salama ili kukidhi mahitaji ya walaji, umeme haba ni tatizo jingine kwao.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo akifurahia uzinduzi wa jengo la Kituo cha mafunzo ya kilimo cha muhogo (Cassava Palace). Kushoto ni Mtekelezaji wa mradi wa Green Voices, Abiah Maghembe na kulia ni Mlezi wa mradi huo, Balozi Getrude Mongela. Picha na Sidi Mgumia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.