Anguko hili la idadi ya wapiga kura halipaswi kufumbiwa macho

Rai - - MAKALA - NA ERIC SHIGONGO

Mjadala mkubwa unaoendelea hivi sasa, ni kuhusu kauli zilizotolewa na wanasiasa mbalimbali nchini katika siku za hivi karibuni, kuhusu suala la kuzidi kupungua kwa idadi ya watu wanaojitokeza kupiga kura, siku hadi siku.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, hivi karibuni akiwa mkoani Kagera, alieleza wazi kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM), kilipata kura chache katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 huku akielekeza lawama kwa watumishi wa umma akisema walipanga kukiangusha chama hicho.

Kauli hiyo ya Waziri Mkuu Majaliwa, ilikuja siku chache baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally kueleza kwamba idadi ya watu wanaojitokeza kupiga kura nchini, inazidi kupungua katika kila uchaguzi, huku akienda mbele na kueleza kwamba wapiga kura nchini wanaona uchaguzi ni sawa na vituko na maigizo.

Dk. Bashiru aliyasema hayo wakati akizungumza katika kongamano la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima (Mviwata), mkoani Morogoro hivi karibuni ambapo alienda mbali zaidi kwa kutolea mfano uchaguzi wa 2010, akisema serikali iliyoingia madarakani ilikosa uhalali wa kisiasa kwa sababu ya kuchaguliwa na watu wachache.

Hoja ya msingi hapa, ni kuzidi kupungua kwa kasi kwa idadi ya wapiga kura. Wanaojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura wanazidi kuongezeka, lakini wanaojitokeza siku ya kupiga kura wanazidi kupungua, kwa nini?

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mwaka 2000 wapiga kura waliojiandikisha walikuwa 10,088,484 na waliojitokeza kupiga kura wakawa 8,517,598, sawa na asilimia 84.4.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 16,407,318 lakini waliojitokeza siku ya uchaguzi, walikuwa 11,365,477, sawa na asilimia 69.3.

Katika uchaguzi mkuu uliofuatia, yaani 2010, idadi ya wapigakura waliojiandikisha ilikuwa 20,137,303, lakini ni wapiga kura 8,626,283 tu waliojitokeza, sawa na asilimia 42.84 ya wapiga kura waliojiandikisha.

Mwaka 2015, kati ya watu zaidi ya milioni 23 walioandikishwa kupiga kura, waliojitokeza kupiga kura walikuwa ni milioni 15.6 tu, sawa na asilimia 67.

Ukitazama mlolongo huo, inaonesha kwamba kuna tatizo mahali. Kwa nini watu wanajiandikisha lakini hawaendi kupiga kura? Yapo mambo mengi yanayoweza kusababisha hali hiyo, yakihusisha makundi yote, kuanzia wanasiasa, wapiga kura wenyewe na serikali.

Ipo dhana kwamba baadhi ya watu, hujitokeza kujiandikisha kupiga kura, kwa lengo la kupata vitambulisho vya kupigia kura tu, ambavyo huwarahisishia kupata huduma mbalimbali kwa kutumia kitambulisho cha mpiga kura. Hawa hawajitokezi kujiandikisha kwa sababu wanataka kupiga kura, la hasha! Ni kwa sababu wanahitaji vitambulisho tu.

Nchini Australia, kupiga kura ni wajibu wa kisheria na yeyote asiyepiga kura kwa sababu yoyote ile, anakuwa amevunja sheria na watu wengi wanaogopa kuvunja sheria, kwa hiyo uchaguzi ukifika, hakuna anayebaki nyumbani kwa kuogopa kukutana na mkono wa sheria.

Ni vizuri ukawekwa utaratibu wa kumfanya kila mtu mwenye sifa na vigezo vya kupiga kura, akaona kwamba ni wajibu wake kufanya hivyo.

Serikali inapoteza fedha nyingi katika kusimamia chaguzi, karatasi za kupigia kura zinatengenezwa kulingana na idadi ya waliojiandikisha, kwa hiyo wasipotokea siku ya uchaguzi, mbali na kushindwa kutumia haki yao ya msingi, lakini pia wanaisababishia serikali hasara.

Lakini suala jingine lililoelezwa hata na Dk Bashiru, ni kuhusu wananchi kukosa imani na jinsi chaguzi zetu zinavyoendeshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec). Wapo ambao wanaamini kwamba mshindi anakuwa ameshapangwa kabla hata ya uchaguzi na kinachofanyika pale, kinakuwa ni kama ‘maigizo’ kama alivyonukuliwa Dk. Bashiru.

Mwananchi haamini kama bado anayo nguvu kupitia kura yake moja kumuweka au kumuondoa mtu madarakani! Haamini kama karatasi la kupigia kura ni silaha yake anayoweza kuitumia kuamua nani apewe dhamana ya uongozi na nani asipewe.

Yawezekana zipo sababu kadhaa ambazo zimewafanya baadhi ya watu kupoteza imani na namna uchaguzi unavyoendeshwa na wahusika wameamua kuzinyamazia, matokeo yake ndiyo haya, idadi ya wapiga kura inazidi kupungua.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi, inatengewa bajeti kutoka serikalini kila mwaka. Ufike wakati sasa, katika bajeti hii kutengwe fungu maalum kwa ajili ya kuwahamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura.

Nchini Marekani kwa mfano, licha ya wananchi wake kuwa na uelewa mkubwa kuhusu haki za kiraia na masuala ya demokrasia, uchaguzi unapowadia, hamasa huwa kubwa sana mitaani.

Katika uchaguzi wa 2016 uliowakutanisha Donald Trump na Hillary Clinton, wasanii wakubwa kama Beyonce, Jay Z, John Legend, Madonna, Rick Ross na wengine wengi, walifanya kazi kubwa ya kuwahamasisha Wamarekani kujitokeza kupiga kura.

Nchini Tanzania, katika uchaguzi wa 2005, Kampuni ya Global Publishers LTD iliandaa tamasha la Kupiga Kura Siyo Ushamba. Lengo lilikuwa ni kuwahamasisha wananchi kupitia kwa wasanii wa muziki na filamu, kujitokeza kupiga kura kwa sababu kupiga kura siyo ushamba.

Matamasha ya namna hii, yanapaswa kuendelezwa badala ya kuviachia vyama vya siasa pekee na watu binafsi ndiyo viwahimize wanachama na wananchi kupiga kura.

Lakini pia tatizo lingine linatajwa kuwa ni ukosefu wa elimu ya uraia. Watu wengi hawaoni umuhimu wa kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura, na hata wakijiandikisha hawaoni umuhimu wa kuamka asubuhi siku ya uchaguzi na kwenda kupanga foleni kwa ajili ya kuwachagua viongozi wanaowataka.

Wanadhani kwamba suala la kuchagua viongozi wa nchi, haliwahusu na kwamba kuna kundi fulani ambalo lenyewe kazi yake ndiyo hiyo, ya kuchagua nani aongoze wapi. Si jambo la kushangaza kumsikia mtu anajigamba kwamba ‘sijawahi kupiga kura hata mara moja’, yaani anaona kushindwa kutumia haki yake ya kikatiba, ni ujanja.

Ufike wakati sasa, nguvu ielekezwe kwa vijana waliopo mashuleni na vyuoni, waone umuhimu wa kushiriki kwenye chaguzi mbalimbali nchini, na wao wakawe mabalozi kwenye familia wanazotoka. Lakini pia uwepo utaratibu wa kupita kwenye mitaa na vijiji, kuzungumza na wananchi na kuwafundisha kuhusu haki zao za msingi, ikiwemo ya kupiga kura.

Matatizo haya yasipopatiwa ufumbuzi, yatatufikisha mahali pabaya kama taifa, maana ya demokrasia itakuwa haipo tena. Lazima viongozi wanaoingia madarakani, waingie kwa kuchaguliwa kihalali na idadi kubwa ya wananchi. Inapotokea kiongozi anaingia madarakani kwa idadi ndogo ya watu waliompigia kura, huku watu wengi zaidi wakiwa hawajashiriki katika uchaguzi, akiingia madarakani atawaongoza wote, waliomchagua na wasiomchagua.

Na hapa ndipo unapoibuka mwanya wa viongozi wasiofaa, kuingia madarakani kwa kutumia udhaifu wa Watanzania wengi kutotumia nguvu waliyopewa kikatiba. Kiongozi wa namna hii, hata pale anapoboronga, wananchi wengi hawawezi kumwajibisha kwa sababu hawakumchagua!

Lakini kama ulimpigia kura kiongozi fulani kwa ahadi kemkemu, akiingia madarakani na kufanya ndivyo sivyo, unakuwa na nafasi ya kumwadhibu kipindi uchaguzi mwingine unapokaribia, kwa kumnyima kura yako. Ikiwa kila mwananchi atafanya hivi, uwajibikaji wa viongozi na ufanisi katika kuwahudumua wananchi utaongezeka.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.