AJALI YA MV NYERERE Hakuna sababu ya kuendelea na makosa

Rai - - WIKI - NA HILAL K SUED

Kwanza kabisa napenda kuungana na wananchi wenzangu na watu wengine kwa kutoa pole kwa wote wale waliopoteza ndugu, jamaa na maswahiba wao katika ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere wiki iliyopita.

Baada ya hayo ni vyema niingie moja kwa moja kwenye mada kuu ya makala hii. Ni stori ilele – watawala wetu wanaendelea kufanya mambo yale yale, yanatokea makosa yale yale bila ya hata ya kujifunza chochote.

Sote tukiri kwamba katika ajali ya MV Nyerere kulikuwapo na ucheleweshaji mkubwa kwa upande wa serikali uliotokana na uzembe hadi kupelekea watu wengi kufa. Wanasiasa wakilisema suala hili lililo wazi na ukweli kabisa huambiwa wanatafuta kiki za kisiasa.

Nadhani si sahihi wakaambiwa hivyo kwani kwa taifa kuhuzunika na kutafakuri vyanzo vya ajali hakuwezi ukawa mtaji wowote wa kisiasa, ni kukumbushana tu kila pale makosa yanapotokea – kwa lengo jema la kuzuia kujirudia kwa majanga ya aina hii na kuepusha vifo.

Katika ajali za aina hii (za kuzama vyombo vya majini) ile ya MV Bukoba miaka 22 iliyopita masuala mawili makuu hujitokeza na ambayo hujirudia mara zote: kujaza kwa abiria na mizigo katika vyombo husika kupita uwezo wake, na kuchelewa, au niseme kusuasua kwa utawala kupitia mamlaka zake husika katika kutoa huduma za uokoaji.

Na katika majanga yote haya yanayotokeda uwajibikaji kwa viongozi wakuu wa serikali na watendaji wakuu wa taasisi husika, au uwajibishwaji wao kutoka mamlaka za juu huwa haupo, au kama upo ni kwa kiwango kidogo sana. Katika hili nitatoa mifano miwili kuhusu yanavyotokea kwa wenzetu katika nchi nyingine.

Miaka sita baada ya kuzama kwa MV Bukoba, aliyekuwa rais wa Senegal, Abdoulwaye Wade mara moja alimfukuza kazi Waziri Mkuu wake Bi Madior Boye na baraza lake lote la mawaziri kwa kuchelewesha kutoa huduma za uokoaji wa abiria wa meli ‘MV Joola’ (iliyokuwa ikimilikiwa na serikali) iliyozama pwani ya nchi hiyo September 2002 ambapo watu 1,863 walipoteza maisha.

Kosa lao jingine la vigogo hao wa serikali ni kushindwa kusimamia kanuni za usafiri majini, kwani meli hiyo ilibeba zaidi ya abiria 2,000 wakati ilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,000 tu, na ilidaiwa nusu ya abiria waliokuwamo hawakuwa na tiketi.

Na Aprili 2014 Waziri Mkuu wa Korea ya Kusini Chung Hong-won alijiuzulu wadhifa wake kutokana namna serikali yake ilivyosimamia zoezi la uokoaji wa abiria wa feri iliyozama pwani ya kusini ya nchi hiyo na kuua watu zaidi ya 300. Alichukua hatua hiyo baada ya hasira na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.

Tanzania haina utamaduni kama huo – kwa vigogo wa serikali na mashirika yake kujiuzulu kwa hiari kama itikio la kuzingatia uwajibikaji katika nafasi zao. Viongozi wetu wamezoea kung’ang’ania madarakani hata pale wanapokumbwa na kashfa nzito, au pale tukio kubwa la kufedhehesha, kuchukiza, kuhuzunisha au kuumiza jamii linapotokea chini ya himaya zao.

Kwa kifupi, kujiuzulu kwa hiari kama itikio la kuzingatia uwajibikaji ni kipimo mwanana cha utumishi uliotukuka wa kiongozi yeyote anayeuuchukulia wadhifa wake kama dhamana tu aliyokabidhiwa na umma, na siyo mali yake.

Kwa bahati mbaya sana wapo watu miongoni mwetu wanaohoji vipi kiongozi au mtendaji mkuru ajiuzulu wadhifa wake kutokana na tukio la ajali au kashfa iliyotokea katika himaya yake, wakisema kwani yeye hakuhusika moja kwa moja.

Mara tu baada ya kuzama kwa MV Bukoba kulikoua zaidi ya watu 1,000 kulitokea wito kwa aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi William Kusila na Mkurugenzi Mkuu wa lililokuwa Shirika la Reli (TRC) Limford Mboma kujiuzulu. Idara ya Usafiri wa Majini ya Shirika hilo (TRC Marine Department) ndiyo lilikuwa likisimamia usafiri wa meli hiyo.

Walikataa kujiuzulu na kulikuwapo baadhi ya watu waliowaunga mkono kwamba walihusika vipi – kwani hata hawakuwamo ndani ya meli!

Na kama vile kiburi chake kile hakikutosha, mkuu huyo huyo wa TRC aliendelea kuwa madarakani hata pale zaidi ya watu 300 kupoteza maisha baada ya treni ya abiria waliokuwa wakisafiria kurudi kinyume-nyume kwa kasi na kuanguka karibu na Dodoma mwaka 2002.

Hii inaonyesha kitu kimoja – kwamba viongozi wetu bado hawaelewi maana ya kuwajibika na hivyo wanashindwa kukumbatia tabia ya kimaadili ya kujiuzulu

baada ya kashfa kubwa kutokea chini ya himaya zao ambazo huziumiza sana jamii.

India ni miongoni mwa nchi chache duniani ambazo zina utamaduni uliotukuka kwa viongozi wa juu wa nchi kujiuzulu mara moja kuonyesha uwajibikaji kwa kile kibaya kinachotokea chini ya maeneo yao.

Mwaka 200 waziri wa Usafiri wa Reli wa India, Bi Mamata Benarjee alimwandikia barua ya kujiuzulu kwake kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Atal Behari Vajpayee baada ya treni ya mizigo kuanguka katika Jimbo la Punjab na kuua watu 46 na kujeruhi wengine zaidi ya 150. Fikiria – waziri husika anaandika barua ya kujiuzulu baada ya treni kuanguka kilometa 1,000 mbali na alipo.

Turejee kwa yanayotokea hapa kwetu. Inashangaza hadi ninapoandika makala hii hakuna waziri yoyote aliyeandika kwa rais barua ya kujiuzulu kutokana na tukio la kuhuzinisha la kuzama kwa MV Nyerere.

Siku zote utawala wa Rais John Magufuli umekuwa ukiwahimiza watendaji wake wakuu wakiwemo mawaziri kusimamia kwa ukaribu sana (micromanagement) masuala chini ya maeneo yao ili kuleta ufanisi wa hali ya juu katika uendeshaji wa utawala.

Lakini kuzama kwa MV Nyerere kumeonyesha bado kuna udhaifu mkubwa katika usimamizi huo wa karibu kwani haiingii maanani iwapo waziri Kamwelwe alikuwa hajui suala la ujazaji wa abiria na mizigo kupita kiasi katika safari za meli hiyo. Na kama alikuwa hajui, basi hakika haendani na kasi ya Rais Magufuli. Na kama alikuwa anajua, je, alifanya nini kukomesha hali hiyo?

Na tunapokuja kwenye suala la uokoaji, hapo ndipo bado tuna changamoto kubwa sana. Vyombo husika, kama vipo, ama havijui wajibu wake katika kukabiliana na hali husika, au havina zana hitajika. Na hali hii hujitokeza takriban katika kila janga linalotokea – hususan ajali hizi za majini (na zile za mioto) ambapo uokoaji maisha ya watu hautakiwi kucheleweshwa. Ni kama vile hatujui kabisa abc za uokoaji maisha ya watu.

Mwezi Julai 2012 meli ya MV Skagit iliyokua imetoka Dar es Salaam kuelekea Zanzibar ilikumbwa na upepo mkali na kuanza kuzama kilomita chache kabla ya kufika. Abiria 63 kati ya 290 waliokuwamo walizama maji na wengine 80 hawakupatikana.

Cha kushangaza katika tukio lile ni kwamba muda mchache tu baada ya ajali ile helikopta iliyokuwa imebeba wakuu na viongozi wengine wa serikali ilifika katika eneo la ajali eti ‘kukagua’ hali ilivyokuwa.

Watu walihoji kwa nini helikopta hiyo badala ya kubeba ‘wakubwa’ kwenda kukagua haikubeba maboya na kuwatupia waliokuwa wanahangaika kuogelea – au hata kudondosha vikosi vya waokoaji wakiwemo wapiga mbizi? Hatukujifunza kitu kwani hakuna aliyewajibika au kuwajibishwa katika tukio lile.

Mwezi uliopita kulitokea tukio la moto kwenye kituo cha mpakani na jirani yetu Rwanda cha Rusumo upande wa Tanzania ambapo malori kadha na matenka ya mafuta yaliwaka moto baada ya lori moja kugonga malori mengine yaliyokuwa yamepaki kusubiri kushughulikiwa na mamlaka za Forodha kabla ya kuingia Rwanda. Bahati nzuri hakukutokea maafa makubwa kwa binadamu lakini magari kadha yaliteketea na zake.

Lakini kitu kimoja kilichojionyesha ni kwamba pamoja na hali hiyo ya takriban kila siku kujazana matenka ya mafuta kusubiri utaratibu wa mpakani kuelekea Rwanda, upande wa Tanzania hakuna tahadhari yoyote pale – ya vifaa au wazimamoto/waokoaji ya kukabiliana na majanga kama hiyo. Katika tukio lile mamlaka za Rwanda mara moja zilituma helikopta zilizobeba maji na vikosi vya zimamoto kusaidia.

Zoezi la uokoaji wa meli iliyozama ya MV Nyerere

Mnara wa kumbukumbu ya waliokufa katika ajali ya kuzama kwa MV Bukoba 1996

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.