Kanuni hii ikitumika itapunguza watoto kukaa mahabusu

Rai - - MAONI/KATUNI - NA WILLBROAD MATHIAS

JINSI ya kukamatwa mtoto na vyombo vya dola ni moja ya kanuni ambazo zimeahinishwa katika za Kanuni za Mwenendo wa Mahakama ya Watoto za mwaka 2014 zilizotolewa katika tangazo la Serikali Na. 270 ambalo lilitolewa Julai 25, 2014 na kutafsiriwa rasmi na Ofisi ya Mwanasheria

JINSI ya kukamatwa mtoto na vyombo vya dola ni moja ya kanuni ambazo zimeahinishwa katika za Kanuni za Mwenendo wa Mahakama ya Watoto za mwaka 2014 zilizotolewa katika tangazo la Serikali Na. 270 ambalo lilitolewa Julai 25, 2014 na kutafsiriwa rasmi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ku chapishwa kwa mujibu wa kifungu cha 84 cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria Mbalimbali.

Kanuni hii ya 25 kuanzia kifugu cha kwanza inaeleza hatua mbalimbali ambazo zinatakiwa kuchukuliwa tangu anapokamatwa hadi anapofikishwa mahakamani.

Katika kanuni hiyo inaelezwa kwamba pale ambapo mtoto amekamatwa kwa hati ya kukamatwa, mtoto huyo atapelekwa Mahakamani siku aliyokamatwa, na si zaidi ya siku inayofuatia baada ya kukamatwa kwake, isipokuwa kama kosa ni kubwa.

Mbali na kubainisha hilo, kanuni hiyo inaeleza kuwa mtoto anapokamatwa siku ya Ijumaa baada ya saa za kazi, anaweza kushikiliwa kizuizini mpaka siku ya Jumatatu asubuhi au mtoto anapokamatwa baada ya saa za kazi siku moja kabla ya siku ya mapumziko, mtoto huyo atafikishwa Mahakamani siku inayofuata ya kazi.

Katika kipengele cha tano cha kauni hiyo ndogo kinaeleza pia kuwa pale ambapo haiwezekani kumfikisha mtoto Mahakamani ndani ya saa 24 kama ilivyoelezwa katika kanuni ndogo ya (4) (a)

polisi wataijulisha idara ya ustawi wa jamii ya eneo

ambalo mtoto amekamatwa na baada ya hapo idara ya ustawi wa jamii itashirikiana na polisi kumweka mtoto katika makao yaliyothibitishwa au taasisi au kwa mtu mwenye uwezo mpaka mtoto huyo atakapofikishwa Mahakamani.

Kanuni hiyo inaeleza pia kwamba, endapo mtoto atashikiliwa usiku mzima kwenye kituo cha polisi kwa hati ya kukamatwa, mtoto huyo atapewa chakula na maji ya kutosha, kitanda na mwanga na atawekwa katika chumba tofauti na chumba cha watu wazima.

Piakatikakanunihiyoinaelezwa matumizi ya hati ya kukamatwa mtoto ikifafanua kuwa hati hiyo itaandelea kuwa halali mpaka pale itakapotekelezwa au kufutwa na huku ikifafanua zaidi hati ya mashitaka ambayo inatakiwa kujumuisha maelezo ya kosa mahsusi au makosa ambayo mtoto anatuhumiwa, pamoja na maelezo mengine muhimu ili kutoa taarifa za msingi kuhusu aina ya kosa analoshtakiwa.

Kanuni hiyo inasema pia Mahakama kabla ya kuanza kusikiliza kesi, itahakikisha upande wa mashtaka unampa mtoto au mwakilishi wa mtoto au idara ya ustawi wa jamii nakala ya hati ya mashtaka kwa wakati ili mtoto aweze kuandaa utetezi wake na kwamba pale ambapo mtoto haelewi lugha ya Kiingereza au Kiswahili,Mahakama itahakikisha kuwa hati ya mashitaka na maelezo ya mashtaka yanatafsiriwa katika lugha inayoeleweka kwa mtoto.

Hata hivyo pamoja na kanuni hizo kuweka wazi misimgi mbalimbali ya kumuhudumia mtoto ambaye amejikuta akiwa katika ukinzani wa sheria, wadau wengine bado wanaona bado hazifuatiliwi vilivyo kama zinavyoolekeza.

Chama Cha Wanasheria Tanzania TAWLA ni kati ya wadau hao ambao pamoja na mambo mengine wanasema kwamba bado kuna mazimgira magumu katika maeneo mengi na ukiukwaji wa kanuni hizo wanapokuwa wanashikiliwa watoto.

Katika uchunguzi wao wanasheria hao wanaeleza kuwa mfano wa maeneo hayo ni kama vituo vya polisi ambavyo wanadai si si sehemu zinazojali watoto na mara kwa mara hunyimwa fursa ya kutoa taarifa kuhusu vitendo vya ukatili.

TAWLA wanasema kwamba mbali na vituo vya polisi matukio ya ukatili yanayofikishwa mahakamani huchukua muda mrefu kabla hayajasikilizwa na hata pale kesi zinapofikia hatua ya hukumu, watoto na familia zao mara nyingi hushindwa kusafiri umbali mrefu hadi mahakamani kusikiliza hukumu, na kusababisha kesi kufutwa na wahusika wa ukatili kuachiwa huru.

“Mahakama za watoto zinapaswa kusikiliza kesi za watoto wanaotuhumiwa kisheria hata hivyo kuna mahakama chache za watoto nchini. Kuna uhaba mkubwa wa wanasheria wa watoto. Ucheleweshaji wa kesi kwa muda mrefu hufanya watoto wanaotuhumiwa kwa makosa wakae mahabusu kwa muda mrefu,”wanasema wanasheria hao.

TAWLA wanasema katika tafiti ambazo wamekuwa wakizifanya katika mahabusu, asilimia 30 ya watoto waliokuwa wanashikiliwa walieleza kufanyiwa ukatili na unyanyasaji wakiwa mikononi mwa polisi, maofisa wa magereza na mahabusu wenzao.

Wanasheria hao wanasema kwamba watoto wanakuwa katika hatari zaidi pale wanapowekwa mahabusu pamoja na watu wazima.

Wanasema katika kipindi cha mwaka 2011, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ilikadiria kwamba zaidi ya watoto 1400 walikuwa katika mahabusu ya watu wazima, asilimia 75 ya watoto hao walikuwa wakisubiri kufunguliwa mashtaka.

TAWLA wanasema watoto wanaweza kukaa mahabusu kwa miaka miwili wakisubiri kabla ya kusikilizwa kwa kesi zao.

“Idadi kubwa ya watoto walioko mahabusu ni wale waliofanya

makosa madogomadogo, waliokuwa wakiishi mitaani au

wafanyakazi wa ndani wanaotuhumiwa na waajiri wao. Watoto

hao wako mahabusu kwa kukosa mtu wa kuwajali , wala sio kwa

sababu ni watu hatari au wamefanya kosa lolote kubwa,”wanasema watalaamu hao wa sheria wanawake.

Wanaeleza kwamba zipo njia chache mbadala ya ile ya kuwaweka watoto mahabusu ya watu wazima kuna jela moja tu ya watoto waliohukumiwa na mahabusu tano za watoto kwa upande wa Tanzania.

Wanasheria haoa wanasema kwamba njia nyingine mbadala zilizoko hazitilii maanani urekebishaji wa watoto .

“Kwa mfano, Tanzania bara bado inatumia viboko kama adhabu”. Kuna umuhimu mkubwa wa kufanyia sheria marekebisho ili kesi za watoto ziweze kushughulikiwa mapema na kupunguza kiwango cha watoto wanaohukumiwa adhabu ya kifungo,”wanasema wanasheria hao.

TAWLA wanasema lengo la Kanu ni hizi ni kuanzisha mfumo wa Utendaji na mwenendo unaowiana wa Mahakama za Watoto za Tanzania Bara na kuhakikisha kuwa haki za mtoto chini ya sheria zinazolindwa.

Wanasema kanuni hizi inaelezwa wazi kwamba Mahakama katika kutekeleza mamlaka yoyote yaliyotolewa kwake chini ya Kanuni hizi au katika kutafiti kanuni yoyote, itazingatia lengo la Mahakama ya Watoto.

Kila Mahakamaya watoto chini ya Sheria hii inatambulika kwa jina lake mahsusi na mahali au eneo.

“Mbali na hilo kanuni hizo zinaeleza jinsi mambo kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na Jengo la Mahakama ya mtoto linavyotakiwa kuwa, mazingira, Mazingira ya Mahakama, Uendeshaji wa mashauri, Lugha ya Mahakama, Masharti ya wakalimani, Kuendesha kesi kwa faragha na Uamuzi kuhusu umri,”wanasema wanasheria hao.

Wanasema kwamba licha ya Wizara ya Sheria na Masuala ya Katiba kuandaa mkakati wa kimashirika wa miaka mitano wa kuupa uwezo mfumo wa sheria ili ushughulikie vizuri zaidi watoto waliotendewa ukatili na wale wanaowatendea watoto ukatili na kuwapo kipengele muhimu katika mchakato wa mabadiliko ni uanzishwaji wa Dawati la polisi la Jinsia na Watoto, lakini changamoto ni nyingi kutokana na mazingira ya vituo vingi vya polisi yalivyo.

TAWLA wanasema kwamba katika vituo hivyo vya polisi wanastahili kuwapo muda wote maofisa waliopewa mafunzo stahiki kwa lengo la kuhakikisha kwamba watoto wanahudumiwa ipasavyo bila kujali kama ni watendewa au watuhumiwa wa kosa kutokana na kwamba vituo hivyo vinahusiana na mifumo ya ulinzi wa mtoto na

Wanasema kwa kuzingatia mambo hayo, idadi ya watoto walioko mahabusu itapunguzwa kupitia programu za wananchi za urekebishaji watoto ambazo zitawezesha watoto wanaotuhumiwa au wenye makosa kubakia kwenye familia zao.

“Programu ya msaada wa sheria kwa watoto pia inatakiwa kutekelezwa ili kuhakikisha kwamba watoto wanatetewa, hawawekwi mahabusu kiholela na wale watakaopelekwa mahabusu hawatabaki huko kwa muda mrefu,”wanasema TAWLA.

Wnasema aidha, uandaliwe utaratibu ambao utatoa fursa ya kuendesha mahakama ya watoto kwa njia ya kuzunguka nchi nzima ili kushughulikia kesi za watoto, ili kuhakikisha watoto waliopo mahabusu ama jela wanalindwa na taratibu na sera nzuri.

Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Wanawake TAWLA, Tike Mwambipile akizungumza katika moja ya mikutano hiyo ya chama hicho.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.