Ni kivumbi nusu fainali Mabingwa Afrika

Rai - - MBELE -

KATI ya timu nne zilizobaki, ni mbili tu ndizo zinazotakiwa kwenda fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na hapo ndipo uliopo utamu wenyewe. Timu zilizotinga nusu fainali ni Al Ahly ya Misri, Entente Setif inayoiwakilisha Algeria, Primeiro Agosto ya Angola au Esperance kutoka Tunisia. Huku mechi za hatua ya nusu fainali zikitarajiwa kuanza kuchezwa Oktoba 2, mwaka

KATI ya timu nne zilizobaki, ni mbili tu ndizo zinazotakiwa kwenda fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na hapo ndipo uliopo utamu wenyewe.

Timu zilizotinga nusu fainali ni Al Ahly ya Misri, Entente Setif inayoiwakilisha Algeria, Primeiro Agosto ya Angola au Esperance kutoka Tunisia.

Huku mechi za hatua ya nusu fainali zikitarajiwa kuanza kuchezwa Oktoba 2, mwaka huu, Al Ahly wataitafuta tiketi ya fainali kwa kumenyana na Setif na Primeiro Agosto watatoana jasho na Esperance.

Baada ya mechi hizo za kwanza, timu hizo zitarudiana wiki tatu baadaye, yaani Oktoba 23, na matokeo ya jumla yataamua zitakazocheza fainali.

Kwa kuanza na mchezo kati ya Al Ahly na Setif, hakuna ubishi hapo patachimbika, ikizingatiwa kuwa klabu hizo zina historia kubwa barani Afrika.

Ikiwa na mataji nane ya Ligi Kuu ya Algeria, Setif imetwaa mara mbili ubingwa wa Ligi ya Mabingwa (1988 na 2014) na mwaka 2009 walitinga fainali ya Kombe la Shirikisho.

Kufika kwao hatua hii hakukuwa kwepesi kwani walilazimika kuwaondoa Waarabu wenzao ambao ni mabingwa watetezi, Wydad Casablanca.

Hiyo ikafuta ndoto za Wydad kuingia katika orodha ya timu tatu pekee zilizowahi kulitetea taji hilo. Nyingine zilizowahi kufanya hivyo tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo ni Al Ahly, TP Mazembe na Enyimba.

Katika mchezo wa kwanza wa robo fainali walipokuwa ugenini nchini Morocco, walilazimisha suluhu, kabla ya ushindi mwembamba wa bao 1-0 walioupata mbele ya mashabiki wao.

Ushindi wao dhidi ya Waydad uliifanya timu huyo kufikisha mechi sita bila kufungwa tangu ilipoanza vibaya katika hatua ya makundi. Hivyo, Al Ahly watakutana na kibarua kigumu mbele ya Waalgeria hao.

Al Ahly ‘Mashetani Wekundu’ nao si wa kubezwa, hasa inapofikia hatua hii. Ni mabingwa wa kihistoria Ligi Kuu ya Misri, wakiwa wamelitwaa taji hilo mara 40.

Kama hiyo haitoshi, timu hiyo yenye masikani yake jijini Cairo imeshinda mara nane Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa ndiyo timu pekee kulitwaa mara nyingi taji hilo.

Katika hatua ya robo fainali, walikutana mara mbili na wababe wa soka la Guinea, Horoya, ambapo mchezo wa kwanza walikuwa nyumbani mjini Cairo na kushinda mabao 4-0, na ule wa marudiano ulimalizika kwa timu hizo kutofungana.

Ukiacha mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa kandanda, vipi kuhusu vita ya Primeiro Agosto na Esperance hiyo Oktoba 2?

Huendawengiwanaichukulia poa Primeiro Agosto kwa kuwa ni mara yao ya kwanza kuingia nusu fainali lakini ni moja kati ya timu ngumu, ikilithibitisha hilo kwa kuwang’oa TP Mazembe katika hatua ya robo fainali.

Mchezo wa kwanza uliochezwa mjini Luanda, Angola, ulimalizika wa timu hizo kutofungana lakini ngoma ilipohamia Lubumbashi, zikatoka sare ya bao 1-1, hivyo Primeiro Agosto ikasonga mbele kwa sheria ya bao la ugenini.

Mabingwa hao mara tano Ligi ya Mabingwa, TP Mazembe, hawatamsahau kipa wa wapinzani wao hao, Toni, ambaye katika mchezo wa sare ya bao 1-1 alizuia penalti ya staa Tresor Mputu na bao la wazi la Ben Malango.

Timu hiyo ni mabingwa mara 12 Ligi Kuu ya Angola na wana uzoefu mkubwa Ligi ya Mabingwa kwani hii ni mara yao ya 11 kushiriki ingawa hawajawahi kuwa mabingwa.

Esperance, ambao ni wamelibeba mara 28 taji la Ligi Kuu ya Tunisia, wanashikilia vikombe viwili vya Ligi ya Mabingwa (1994 na 2011) na pia wamecheza fainali mara nne (1999, 2000, 2010 na 2012).

Kibarua chao kikubwa kilikuwa katika hatua ya robo fainali lakini waliweza kuwasukuma nje ya mashindano Waarabu wenzao wa Tunisia, Etoile du Sahel.

Mtanange wa kwanza uliwashuhudia wakichapwa bao 1-0 ugenini, lakini waliporudi mbele ya mashabiki wao, wakashinda mabao 2-1 na kusonga mbele.

Njaa kubwa waliyonayo mashabiki wa Esperance ni kuiona timu yao ikimaliza ukame wa taji la Ligi ya Mabingwa kwani ni miaka saba sasa imepita tangu walipolinyakua.

Timu Al Ahly ya Misri HASSAN DAUDI NA MITANDAO

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.