Viundwe vikosi m aalum vya uokoaji majini

Rai - - MAONI/KATUNI -

TULIDHANI kuwa tulijifunza kutokana na ajali ya kuzama kwa meli ya MV Bukoba iliyotokea Mei 21, 1996, ambapo watu zaidi ya 800 pamoja na wafanyakazi 37, walipoteza maisha.

Tokea wakati huo, inaelekea Serikali haijatoa kipaumbele kwa vyombo na watu wanaosafiri katika maziwa yetu makuu — Victoria, Tanganyika na Nyasa, pamoja na wanaotumia usafiri wa boti na meli baharini.

Vyombo vya majini, ni mara chache vimepinduka na kuzama kutokana na dharura itokanayo na hali ya hewa kama vile dhoruba. Hii ni kwa sababu watabiri wa hali ya hewa mara nyingi hutoa hadhari na ikibidi kuwaasa watendaji kuchukua hadhari—kwa maana ya maandalizi ya kukabiliana na hali itakayojitokeza.

Katika tukio la hivi karibuni ililiotokea Ukara, kisiwa ambacho ni sehemu ya Ukerewe, pamoja na kupinduka na kuzama kwa MV Nyerere na MV Bukoba, ni matokeo ya uzembe wa maofisa waliohusika na uangalizi na uendeshaji wa vyombo hivyo.

MV Nyerere ni mfano mbaya ambao tunaweza kusema umetokana na uzembe uliokithiri. Haiwezekani chombo chenye uwezo wa kuchukua abiria 100, kikapakia mara mbili na zaidi ya idadi hiyo! Hata kama maboya ya uokozi yalikuwapo, yasingetosha kwa abiria waliozidi ambao taarifa zinaonesha walikuwa 164 kwea uchache.

Ni wazi kwamba maofisa husika hawakujali usalama wa abiria na mizigo yao — walijali kuingiza kipato zaidi. Na labda huu ndio ulikuwa utaratibu wao wa kila siku. Isitoshe,kivuko hicho kilibeba shehena ya mzigo ambao uzito wake haujatajwa hadi sasa.

Tukiwa bado tuna masikitiko ya kupoteza watu wengi namna hiyo, tunadhani wakati umefika kwa watu wote wenye dhamana na maisha ya watu — wachukue hatua madhubuti ya kuhakikisha kwamba vyombo vyote vya usafiri vinachukua idadi ya abiri iliyoruhusiwa kisheria.

Utaratibu huu uhusike vile na usafirishaji wa abiria — hasa mijini — ampapo watu hujazwa kwenye mabasi kama mihogo. Hili ni muhimu zaidi kwa kuwa litaepusha pia watu kuambukizana magonjwa — hasa wakati huu kukiwa na tishio la ugonjwa wa Ebola.

Lakini pia, tunashauri kwamba wakati umefika sasa kwa Serikali kuanzisha vikosi vya uokoaji katika sehemu zote za maziwa makuu na ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi. Serikali pia iimarishe Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kulipa kipaumbele kwa maana ya vifaa na watumishi wakiojifunza vizuri mbinu za kisasa za uokoaji.

Tanzania inajenga reli ya kisasa SGR ambayo itatumia treni za kisasa za mwendo kasi. Sambamba na ujenzi huo, uende pamoja na mafunzo mahususi kwa vijana watakaosimamia reli hiyo ma treni zake. Pia pawepo mafunzo, ndani na nje ya nchi kwa kikosi maalumu kwa ajili ya uokoaji kikiwa na vituo maalumu katika njia zote.

Tusingoje tukio la kutisha kama hili la MV Nyerere. Kuzuia ni bora kuliko kutibu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.