Chadema yafuta wakuu wa mikoa, wilaya

»Yatumia miaka 25 kujipanga upya

Rai - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimezifuta nafasi za wakuu wa mikoa na wilaya kwa lengo la kurudisha mamlaka na maamuzi yanayohusu mustakabali wa nchi kwa wananchi.

Uamuzi huo wa Chadema umekuja baada ya kuhuisha sera zake za kitaifa baada ya miaka 25 ya tangu kuasisiwa kwake.

Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi wa sera zao mwanzoni mwa wiki hii, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema lipo jambo linalowapa utofauti mkubwa kati yao na chama kilichopo madarakani ni mfumo wa utawala uliopo nchini kwa sasa.

Alisema mfumo huo ni moja ya sababu ya kukwama kwao kuijenga demokrasia ya kweli juu ya Taifa letu na kwamba anaamini madaraka mengi yamewekwa kwa Rais na kwa Baraza la mawaziri.

“Chochote cha maana kinachohusu nchi yetu kinaamuliwa na makao makuu, aidha ni Dar es Salaam ama Dodoma.

“Kwa hiyo watawala wetu wanakuwa wanahodhi maamuzi yote yanayohusu mustakabali wa nchi yetu. Na Rais mwenyewe amekiri kuwa kazi yake ni ngumu mno. Kila uamuzi wa mwisho wa nchi hii unamtegemea Rais, hata huyo mtu angekuwa malaika, atafika mahali atashindwa.

“Mataifa mbalimbali duniani yamekuwa na utaratibu wa kugatua madaraka, kupeleka mamlaka kwa watu, si kukusanya madaraka kwa watawala, wenzetu wa Kenya wamefanya mabadiliko ya Katiba, wamefanya mfumo wa kugatua madaraka, wakaanzisha serikali za majimbo ambazo zina uwezo wa kufanya maamuzi kuhusu rasilimali na watu waliopo katika eneo lile. Kenya ukubwa wake ni nusu ya Tanzania.

“Tuna nchi kubwa na sisi ndani ya chama chetu, tumetengeneza sera za ndani ya chama zinazotambua uwapo wa majimbo 10 ndani ya nchi yetu, mawili yakiwa Zanzibar na nane Tanzania Bara.

“Ni lazima tufike wakati tukubaliane, viongozi wa kisiasa katika nchi hii, wasiwe wa kuteuliwa, wawe ni viongozi wa kuchaguliwa na wananchi, kwa kura za wananchi, kwa sababu tabaka kubwa la viongozi wanayoyumbisha nchi yetu, usalama wa raia, uhuru wa raia ni hawa watu wanaoitwa ma RC na ma CC, ambao hawawajibiki kwa wananchi, wanawajibika kwa waliowachagua.

“Chini ya mfumo wetu wa utawala wa majimbo, viongozi wote wa kisiasa utachaguliwa na wananchi kama ilivyokuwa kwenye nchi mbalimbali duniani, utawala unashusha mamlaka chini, watu wanajiongoza wenyewe…”

MAMBO MATATU MUHIMU

Sera mpya ya chama hicho imejikita kwenye mambo matatu muhimu ambayo ni uhuru wa watu, uchumi na huduma za jamii.

Hii ni mara ya pili cha Chadema kutangaza sera zake za Kitaifa, sera ya kwanza ya chama hicho ilianza kutumika mwaka 1993, ikiwa ni miaka miwili kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995.

Chama hicho, kimeiboresha tena sera yake hiyo ikiwa ni miaka miwili kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Pamoja na chama hicho kuangalia mambo matatu muhimu, lakini pia maeneo hayo yametazama maeneo 12 ya kimkakati.

Alisema wametumia mwaka mzima kufanya tafiti, kukusanya mawazo kutoka kwa watu mbalimbali wakiwamo wataalamu.

Pamoja na mambo mengine, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai alisema sera hiyo itakuwa ikifanyiwa marekebisho kulingana na wakati.

Alisema eneo la kwanza ya sera hiyo, ni ile inayohusu uhuru wa watu, ambapo hata Mwalimu Julius Nyerere alipata kuzungumzia suala la maendeleo ya watu.

“Hili la maendeleo ya watu tumelifafanua vizuri kwenye sera zetu, kwa sababu watu wakiwa na maendeleo automatically maendeleo ya vitu vitakuja vyenyewe lakini ustawi wa watu ndiyo unaanza kwanza.

“Pia maeneo yanayotoa haki za msingi, je katiba inakidhi matamanio ya walio wengi? Kwenye utawala wa sheria, kuna mihimili mitatu je kila mhimili ni namna gani uko huru,”alihoji Mbowe.

Alitaja eneo la pili ya sera hiyo kuwa ni zile zinazolenga misingi ya uchumi.

“Katika eneo hili tumeainisha ni kwa namna gani wananchi wanapata huduma za kijamii, namna uchumi utakavyokuwa endelevu badala ya kuhodhiwa na Serikali.

“Huduma za jamii haziwezi kuwa endelevu kama kuna uchumi usiokuwa imara na si uchumi hodhi bali ni ule unaoheshimu uwekezaji wa ndani nje ya nchi,”alisema.

Alitaja eneo jingine la sera hiyo kuwa ni linalolinda na kuihuisha jamii kupata huduma ya maji na barabara.

“Yasiwe mambo yanayofanywa na sekta binafsi bali yafanywe na Serikali. Haya mambo lazima yasimamiwe na Serikali kwa sababu sasa kumejengeka dhana kuwa Serikali ikijenga shule, zahanati, barabara inakuwa ni zawadi kutoka kwa Serikali au CCM hii ni haki ya msingi ya wananchi na si msaada,”alisema.

Kutokana na hilo, Mbowe alisema anakaribisha Serikali iliyoko madarakani kunakili sera zao kwa yale ambayo wataona yanawafaa lakini wawe na ujasiri wa kukiri kuwa ni sera ya Chadema.

“Tunawakaribisha walio madarakani wa-copy yale ambayo wataona yanawafaa lakini wawe na ujasiri wa kutushukuru, wasione aibu kuja kwetu kwa sababu siku zote kitu cha kuchakachua unakuwa huipati vizuri hivyo waje tutawasaidia,”alisema.

Pia aliwataka Watanzania, wanazuoni kuzisoma sera yao hiyo mpya na kuzichambua ili waweze kupata maoni yao.

SABABU ZA KUTOA SERA

Mbowe alisema wameamua kutoa sera ya namna hiyo kwa sababu hawaoni mafanikio ya watu kama taifa kwa sababu ilisababishwa umasikini wa kifikra.

Alisema uchumi wa kijamaa ulikuwa na tatizo kubwa kwamba kiongozi mzuri ni yule ambaye ni maskini jambo ambao si sahihi.

Katika hilo, alisema Chadema inaamini katika mafanikio ya mtu mmoja mmoja ambayo yanatengeneza mafaniko ya taifa kwa ujumla.

“Umaskini si sifa ni laana, huu ni ugonjwa mkubwa wa taifa letu… Eti kiongozi wa watu lazima awe masikini, sisi Chadema tunakataa, tunaamini kiongozi ni yule mwadilifu, mwaminifu.

“Lazima tujikite katika kunyanyua uwezo wa watu, tuwasukume kutafuta mali kukuza uchumi wa taifa zima,”alisema Mbowe.

MASHINJI

Naye Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji, alisema wametumia mwaka mmoja kufanya utafiti kuandaa sera hizo.

“Tulijiuliza maswali kadhaa kwamba; je tupo njia sahihi kama taifa? Uchumi wa taifa letu uko vizuri? Pia tukaangalia tuna vikwazo gani kama taifa.

“Pamoja na yote hayo sisi Chadema tunaamini haijalishi unatoka wapi, una rangi gani kikubwa tunamwangalia mtu ambaye ana mchango kwa maendeleo ya watanzania ndiyo maana hatuna shaka kabisa kuwa na uraia pacha,”alisema.

Dk. Mashinji alisema hakuna mkakati wowote ambao umeandaliwa na Serikali kuhusu viwanda.

SUMAYE

Akitoa neno la shukrani baada ya uzinduzi huo, mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye aliipongeza sera hiyo akisema hata CCM haijapata kutoa sera ya hiyo.

Alisema wakati akiwa CCM pale wanapotoa sera inaishia kwenye Kamati Kuu ya chama lakini haipati mawazo ya watu wengine kama amvayo Chadema imefanya.

Akigusia baadhi ya maeneo ya sera hizo, Sumaye alisema kama serikali haijaweka sera na kama uchumi umeelemewa haiwezi kuzungumzia kuhusu viwanda.

“Huduma za jamii ni product za uchumi, hujaweka sera na uchumi uko vibaya halafu unazungumzia viwanda ndio vile inaishia mtukuwa cherehani nne eti ni viwanda,”alisema Sumaye.

Maeneo muhimu 12 ya misimamo ya kisera yaliyoanishwa na chama hicho ni pamoja na Katiba, utawala, uchumi wa soko jamii, siasa za ndani, siasa kijamii, elimu na sayansi, afya, usimamizi wa ardhi, kilimo, miundombinu, mazingira na mambo ya nje.

Uzinduzi huo umehudhuriwa pia na mwakilishi kutoka ubalozi wa Marekani nchini, Nigeria, mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), wanaharakati na viongozi waandamizi wa chama hicho.

UZINDUZI: Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (katikati) na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji wakizindua Sera ya chama ya Mwaka 2018, Dar es Salaam jana. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu. Picha na Fidelis Felix

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.