Wasomi watoa suluhisho

»Wasema kujiuzulu si tiba

Rai - - MBELE - NA WAANDISHI WETU

Kwa kuwa zipo nadharia kadhaa zilizosababisha ajali, kwa mfano kivuko kujaza abiria na mizigo kuliko uwezo wake, hilo ni la kushughulikia na kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi.

AJALI za mara kwa mara za majini zinazoikumba Tanzania kwa takribani miaka 22 sasa zimewaibua wasomi, ambao wameamua kujikita kwenye kutoa suluhisho la ajali hizo na si kulaumu kama zinavyofanya baadhi ya kada.

Hatua hiyo imekuja baada ya kivuko cha MV Nyerere kilichokuwa kikifanya safari zake kutoka Bugorora na Ukara, jijini Mwanza, kuzama mwishoni mwa wiki iliyopita, ndani ya Ziwa Victoria.

Ajali hiyo ambayo inadaiwa kuua watu zaidi ya 200 na kiasi kikubwa cha mizigo kupotea, inafanya idadi ya ajali kubwa za majini kufikia nne katika kipindi cha miaka 22.

Ajali ya kwanza kuchukua uhai wa watu wengi na kiasi kikubwa cha mizigo, ilitokea ndani ya Ziwa Victoria ikiihusisha meli ya MV. Bukoba iliyokuwa ikifanya safari zake kati ya Mwanza na Bukoba.

Ajali hiyo iliyotokea Mei 21, 1996 inakadiriwa kuchukua roho za watu zaidi ya 800 na kiasi kikubwa cha mizigo kikiteketea, huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni kuzidisha abiria na mizigo.

Septemba 10, 2011, Tanzania ilirejea tena kwenye majonzi baada ya kutokea kwa ajali ya majini safari hii ikihusisha meli ya Mv Spice Islander iliyokuwa na uwezo wa kubeba abiria 605 na tani 500 za mizigo.

Hata hivyo, meli hiyo iliyokuwa ikifanya safari zake kati ya Unguja na Pemba, ilikadiriwa kubeba zaidi ya abiria 800 na kiasi kikubwa cha mizigo kuzidi uwezo wake, hatua iliyosababisha kuzama kwenye mkondo wa Nungwi ikitokea Unguja kwenda Pemba na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 240.

Mwezi Julai, 2012 Tanzania ilizama tena kwenye majonzi baada ya meli ya MV Skagit iliyokuwa ikifanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Zanzibar, kupata ajali iliyodaiwa kusababisha vifo vya zaidi ya watu 50 na kiasi kikubwa kwa mizigo.

Meli hiyo iliyokuwa na uwezo wa kubeba abiria 300 na tani 26 za mizigo, ilidaiwa kuzama katika eneo la Chumbe kutokana na kudaiwa kubeba idadi kubwa ya watu na mizigo.

Ajali zote hizo ziliisukuma serikali kuchukua hatua kadhaa za kuzikomesha ikiwa ni pamoja na kuunda Tume, Kamati pamoja na kununua meli mpya, lengo likiwa ni kudhibiti ajali za namna hiyo.

Hata hivyo, miaka sita baadae imeibuka ajali ya MV Nyerere, ambayo mazingira ya tukio zima yanarandana kwa karibu na ajali zote zilizotangulia.

Hatua hiyo imewaibua baadhi ya wasomi ambao katika mazungumzo yao na RAI, wameweka wazi kuwa sasa inatosha kwa mamia ya Watanzania kupoteza maisha kwa ajali za majini na badala yake ni vema suluhisho la kudumu likapatikana na wao wametoa mapendekezo yao.

PROFESA KESSY

Akizungumza na RAI, Mbunge wa zamani wa Bunge la Afrika Mashariki, Profesa Nderakindo Kessy alisema huu si muda wa kunyoosheana vidole kuwa nani anatakiwa kufuata sheria ama kuwajibishwa.

Alisema suala la viongozi kutakiwa kufuata sheria ikiwamo kujiuzulu pamoja na mambo mengine ni suala la kujidanganya kwa sababu Tanzania ya sasa haifuati sheria.

“Ukiangalia kuanzia chini hadi juu hamna anayefuata sheria. Tujiulize Tanzania ya leo tumepiga hatua kufuata sheria au tumezorota? Jibu ni kwamba kila mahali walio wadogo na wakubwa wanavunja sheria. Ni jambo la kujidanganya kumtaka Waziri Mkuu afuate sheria. Huu si muda wa kunyoosheana vidole.

“Hata wale wanaopaswa kusimamia sheria hawana uhuru wa kusimamia sheria, hivyo sioni haja ya kumnyooshea kidole Waziri Mkuu. Kwa kawaida tukiwa kwenye familia wale walio wakubwa ndio huanza kufuata sheria na watoto wanafuata mifano ya wale wazazi. Pia tukiangalia uongozi tulio nao sasa ni wa kufuata sheria? Jibu ni hapana!

“Haya tuliyaona miaka ya 1990, ndio maana ikaundwa kamati ya kudai Katiba mpya (NCCR). Kwamba kasoro zilizoonekana kwenye Katiba ndizo zilizosababisha kuweka uongozi usiofuata sheria, sasa nchi kama inaweka uongozi usiofuata sheria itaweza kusimamia sheria? Alihoji Prof. Kessy.

Prof, Kessy alisema suluhu pekee ni viongozi kufuata sheria kwenye kila jambo ikiwa ni pamoja na kuongeza udhibiti kwenye maeneo yote yanayohusisha wananchi.

PROFESA SHARIFF

Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abdul Shariff alisema suala linalotakiwa kuanza kutekelezwa kwa muda wote ni kudhibiti wingi wa abiria kwenye meli na vivuko.

Alisema licha ya kutokea ajali nyingi zinazoshabihiana na kuzidisha uzito, ajali hizo bado hazijawa funzo kwa viongozi na serikali kwa ujumla.

Alitolea mfano kuwa licha ya kutokea ajali ya meli ya Spice Island na serikali kununua meli mpya kubwa hadi sasa meli hiyo haijaanza kufanya kazi.

“Ni jambo la kushangaza ila tunaweza kuona namna gani serikali inatakiwa kuchukua hatua kuhakikisha idadi ya watu wanaotakiwa ndio wanapanda kwa uzito unaotakiwa.

“Hizo ni hatua za lazima ila isiwe kama Zanzibar ambako wamenunua meli ambayo haifanyi kazi,” alisema.

DK.BANA

Kwa upande wake Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana alisema serikali inatakiwa kujenga mfumo ambao utahakikisha chombo cha majini au nchi kavu na miundombinu yote stahiki inakuwa katika hali inayoruhusiwa.

Pia aliishauri serikali iweke vigezo kwa vivuko vyote kuwa na taratibu za kutambua watu waliopanda na idadi yao kamili.

“Lazima kuwepo na vigezo kama tunavyopanda usafiri wa gari na ndege. Hiyo inakuwa nafuu kidogo, pili hizi mamlaka za udhibiti kama Sumatra, lazima wawe na utaratibu mzuri wa kudhibiti vyombo vya usafiri, mfano jana (mwanzoni mwa wiki hii) nimepanda Kagongo kuelekea Busisi, tulikuwa tunaingia tu hakuna taratibu zozote wala hakuna anayejali kama kuna uzito gani, wakati ajali imetokea kama wiki hakuna anayejifunza.

“Tatu, nadhani hizi tume tunazounda tuhakikishe mapendekezo yanafanyiwa kazi. Kwa mfano kulikuwa na tume za ajali ya Bukoba, Spice island, tunatakiwa kujifunza kutumia matokeo ya yale ambayo yametokea na kujifunza,” alisema.

DK. KAHANGWA

Hoja hiyo pia iliungwa mkono na Mhadhiri mwandamizi wa chuo hicho, Dk. George Kahangwa alisema serikali inapaswa kuchukua hatua za muda mrefu na mfupi.

Alisema licha ya kutokea ajali na watu kupoteza maisha, bado vivuko vinaendelea kutumika na watu wanasafiri.

“Kwa kuwa zipo nadharia kadhaa zilizosababisha ajali, kwa mfano kivuko kujaza abiria na mizigo kuliko uwezo wake, hilo ni la kushughulikia na kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi.

“Elimu ya msafiri ni muhimu sana kwa wasimamizi wote wa vyombo vya usafiri. Pia elimu hiyo itolewe mara kwa mara katika vituo mbalimbali vya kusafiria kama meli, gati za usafiri, au mabasi, kama inavyofanyika kwenye ndege kuwa lazima watoe elimu kuhusu hatua za kuchukua kwa usalama wa abiria.

“Inatakiwa kuwa kama utamaduni wetu, isiwe ndege peke yake. Kwa mfano tiketi za vivuko, zinatakiwa kuwa na namba vilevile, kama ni abiria 100, ukipewa tiketi ioneshe kabisa namba 80 kati ya 100. Kwa mfano suala la maboya nalo linatakiwa kuelekezwa kwa abiria kama ilivyo kwenye ndege. Tuwe na utaratibu wa kuendelea kulinda usalama wa wasafiri,” alisema.

RUNGWE

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), Hashim Rungwe, alisema vyombo vingi vya usafiri wa majini zikiwamo meli na vivuko vimerithiwa kutoka kwa wakoloni hivyo vinatakiwa kufanyiwa ukarabati mkubwa na kununuliwa vingine vipya.

Pia ameishauri Serikali kuhakikisha inavifanyia ukarabati vivuko vyote nchini ikiwamo meli kongwe ya MV Liemba inayotoa huduma katika Ziwa Tanganyika ambayo alidai kuwa imekuwa ikifanya kazi karibu miaka 115 sasa.

Alisema Serikali inatakiwa kununua vivuko vipya na vya kisasa katika maeneo mbalimbali yenye uhitaji ili kuwawezesha wananchi kupata usafiri wa uhakika na wa haraka kama ilivyoamua kununua ndege mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari wiki hii jijini Dar es Salaam, Rungwe pia alitoa salamu za rambirambi kutokana na vifo vya zaidi ya watu 227 waliofariki dunia katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea Septemba 20 mwaka huu.

“Kama pale Ukerewe weka kivuko cha kisasa kinachokwenda hata kwa dakika 45 au saa moja, hata kwa kukopa kwa sababu tunakopesheka sisi tutalipa. Kama Taifa halina fedha likope tununue vivuko tutalipa kwa sababu kwani ni aibu Taifa kudaiwa? Alihoji Rungwe.

Kuhusu udhibiti wa ubebaji wa abiria na mizigo kupita kiasi alishauri kuhakikisha mtu anayekatisha tiketi kuwa na idadi kamili ya watu wanaopanda katika vivuko pamoja na mtu atakayehakikisha mizigo inayopandishwa haizidi uzito unaotakiwa.

Pia alitaka kuimarishwa kwa ulinzi na usalama wa abiria wakati wa kushuka kwa kuwazuia abiria wasisogee kwenye mlango kabla ya kivuko kusimama.

“Mbona kwenye ndege abiria hawasimami kabla haijatua badala yake wanaendelea kukaa na kusikiliza maelekezo ya wahudumu mpaka pale inapotua na kusimama kabisa na kuruhusiwa kushuka.

“Chama chetu pia kinaishauri Serikali badala ya utaratibu wa sasa wa kusubiri matukio ya hatari yatokee ndipo ianze kuwawajibisha watumishi wake inatakiwa ifuate kanuni na taratibu za mfumo mzuri wa utumiaji wa vyombo hivi vya usafirishaji kwa kufuata maelekezo ya waundaji na watengenezaji wa vyombo husika” alisema Rungwe.

Alisema chama hicho kimetoa rambirambi ya Sh 300,000 kama mchango katika kuomboleza msiba huo wa kitaifa.

UCHUNGUZI WA RAI

Mara baada ya kutokea kwa ajali ya kivuko cha MV Nyerere, RAI lilifanya uchunguzi kwenye vivuko kadhaa nchini na kubaini kuwa hakuna udhibiti wa idadi ya abiria wanaotakiwa kuingia ndani ya vivuko vingi. Lakini pia hakuna namna sahihi ya kuzuia abiria wasisogee mbele wakati kivuko kikielekea kutia nanga kwa ajili ya kuwashusha.

Limekuwa ni jambo la kawaida kwa idadi kubwa ya abiria kukimbilia mbele pale tu wanapoona kivuko kikikaribia gati, hatua inayoweza kusababisha uzito kuongezeka kwenye eneo moja hali inayoweza kukibinua.

Imeandaliwa na Gabriel Mushi, Leonard Mang’oha na

Edwin Mkenda (SAUT)

KIVUKO: Kivuko cha MV Nyerere kilichozama, kikiwa kimeibuliwa na kugeuzwa kutoka ndani ya maji na kukaa upande mmoja katika harakati za kukiondoa majini. Picha: Fredrick Katulanda

Dk. Benson Bana

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.