NI KARAHA YENYE IKRAHI INAYOCHEFUA MOYO

Rai - - MBELE - MUDHIHIR MUDHIHIR Mudhihir M. Mudhihir, Kalamu ya Muungwana.

MASALAALE! Huu kama si uzushi ni kitu gani basi! Ati stara inayomletea mtu staha akasitirika nayo ibebe karaha yenye ikrahi inayochefua moyo hadi kutapisha vya tumboni! Basi hii ndoa ya karaha na stara ikauteka nyara ufahamu wangu kwa kiwango kikubwa. Kumbe si kila usilolifahamu basi halo halipo. Mengi tusiyoyajua kwa kuyaona, kuyasikia na kuyaonja hayo yapo tele. Upo hapo au upo upo tu?

Stara huhifadhi neema macho ya wivu wa choyo yakaingiwa kiwi yasione. Stara huficha aibu ya mtu hadi wenye pekepeke na mambo yasiyowahusu wakishindwa kupekechua. Mapazia madirishani na milangoni si pambo ni stara. Vyumba ndani ya majumba na vijumba si fasheni, kanuni na sheria bali navyo ni stara. Na mtu akivaa vizuri akapendeza si utanashati peke yake, bali husitiri na viletavyo karaha machoni mwa watu. Karaha si kitu cha kukifumbata kiganjani. Karaha ni kadhia ambayo athari yake kubwa kwa mwanadamu ni kuchefua moyo. Ni kadhia ambayo inaweza ikayageuza macho, au ikachoma masikio, au ikazizimisha mwili. Kumbe karaha ikidhibitiwa ili isionekane kwa macho, au isijipenyeze puani, au isigonge masikioni hiyo huwa si karaha tena? Mjadala hu unalenga kutushawishi tukubali kuwa stara inaweza kuficha karaha?

Ikiwa tunatamani kwelikweli kuamini kwamba stara inaweza kuisitiri karaha kama ifanyavyo kwa aibu, tunatamani pia kuamini kwamba karaha isitiriwe badala yakuepukwa? Uchafu ukifunikwa kwa kawa iliyopambika hapo tunaupamba uchafu upambike au tunalichafua pambo lichafuke? Hivyo rihi ya uvundo ikinyunyiziwa manukato hugeuka ikanukia waridi? Hapa ndipo nilipokuja kutanabahi kuwa “ahaa, kumbe stara kusitiri karaha ni karaha yenye kukirihisha!”

Utamuona mtu ana akili zake amefanya tendo la fedheha inayofedhehesha kwelikweli, kakilaza kichwa chake begani mwake akiwarai watu ati wamsitiri mambo yasifike barazani. Mtihani huu kwa kauli iliyosahihi kabisa ni “karaha ya stara.” Kwa wenye roho za kiungwana hutokea tena kwa nadra wakamvika nguo aliyekutwa uchi. Bali nijuavyo mimi pengine hata wewe pia, mtu hujivika stara mwenyewe. Aliyeinyea kocho maadamu si muwele aifue mwenyewe.

Namshukuru Mungu mimi na wenzangu tumepata baba anayetambua karaha na stara. Anasema wale wanaojistiri kwa stara wapewe raha wanazostahiki na wale wanaoendekeza karaha wasifanyiwe mzaha mzaha kwani huo hutumbua usaha. Dhamira ya baba mwenye nyumba inatekelezeka ikiwa tutashikana mikono katika kukataa kutoa stara kwa karaha. Kwa hakika, karaha haistiriwi bali huondoshwa.

Wapo waliyoumbwa na huruma wasemao kuwa eti asiyeweza kustahamili basi astahamiliwe. Ni sawa lakini hadi lini? Na baadhi yao huongeza kuwa kutenda kosa si kosa bali kurejea kosa. Wengine wanauliza kuwa anayefanya kosa la kukanyaga moto anataraji nini zaidi ya kuungua papo hapo? Na wengine sijui ndiyo karaha au stara wanasema kuwa hili si jambo la kuoneana haya maana muonea haya mke ndugu hazai naye.

Kalamu ya Muungwana haina cha kuongeza wala kupunguza katika hoja za hapo juu. Bali kama dhamira ya baba mwenye nyumba yetu tunaiunga mkono, basi kila mmoja akatae kustiri karaha. Inawezekana tukikubali kuwa kijinga na kijinga ndipo moto uwakapo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.