Tuepuke chaguzi za marudio za kulazimisha

Rai - - MAONI/KATUNI -

KWA mara ya kwanza nchi imeonekana kuwa na fedha nyingi zinazoeweza kuendesha chaguzi za marudio bila

tatizo.

Aidha, vyama vya siasa navyo vimebeba taswira ya namna hiyo hiyo kwamba vinazo fedha za kufanya kampeni za mara kwa mara, lakini hazina fedha za kutatua kero za wananchi.

Katika kipindi kifupi cha miaka mitatu tangu kufanyika kwa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 tayari zimeshafanyika chaguzi ndogo zaidi ya tatu, huku nyingine zikiendelea, huu ni ufujaji wa fedha za wananchi. Haukubaliki.

Kwa miaka mingi tangu kurejea kwa siasa za vyama vingi, chaguzi za marudio zilikuwa zikifanyika kwa nadra sana hasa mchaguliwa anapofariki dunia, tofauti na sasa wachaguliwa wanaamua wenyewe kuachia ngazi kwa upande huu na kwenda kuwania kwa upande ule.

Tunatambua wazi haya ni matakwa ya kikatiba, lakini ipo haja ya kuyakomesha ili kuepuka kuliingiza Taifa kwenye matumizi ya fedha na upotevu wa muda.

Utamaduni huu mpya haukubaliki na unadhoofisha jitihada na dhamira ya Rais ya kutaka watu wafanye kazi zaidi na kusubiri mwaka wa uchaguzi ndipo wafanye siasa za majukwani.

Tunaamini kila mtu anayo haki ya kuchaguwa na kuchaguliwa, lakini hatukubaliani na mwenedno huu wa baadhi ya wanasiasa wa kujiuzulu nafasi zao kwa sababu ambazo hazioneshi kuwa na uzito stahiki.

Upo uwezekano mkubwa wa viongozi wanaokerwa nay ale yanayofanywa ndani ya vyama vyao kusubiri hadi muda mwafaka wa kufanya uchaguzi Mkuu ufike ili wakatekeleze matakwa ya mioyo yao.

Hama hama ya sasa inaibua wingu la mashaka kwa wapiga kura ambao huenda kwa makusudi wengi wao wameamua kususia chaguzi hizi ndogo zinazoendelea.

Aidha kitendo cha wachaguliwa wale wale waliojiuzulu, kusimama tena katika majimbo yale yale nap engine kata zilezile kinaondoa maana nzima ya uchaguzi.

Tunaamini Serikali ya awamu ya Tano haifurahishwi na mwenendo huu wa wabunge kuachia nafasi zao na kuitia hasara Serikali kwa kufanya chaguzi za marudio.

Imani yetu kwa serikali ni kwamba yanayotokea sasa kamwe hayataruhusiwa yaendelee kwenye awamu ijayo na njia pekee ya kuyakomesha haya ni kufanya aidha marekebisho, maboresho au kupata Katiba mpya itakayobeba mwarobaini wa ufujaji huu usio wa lazima.

Jambo muhimu na la msingi kwa sasa ni kuhakikisha nchi na wananchi wake wanajielekeza katika kusaka suluhu ya matatizo ya wananchi waliowengi mijini na vijijini.

Bado hatuna barabara za kutosha, hatuna huduma bora za afya, maji safi na salama ni kizungumkuti na hata elimu yetu bado haijawa bora kwa kiwango kinachopaswa kiwe.

Fedha hizi zinazotumika kwenye kufanya chaguzi za marudio, zingeweza angalau kupunguza matatizo kwenye maeneo hayo ambayo yanapaswa kusimamiwa kikamilifu na Serikali.

Inaelezwa kuwa chaguzi moja ndogo ya marudio ikihusisha jimbo, inagharimu zaidi ya bilioni moja, sasa kwa idadi ya majimbo yaliyofanya na yanayotarajia kufanya chaguzi za marudio hadi sasa ni wazi tungeweza kusaidia vifaa, tiba, vifundishio, ujenzi wa barabara kwa urefu kadhaa ama hata kupeleka maji safi na salama kwa wasiokuwa nayo.

Aidha tunatoa rai kwa wanasiasa kuacha kuwahadaa wananchi kwa kusimama kuomba kura huku wakitambua wazi wanapigania matumbo yao na si maslahi ya wengi.

Kwa pamoja kwa maana ya wanasiasa, serikali na hata wananchi tunaouwezo wa kuepuka chaguzi za marudio zisizo za lazima.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.