Modric alivyovunja ngome ya Ronaldo, Messi Ulaya

Rai - - SPOTI -

MWANZONI mwa wiki hii, kwa mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka 10, mastaa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi

waliishuhudia tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Shirikisho la

Soka la Kimataifa (Fifa) ikitua kwa mchezaji mwingine.

Ikumbukwe kuwa tangu kiungo wa zamani wa timu ya Taifa ya Brazil, Kaka, alipoibeba mwaka 2007, tuzo hiyo ambayo mshindi wake hupatikana kwa kura za makocha na manahodha wa timu za taifa,

waandishi wa habari za michezo, na mashabiki, imekuwa ikichukuliwa na aidha Ronaldo au Messi.

Safari hii, Messi alishindwa kuingia hata ‘top three’ katika orodha iliyotolewa Septemba 3, mwaka huu, hivyo kuuacha mchuano mkali kati ya Luka Modric, Ronaldo na staa wa Liverpool, Mohamed Salah.

Hafla hiyo iliyofanyika Jumatatu iliyopita jijini London, ilimalizika kwa Modric kutangazwa kuwa mshindi, akijikusanyia zaidi ya asilimia 29 ya kura zilizopigwa, kigezo kikiwa ni mafanikio ya mchezaji kuanzia Julai 3, 2017, hadi Julai 15, mwaka huu.

Miongoni mwa waliopiga ‘kura ya ndiyo’ kwa Modric ni kocha wa England, Gareth Southgate, mkongwe Ryan Giggs (sasa kocha wa Wales), nahodha wa Madrid na timu ya taifa ya Hispania, Sergio Ramos, na Messi.

Aidha, Modric (33), aliweza kuwafunika nyota hao kutokana na kiwango chake kilichompa tuzo ya Mchezaji Bora wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu huko Urusi, ambapo akiwa nahodha aliiwezesha kufika fainali.

“Ni wazi kabisa kuwa kutajwa Mchezaji Bora wa Dunia inategemea sana na fainali za Kombe la Dunia na kiwango alichokionesha (Urusi) hakikuwa cha kawaida,” anasema Paul Merson, mchambuzi wa soka mwenye jina kubwa nchini England.

Kama hiyo ya kung’ara Urusi haitoshi, msimu uliopita, kiungo huyo wa kimataifa wa Croatia akiwa mchezaji muhimu katika eneo la kiungo, aliiwezesha Real Madrid kunyakua taji la tatu mfululizo la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ronaldo, ambaye anaichezea Juventus ya Serie A aliyojiunga nayo katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi ya mwaka huu, alishika nafasi ya pili, akiwa na asilimia 19 ya kura zilizopigwa.

Hata hivyo, si kwamba msimu uliopita haukuwa mzuri kwa Ronaldo kwani kwa mara ya sita mfululizo alitwaa kiatu cha mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa akiwa na mabao yake 15 na mwisho wa siku mchango wake huo wa kuzipasia nyavu uliipa Madrid taji hilo.

Katika fainali za Kombe la Dunia, alifunga mabao manne, ikiwamo ‘hat trick’ dhidi ya Hispania, lakini tatizo likawa moja. Akiwa ndiye nahodha, Ureno iliishia hatua ya mtoano (16 bora), hivyo Modric anakuwa bora zaidi kwa kuwa aliipeleka Croatia fainali.

Sehemu ya waliomchagua Ronaldo usiku ule jijini London ni makocha Cisse Aliou (Senegal), Herve Renard (Morocco), Santos Fernando (Ureno), Belmadi Djamel (Algeria), na nahodha wa England, Harry Kane.

Salah aliyekuwa moto wa kuotea mbali msimu uliopita, ambapo alifunga mabao 32 katika mechi zake 38 za Ligi Kuu ya England, aliburuza mkia mbele ya Modric na Ronaldo, akiwa na asilimia 11 ya kura.

Kwa upande wa kura, waliokuwa upande wa mwanasoka huyo raia wa Misri ni mchezaji mwenzake katika kikosi cha Liver ambaye ni nahodha wa Uholanzi, Virgil van Dijk, na kipa mkongwe wa Mafarao hao, Essam El Hadary.

Kilichowashangaza wengi ni kwamba Messi na Ronaldo hawakuhudhuria hafla hiyo katika Ukumbi wa Royal Festival Hall na hata Modric alipotajwa kuwa mshindi, nyota hao hawakutumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kumpongeza.

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.