Fikra za Mwalimu na kidole cha Lowassa kwa UDSM

Rai - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

MWALIMU Julius Nyerere amekuwa mwanasiasa pekee nchini ambaye matendo, fikra, mitazamo na kauli zake bado zinaishi, ingawa ametimiza miaka 19 sasa tangu afariki duniani, Oktoba 14, 1999.

Kumbukumbu ya kifo chake kwa mwaka huu ilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, hotuba na masimulizi yake yalitanda kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

MWALIMU Julius Nyerere amekuwa mwanasiasa pekee nchini ambaye matendo, fikra, mitazamo na kauli zake bado zinaishi, ingawa ametimiza miaka 19 sasa tangu afariki duniani, Oktoba 14, 1999.

Kumbukumbu ya kifo chake kwa mwaka huu ilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, hotuba na masimulizi yake yalitanda kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Jambo la kufurahisha zaidi ni wasomi na wanasiasa kuendelea kuzienzi fikra za Mwalimu Nyerere, kwa namna tofauti tofauti.

Miongoni mwa namna hizo za kumuenzi na kumkumbuka Mwalimu ni mdahalo wa wanazuoni ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, uliobatizwa jina la Mienendo ya Uchaguzi na Mustakabali wa Mataifa ya Afrika.

Mdahalo huo ulifanyika katika ukumbi wa Nkurumah uliopo ndani ya chuo hicho.

Miongoni mwa wanasiasa walioshiriki ni Waziri Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa.

Katika Mdahalo huo Lowassa aliweka wazi kuwa kinachoonekana sasa ni kama chuo hicho ambacho kilikuwa tanuru la fikra, kimekuwa goi goi.

Alisema Chuo kikuu kimekuwa kimya sana katika kukemea na kusemea masua mazito, tofauti na ilivyokuwa hapo awali, kani hata Mwalimu alikuwa akifika hapo na kuulizwa maswali na kuyajibu.

“… ukiacha kigoda cha Mwalimu, mmekuwa kimya sana, wakati wetu palikuwa tanuru la fikra, Mwalimu alikuwa anakuja anapewa maswlai anajibu.

“Tanuru la fikra lilikuwa ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, naona wajibu huo mmeusahau kidogo, msiwe goigoi onyesheni njia. Mzee Butiku alisema jana kuwa anaona kuna viashiria vya uvunjifu wa amani. Neno hilo mimi halinitoshelezi, msamiati huu nahitaji uwe mkali kidogo.

“Mimi naona nchini kuna tatizo la hofu na chuki, inajengwa hofu kubwa sana kwa wananchi wakati wa uchaguzi, hofu hii inawafanya wananchi kuwachagua watu wasiopenda kuwachagua..”

Lowassa alitolea mfano uchaguzi mdogo wa jimbo la Monduli, ambapo alisema kulikuwa na magari ya polisi 49, kati ya hayo manne ni magari maalum ya upupu.

Alisema inakuwa tabu kwa vyombo vya dola kusimamia uchaguzi. Alikwenda mbali zaidi kwa kuusifia uchaguzi wa Kenya kwa sababu waliofanya makosa katika Tume yao ya Uchaguzi walichukuliwa hatua kwa kupelekwa mahakamani.

“Uchaguzi wa hapa kwetu, msimamizi ni mtumishi wa serikali na analipwa na serikali na wengine wanasema waziwazi nimepewa kazi na serikali nitaiangushaje serikali.”

Aliipa nguvu hoja yake hiyo kwa hoja kuwa anashangaa upinzani hawajashinda uchaguzi mdogo hata mmoja, akidai sababu kubwa ni mbinu zilizowekwa ili wasishinde uchaguzi. “Lakini pia kuna chuki mbaya sana, ukiwa mwanachama wa CCM na mwenzako Chadema basi mchukiane.”

Alisema kwa sasa inatia hofu kwa nchi iliyokuwa na amani, utulivu na umoja kwa miaka mingi sana ikishuhudia mambo ya ajabu na kwamba ipo haja ya kukemea mapema.

“Nafikiri kuna haja kubadilika, wenzetu wa Uingereza wanautaratibu wa kama kukiwa na shida kubwa inapelekwa kwa Malkia.

“Hapa hakuna malkia kwa hiyo kila mmoja ana ndevu, inakuwa tabu ingefaa tukawa na utaratibu wa kutufanya kuacha chuki na hofu.

“Na pengine Katiba ile ya Warioba ipewe nafasi maana ina mapendekezo ya kuwapo kwa Baraza la wazee la ushauri ambao wanaweza kuwaita viongozi na kuwaambia hili na hili si sawa, haitoshi kusema kuna viashiria, waambieni hili si sawa, linaharibu ushirikiano wetu, linaharibu umoja wetu.”

DK. BASHIRU: SISTAHILI HESHIMA HII

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally alisema kuwa heshima aliyonayo sasa si yake bali ni ya chama chake na kwamba yeye kama Bashiru hastahili.

Aliyasema hayo wakati akijibu baadhi ya hoja zilizoelekezwa kwake na chama chake kwenye mdahalo huo.

Akiinuka kuchangia kwenye mdahalo huo, Dk. Bashiru alisema: Nakushuru sana Mwenyekiti, mimi sikunyoosha mkono, niliamua kuja kujifunza hapa, lakini napokea heshima hiyo kwa unyenyekevu.

Nasikitika Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema bada ya kusema ameondoka na aliyoyasema yalihitaji majibu kutoka kwenye chama.

Sasa naomba mliopo Katibu Mkuu (Dk. Vincent Mashinji) upo sikia majibu yangu kwake.

Lapili nasikitika Zitto ametoka pia, ambaye ni rafiki yangu sana, anahoji kwanini nipewe heshima hiyo, hii heshima si yangu ni heshima ya chama changu, chama kinachotawala kwa ridhaa ya kura za watanzania. Mimi sistahili heshima hiyo kama Bashiru.

La kwanza mimi nikiingia kwenye ukumbi huu naingia kwa hisia kali, tangu mwaka 1998 sijaondoka mpaka Rais Magufuli (Dk. John) aliponichomeka huko niliko.

Na mimi ni miongoni mwa watu tuliopewa heshima na Profesa Mukandara akiwa Makamu Mkuu wa chuo, kuunda Kamati ya kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere mwaka 2008 ikiongozwa na Profesa Issa Shivji mimi namuita Issa…na najisikia fahari kuona kigoda kinaandaa mijadala na hakijafa.

Ndugu zangu suala la mijadala ni kama damu kwenye mwili, kuna faida tatu, kwanza mnaweza mkabadilisha mazowea mabaya kwa jamii yenu, kupitia mijadala, pili mnaweza mkadumisha mazowea mazuri mliyoyarithi kwa vizazi na vizazi yakadumu, na ndio maana nafurahi kuona vijana wako hapa.

Lakini tatu mnaweza mkabuni mazowea mapya na mkayajenga na dhamana ya kufanya kazi hiyo kwa nchi masikini kama Tanzania ni Vyuo Vikuu vya umma, niseme mbele yenu mimi kama Katibu Mkuu nitapigia debe bajeti ya serikali kwenye vyuo vyetu vikuu vya umma ili vifanye kazi ya kukuza maarifa, vizalishe wasomi watakaotusaidia kutukomboa kifikira na kimaendeleo.

Na ndio maana chama chetu tunashiriki kwenye mijadala, nilishamwambia Mzee Butiku alipokuja kunieleza habari ya kunialika Dodoma, nikamwambia mimi niko tayari kujadiliana na wanasiasa wenzangu kwa shariti moja tu.

Sitashiriki kwenye mijadala wa kubishania mgawanyo wa vyeo na maisha ya anasa, sitashiriki katika mazungumzo yoyote ambayo mjadala tangu asubuhi mpaka jioni ni mjadala ni namna ya kugawana vyeo na mkishavipata muishi kwa maisha ya anasa.

Mijadala ndio namna ya kuiponya nchi yetu, mijadala itatufanya tujisahihishe, tumekosea sana katika nchi hii, tumepotea sana katika nchi hii na mbaya zaidi tumeanza kuogopa kusema ukweli.

Mjumbe wa Kamati Kuu (Lowassa) amesema habari ya hofu. Ni kweli wezi wa mali za umma, wakwepa kodi, matepeli wa kisiasa, walionunua mashirika ya umma bila kuyaendeleza, walioingia kwenye mikataba ya kutuibia mali, madali na makuwadi wa soko huria, lazima wataishi na hofu.

Sasa wakianza kusambaza hofu zao na kuziingiza kwa wananchi, tusizikubali, hofu za wananchi ni maji safi, elimu bora, ni haki mahakamani ni haki ya ardhi yao ni tija ya uzalishaji wao na mapato ya jasho lao ya haki, hizo ni hofu halali za wananchi.

Zipo hofu za kuchonga, kuna watu wanamidomo mirefu, mipana wanaingia kwenye magrupu ya wasapu na mitandao ya kijamii, kutisha wananchi wakati wanazo hofu zao halisi.

Nchi hii hatukubali kutengeneza hofu za kuchonga, hofu halisi tuzijadili, njaa, maji, ardhi, haki mahakamani na unaweza kuwa na mambo mengi yanayohusu maisha ya wananchi walio wengi na hasa masikini.

Kwa hiyo tusisambaze habari kuna hofu, hakuna hofu ambayo inagusa walarushwa, hata kama amekimbilia kwenye vyama tutamfuata, ilimradi haki imetendeka.

Suala lingine ni usalama, ndugu zangu mimi tangu nimeteuliwa nimezunguka katika mikoa 14 kwa miezi mitatu, wenzangu wakasema kipindi kilichopita vijana wa CCM na Chadema wanachukiana , wanapigana ngwara, Polisi wakae ndani eti kwa sababu watasababisha hofu!

Mimi ninao vijana ndani ya CCM na Chadema watakuwa nao. Imekuwa nadra katika ushindani, kukaa na kusalimiana na kupendana, wanafukuzana utafikiri si wa nchi moja, halafu polisi wawaache watoboane macho!

Itakuwa kutowajibika, ni kweli tuna matatizo katika vyombo vyetu, na vina uwezo mdogo ambao tunatakiwa kuujenga. Lakini hatujafikia kiwango hicho cha kusema tunahatarishi usalama, tukisema hivyo tutakuwa tunahatarisha uchumi wetu kwa maneno ya reja reja.

Mwisho, naafiki matatizo ya nchi hii yatasuluhishwa na umadhubuti wa vyama vya siasa, haina mjadala. Tangu nimeingia CCM nimekuta matatizo matatu, na wewe Chadema ndio unanifuata, lakini sasa hivi naanza kukuacha sana.

La kwanza nimekuta tatizo la kutokuwa na mtazamo wa pamoja, nini mnatakiwa kufanya, mnabishana nyie kwa nyie. Kwa hiyo suala la itikadi ambalo ndilo litakalowapa mtizamo wa pamoja ni tatizo kubwa zaidi ndani ya CCM kuliko vyama vingine na ndio maana tumekubaliana tuanze kujenga vyuo vya itikadi na tunavijenga kwa kasi na nimeona vinachelewa, nimesema tuanze hata kwa mahema.

Ninakozunguka hatuelewani, nikipaza sauti tunababaishana utafikiri hatuko chama kimoja, natamka mbele yenu, CCM bado inasimamia misingi ya Azimio la Arusha, asiyetaka kusimamia misingi hiyo aondoke afuate vyama vingine kama wengine wanavyoondoka kutoka kwenye vyama hivyo kuja CCM.

Tukiwa na mtazamo wa pamoja wa kiitikadi kwamba sisi tunasimamia utu, haki ya walio wengi, wavuja jasho na wafanyakazi, tutaelewana.

Vyama vyetu havina nidhamu, wanachama hawana nidhamu, hawahudhurii vikao, hawafuati kanuni na taratibu ukizisimamia wanakuwa wakali.

WIZI NDANI YA CCM

Katika mdahalo huo, Dk. Bashiru alisema ndani ya CCM kuna majizi ambao wanajifanya wazalendo, lakini wamepora ardhi, wameiba magari na wanapozungumza majukwaani wananchi wanaweza kuwaamini na kudhani ni wazalendo kweli.

Edward Lowassa

Dk. Bashiru Ally

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.