Nyerere alikuwa ‘dikteta’ wa Muungano

Rai - - MAKALA - NA BALINAGWE MWAMBUNGU

MUUNGANO ni kitu kizuri. Hata wahenga walisema kuwa kidole kimoja hakiwezi kuua chawa, au, umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.

Hii ni dhana ambayo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliamini, ni katika mantiki hiyo aliweza kuziunganisha kabila zaidi ya 120 za iliyokuwa Tanganyika, zikasimama pamoja na kuweza kulishawishi Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuridhia ipewe uhuru.

Kuna sehemu naadhani historia inapotoshwa, kwamba Waingereza walikuwa wakoloni—walioitawala Tanganyika. Hapana. Waingereza waliitawala (colonized) Kenya— lilikuwa koloni lao. Walitawala Tanganyika kwa niaba ya Umoja wa Mataifa (League of Nations) ambayo sasa inajulikana kama United Nations. Ni kama vile mtu anakabidhiwa dhamana ya kumlea mototo ambaye hana nasaba naye, kwa sharti kwamba akisha kua, anaweza kuachiwa akasimama mwenyewe.

Ndio maana tunasoma kwamba Mwalimu Nyerere alikwenda kwa mara ya kwanza mwaka 1958 (?) Umoja wa Mataifa (UN) na kulihutubia Baraza Kuu, akidai Uhuru wa Tanganyika. Hakwenda Uingereza kwa sababu Tanganyika ilikuwa Trust Territory na sio koloni la Uingereza.

Katika makala haya nitaeleza mambo mawili makuu—Mwalimu Nyerere na Muungano, Mwalimu Nyerere na Ujamaa. Hoja hizi ni muhimu katika muktadha wa kumtazama Mwalimu kama mkombozi (liberator), na Mwalimu kama dikteta wa suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kwanza napenda kukiri kwamba mimi ni mfuasi wa Mwalimu Nyerere, niliofanya nao kazi kama mwandishi wa habari Daily/Sunday News, wananijua hivyo. Niliwahi kushika nafasi ya juu ya uongozi kama Katibu wa Tawi wa Jumuia ya Wafanyakazi (JUWATA) kwenye kampuni ya Tanzania Standard Newspapers (TSN), wachapishaji wa magazeti niliyoyataja hapo juu. Kutokana na wadhifa huo nikawa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Tawi la Chama cha Mapinduzi (CCM), tawi la Printpak Daily News— wakati huo chama kilikuwa kimeshika hatamu za uongozi kwenye mashirika na taasisi zote za umma na Serikali—kuhakikisha kwamba viongozi wanasimamia utekelezaji wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na kufuata miongozo yote ya Chama, ikiwa ni pamoja na maadili ya uongozi.

NYERERE NA MUUNGANO

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar haukuwa muungano wa mapenzi kati ya nchi hizi. Ulikuwa muungano wa haja. Ni kweli kwamba Mwalimu alikuwa muumini mkubwa wa ndoto ya Muungano wa Bara la Afrika— lakini aliamini kwamba muungano huo utafikiwa gradually—taratibu na sio wa ‘paa’ mara mmeungana kama ndoa ya mkeka.

Aliamini kwamba Afrika itakuwa na nguvu zaidi ikiunganisha nchi kimakundi. Mwalimu alikuwa tayari kuahirisha Uhuru wa Tanganyika, ili nchi tatu—Kenya, Uganda na Tanganyika, zipate uhuru siku moja. Halafu viongozi wakae pamoja (kabla mizizi ya utaifa haijazama na viongozi kunogewa madaraka), na kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki.

NdotoileilimponyokaMwalimu. Kama nilivyosema awali—Kenya ilikuwa ni koloni la Waingereza, walikuwa na mizizi mikubwa kwa maana ya mashamba na viwanda—hawakupenda kuukimbilia muungano. Wazungu walishamsoma Nyerere—alikuwa na dalili za kisoshalisti—kupenda maendeleo ya pamoja. Kenya pia ilikuwa na nyufa za ukabila, kwa hiyo Rais wa kwanza, Jomo Kenyatta, aliitazama Kenya katika mustakabali huo—Kikuyu kwanza.

Waingereza walitawala Uganda kupitia kampuni ya East African Company—halikuwa koloni kama Kenya. Ugnda pia ilikuwa inatawaliwa katika mfumo wa kifalme—Buganda chini ya Kabaka ikiwa ndio yenye nguvu zaidi. Falme nyingine kubwa zilikuwa Ankole, Toro, Bunyoro na Busoga. Ilitakiwa falme hizi ziungane na kuingia kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki kama nchi moja.

Kwa hiyo matatizo ya Kenya na Uganda yakawa kikwazo kwa Mwalimu Nyerere—akakubali Tanganyika iende kivyake— ikapata Uhuru Desemba 9, 1961 kabla ya Uganda na Kenya.

Baada ya nchi zote kupata uhuru, zikaanza juhudi za kuunda shirikisho, lakini tukio la ghafla mapinduzi ya Zanzibar— Mapinduzi yaliyong’oa utawala

wa kisultani Januari 12, 1964, yalibadili taswira na mwelekeo wa kisiasa, na kiulinzi wa Nyerere. Zanzibar ilikuwa tishio kwa usalama wa Tanganyika. Kuna usemi kwamba wanapokohoa Zanzibar, Kigoma wanapata mafua. Yaliyofuata ni historia. Mwalimu alihama kutoka dhana yake ya ‘gradual unification’ na kuunda muungano wa dharura.

Hiyo ndiyo sababu kuu ya kuunda Muungano wenye matege kama rafiki yangu Chris Rweyemamu (rip) alivyokuwa anasema. Huu ndio muungano ambao wahafidhina ndni ya CCM wanaung’ang’ania kwa udi na uvumba. Kuna upuuzi unaosemwa kwamba zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania sio hawaijui Tanganyika— walizaliwa Tanzania—kwa hiyo hwaijui Tanganyika. Eti wanaodai Tanganyika ni kizazi cha zamani na kinakwisha!

Katika uhai wa taifa la Tanzania, kumekuwa na Tume tatu. Tume ya Jaji Fracis Nyalali, Tume ya Jaji Robert Kisanga na Tume ya Jaji Joseph Warioba, zote zilikusanya maoni kuhusu Muungano pamoja na mambo mengine. Mara tatu Watanzania wameulizwa kuhusu Muungano, na mara tatu wamejibu, wanataka serikali tatu.Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano; na mara tatu CCM wameyakataa matakwa ya Wananchi.

Nyuma ya uwamuzi huu, ni msimamo wa Mwalimu Nyerere. Sitaki kurudia aliyoyasema Nyerere, kwa sababu sikubaliani na Nyerere, sijawahi kukubaliana naye, sintakubaliana na utetezi wa muungano kama ulivyo sasa. Mwalimu alifanya udikteta na hakutaka majadiliano katika hili. Hata Abeid Amani Karume, alitaka Muungano ujadiliwe upya, Nyerere hakutaka kwa sababu tu ni muungano pekee katika Afrika—ni success story ya Nyerere peke yake katika Afrika. Baada ya kung’atuka akarudi ulingoni:

“Mmevunja Azimio la Arusha, nikanyamaza, sasa mnataka kuvunja Muungano. Hapana.”

UJAMAA NA KUJITEGEMEA

Sera ya Ujamaa na Kujitegemea, wengine wanasema ilikuwa ‘utopian’—siasa ya kufikirika. Mimi nilikuwa kada wa TANU na mmoja wa waasisi wa CCM. Ni muumini wa Azimio la Arusha lililosheni maudhui ya Ujamaa na Kujitegemea, pamoja na miiko yake na dhana kuharakisha (sio kuleta) maendeleo kwa njia ya kujitegemea.

Nakubaliana na Mwalimu, Baba wa Taifa, kwamba maendeleo sio ya vitu— maendeleo ni ya watu—kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya wananchi katika ujumla wao.

Haya ndio yalikuwa maudhui ya Azimio la Arusha. Angeamini tofauti, Mwalimu angejenga barabara ya lami kutoka Musoma kwenda Butiama, angejenga hekalu Butiama, angejenga uwanja wa ndege wa kimataifa Musoma, au angetandika reli ya kutoka Mwanza kwenda Musoma au Arusha kwenda Musoma kupitia mbuga zisiso na watu na wala hazitakuwa na watu. Hakufanya hivyo. Sio kwamba alipenda ukale—alitaka na alitamani maendeleo ya watu—maendeleo ya pamoja kwa Wananchi wote.

Tunapoadhimisha miaka 19 ya Tanzania bila Nyerere, tukiri kwamba aliondoka kwa huzuni. ‘Nawahurumia Watanzania’— alijua kuwa kutakuwa na kipindi kigumu mbele yao—kipindi cha unyang’au, ufujaji wa rasilimali ya nchi, ukandamizaji wa fikra huru na ubinywaji wa haki za binadamu. Yaliyojiri baada ya Mwalimu kututoka, sina sababu ya kuyarudia, sote tunayajua.

Nakumbuka maneno yake kwamba baada ya Azimio la Zanzibar, wenye akili, walielewa kuwa Ujamaa ndio basi tena. Wameikata tamaa, lakini hata Kujitegemea hamtaki! Yalikuwa maneno ya kukata tamaa. Alikuwa hana madaraka tena ya kukataa kama alivyolikmalia Bunge na Hoja ya Tanganyika. Akasema sera ya chama chake ni Serikali Mbili, anayetaka serikali tatu aondoke kwenye chama chake.

Tunaomkumbuka Mwalimu, maneno haya yanagonga mioyoni mwetu. Mwalimu aligeuka dikteta. Wabunge wakaogopa. Hoja ya G55 ikafa kifo chamende.

Mwalimu alitetea Umoja na Mshikamano wa Kitaifa, hakupenda viongozi watazamane kwa jicho la ukabila, dini, ukanda wala rangi. CCM walikataa Mfumo wa Vyama vingi vya Siasa, Mwalimu kwa ushawishi, alidikteti mfumo wa vyama vingi ambao sasa unabomolewa— kwa sababu hayupo. Mwalimu hakuwa mtu wa kukumbatia ukale.

Wanaosema wanamuenzi Mwalimu, muasisi wa chama chao, wanamuenzi Mwalimu yupi na kwa lipi hasa?

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.