Ipo haja ya kuzichunguza taasisi zinazotoa fursa ya kusoma ng’ambo

Rai - - MAKALA - NA HASSAN DAUDI

PASI na shaka uwepo wa taasisi mbalimbali zinazowawezesha Watanzanjia kupata fursa za kwenda kusoma nje ya nchi umekuwa na faida kubwa.

Katika miaka ya hivi karibuni, tumeshuhudia ongezeko kubwa la taasisi zinazofanya kazi hiyo, ambazo kwa bahati nzuri, nyingi zimekuwa zikishirikiana kwa karibu na Serikali.

Hivi sasa, ni suala la kuamua tu, kwani mwanafunzi anaweza kupata elimu yake ya ngazi yoyote, mfano cheti, stashahada, na shahada, katika vyuo vya ndani au vilivyopo nje.

Aidha, wapo baadhi ya wanafunzi wanaolazimika kwenda nje kusoma kwa sababu ‘course’ wanazozipenda hazipo nchini.

Pia, imebainika kuwa kuna baadhi ya wanafunzi wanaokwenda kusoma nje ya nchi hukwepa gharama kubwa za kusoma katika baadhi ya vyuo hapa nchini.

Hivyo basi, inatoa mwanya si tu kwa waliokuwa na ndoto za kusoma nje, pia inairahisishia kazi Serikali katika kukabiliana gharama zitokanazo na ongezeko kubwa la wasomi nchini.

Pia, ni faida kubwa kwa Serikali kwa kuwa baadhi ya wanaokwenda nje husomea ‘course’ ambazo mwishowe huwa na faida kubwa katika utekelezaji wa sera iliyopo.

Mfano; mwanafunzi anayekwenda ng’ambo kusomea masuala ya mafuta na gesi, ni wazi atakuwa na msaada mkubwa katika sera ya Tanzania ya Viwanda.

Hata hivyo, licha ya mchango wa taasisi hizo katika sekta ya elimu, bado zinatakiwa kutupiwa jicho la tatu, kwa maana ya kufuatiliwa kwa kina katika utendaji kazi wake.

Je, ni kwa kiwango gani tunaweza kujiridhisha kuwa hakuna ‘ujanjaujanja’ wa baadhi ya taasisi katika shughuli hiyo nyeti katika maendeleo ya elimu nchini?

Wasiwasi mkubwa ukiwa ni huenda kuna kundi la wafanyabiashara wasio waadilifu wameanzisha taasisi hizo kwa lengo la ‘upigaji’, ipo haja ya Serikali kuongeza umakini.

Licha ya juhudi za Serikali kuhakikikisha taasisi hizo zinasajiliwa, bado ni ngumu kujiridhisha kuwa mfumo wa utoaji huduma una tija kwa walau asilimia 95.

Tuanze na hili la ubora wa elimu inayotolewa na baadhi ya vyuo vya nje ukilinganisha na vilivyopo nchini. Ukweli ni kwamba si tu kwa kuwa ni Marekani, China au Uingereza, basi kila chuo kitakuwa na hadhi ya juu.

Hapo ndipo unapoweza kujiuliza, kama ni hivyo, ni kwa kiasi gani taasisi hizi zina uadilifu wa kutosha katika kukabiliana na vyuo vya ujanjaujanja vilivyopo huko?

Ieleweke kuwa hata katika mataifa hayo, vipo vingi visivyo na ubora, tena vikiwamo vilivyozidiwa na vinavyopatikana Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

Je, taasisi tulizonazo zinakabiliana na hilo kwa kiwango gani? Au kwa kuwa mwanafunzi anataka kwenda kusoma nje, basi ili kuipata fedha yake, atatafutiwa chuo chochote huko ughaibuni?

Kuliweka hilo vizuri , kama ‘course’ anayoitamani mwanafunzi inatolewa kwa kiwango cha juu pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuliko huko Canada, taasisi iko tayari kuweka kando masilahi yake na kumshahuri abaki nchini?

Kwa leo, safu hii ya ‘Macho Yameona’ haina la ziada, ikiwa haina chembe ya shaka kuwa ujumbe umefika kwa mamlaka husika na utafanyiwa kazi kwa masilahi mapana ya sekta ya elimu inayokabiliwa na changamoto lukuki.

Pia, safu hii inatoa rai kwa Serikali kuboresha mfumo wa elimu nchini ili kuepusha idadi kubwa ya Watanzania wanaokimbilia kwenda kusoma nje.

Ifahamike kuwa asilimia kubwa ya wanaofanya hivyo ni kutaka elimu bora, hasa katika masomo ya sayansi ambapo kwa vyuo vya hapa nchini changamoto kubwa imekuwa ni uhaba wa vifaa vya kufundishia kwa vitendo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.