KUTOLIPA MAFAO Taasisi 98 kuburuzwa mahakamani

Rai - - MBELE - NA SAFINA SARWATT, KILIMANJARO

MENEJA Kiongozi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mkoa Kilimanjaro, Jamal Nchula, inakusudia kuziburuza Mahakama taasisi 98 binafsi na za umma kutokana na kushindwa kulipa michango ya wafanyakazi wao kwa wakati.

Taasisi hizo zimeshindwa kutekeleza majibu wao katika kipindi cha Januari hadi Agosti mwaka huu, hatua iliyosababisha kudaiwa jumla ya Sh. milioni 453.

Nchula alisema baadhi ya waajiri walioshindwa kulipa michango ya wafanyakazi kwa wakati mbali ya kutowatendea haki wafanyakazi wao, lakini pia wanakwamisha utendaji kazi wa mfuko huo.

“Baadhi ya waajiri wanachelewesha michango ya wafanyakazi, hilo linatukwamishi sisi kutoa huduma bora kwa wateja wetu ambao ni waaminifu, “alisema.

Kwa upande mwingine alisema hadi kufikia sasa zaidi ya kesi 300 za madai zimefunguliwa na wanachama tangu kusitishwa kwa fao la kujitoa.

Hatua hiyo imekuja baada ya Bunge kufunga hoja kuhusu malipo ya mafao ya kujitoa kwa kupitisha Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) yenye mafao ya kukosa ajira.

Sheria hiyo ambayo ilianza kutumika Agosti mosi mwaka huu imeunganisha mifuko minne ya PSPF, LAPF, PPF na GEPF na kuunda mmoja (PSSSF).

Agosti 17, Waziri Jenista Mhagama mwenye dhamana ya kazi na ajira nchini alisaini kanuni za Sheria ya Hifadhi ya Jamii kuruhusu kuanza kutumika kwake.

Kwa mwanachama atakayeachishwa kazi, kanuni zinasema atalipwa fao la kutokuwa na ajira ambalo ni sawa na theluthi moja (asilimia 33.3) ya mshahara aliokuwa anapokea akiwa kazini.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi, Meneja Kiongozi wa NSSF -Mkoa Kilimanjaro, Jamal Nchula alisema baadhi ya wanachama bado hawajapata elimu ya kutosha kuhusu sheria hiyo mpya.

Alisema wanachama wengi wanaamini kuwa mifuko wa hifadhi ya jamii ni kama vyama vya kuweka na kutoa fedha zao kama ilivyo (Saccos).

Alifafanua zaidi kuwa wafanyakazi wengi hawana uelewa juu ya mabadiliko hayo ya sheria hali inayochangia kuwepo kwa malalamiko kuhusu mafao ya kukosa ajira pale ajira zao zinapokoma kwa sababu yoyote ile.

Alisema hadi sasa kuna zaidi ya madai 300 ya kujitoa uanachama yaliyofunguliwa na wanachama kabla ya kupitishwa kwa Sheria hiyo mpya ya hifadhi ya jamii ambapo kwa sasa yanasubiri kukamilika kwa kanuni za Sheria hiyo ili kulipa mafao ya kukosa ajira kwa wanachama hao.

Alisema baadhi ya wanachama wa mfuko huo wamesema kuwa tangu mwaka 2016 hawajapewa mafao yao na kwamba mpaka sasa bado hawajapata majibu sahihi.

Waziri Jenista Mhagama

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.