JE, NYERERE ANGEMPOKEA JOSEPH KASAVUBU?

Rai - - MBELE - NA NDAHANI MWENDA

OKOTOBA 23, 2016, Rais John Magufuli alimpokea Mfalme wa Morocco, Mohammed VI na ujumbe wake. Mfalme huyo alikuja Tanzania kushaiwish­i uungwaji mkono katika kampeni ya nchi hiyo kurejeshwa kwenye Umoja wa Afrika (AU).

Katika ziara ile, Tanzania na Morocco zilitilian­a saini mikataba 21 yenye thamani ya Shillingi trillioni 4 za Kitanzania katika ushirikian­o wa sekta mbalimbali kama afya, elimu, gesi, ujenzi na viwanda. Lalini hapo awali, Tanzania na Morocco hazikuwa na uhusiano mzuri baada ya Sera ya Nje ya Tanzania kuitambua Sahara Magharibi kama nchi huru. Morocco hadi leo, imegoma kuipa uhuru wake na watu wa Sahara wamekuwa wakipata manyanyaso kutoka katika utawala wa Kifalme.

Tanzania kwa siku nyingi ilikuwa ni mtetezi wa mataifa mengine yaliyokuwa yakionewa ndani na nje ya Afrika, iliweka msimamo wa kutokuwa na uhusiano na Morocco, Israeli na Afrika Kusini iliyokuwa chini ya Makaburu. Hiyo ni katika enzi za utawala wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, Rais Ali Hassan Mwinyi na Rais Jakaya Kikwete.

Katika hali ya kuonyesha anajali utu na haki kwa kila binadamu wa dunia hii, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema: “Uhuru wa Tanzania hautakuwa umekamilik­a hadi nchi zote za Afrika ziwe huru.” Alimaanish­a kuwa hatuwezi kuwa huru, wakati ndugu zetu (Waafrika), wapo kwenye ukoloni ulele ambao tunaupinga. Unawezaje kuwa huru nduguyo yupo kifungoni ? Lahasha huo sio Uhuru!

Mwalimu na Tanzania kwa ujumla, tulikuwa mstari wa mbele kuhakikish­a nchi za Afrika zinapata uhuru na haki ya kujitawala ( The right to Self-Determinat­ion) kuanzia nchi kama Zimbabwe, Afrika Kusini, Namibia, Msumbiji, Angola, Cape Verde, Guinea-Bissau na nyinginezo.

Makao makuu ya harakati za ukombozi yalihamish­iwa Dar es salaam mwaka 1974 kutoka Accra, Ghana. Hivyo basi, Tanzania ilijipamba­nua kuwa ni nchi inayojali usawa na haki kwa binadamu wote bila kubagua eneo wanalotoke­a, rangi zao, dini zao wala makabila wanayotoke­a.

Mwaka 1961, miezi michache kabla ya Tanganyika haijapata uhuru, akiwa kwenye Mkutano wa Nchi za Jumuiya ya Madola (Commonweal­th), Mwalimu Nyerere aliwambia wajumbe wa mkutano kuwa Tanganyika haitajiung­a kwenye jumuiya hiyo kama Afrika Kusini itaendelea kukaliwa na Makaburu. Huo ndiyo ulikuwa msimamo wetu, kutetea watu wanaokanda­mizwa.

Imani hii ndiyo iliyofanya taifa letu kuwa kimbilio la wanaharaka­ti wote duniani, tuliwapa chakula, mavazi na mafunzo ya kijeshi. Ushahidi unajidhihi­risha ukienda Mazimbu-Morogoro, Iringa na maeneo mengine kule Dodoma.

Mashujaa wa Tanzania walimwaga damu kupigania uhuru wa ndugu zetu (Waafrika) hii ililifanya taifa letu kuwa kituo cha wanamapind­uzi duniani.

Ukienda leo Maputo, Mji Mkuu wa Msumbiji, mwili wa Kanali Ali Mahfoudh, umezikwa kwenye makaburi ya mashujaa wa nchi hiyo, kwa saababu wanatambua mchango wake kwa taifa hilo.

Tuliweka mwenge kwenye kilele cha Mlima Kilimanjar­o, kwa lengo la kuleta mwanga kwenye giza, kuleta matumaini kwa wale waliokata tamaa dunia kote. Kama hatuna tena imani hiyo, maisha yetu sisi kama taifa yana maana gani ?

Morocco ilijitoa yenyewe kwenye Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), miaka 34 iliyopita, umoja huo sasa unajulikan­a kama AU. Ilijitoa kwa kutaka kuendeleza siasa zake za kikoloni dhidi ya watu wa Saharawi.

Tanzania na nchi nyingi za Afrika zilipinga ubeberu wa Morocco dhidi ya watu wa Sahara. Tangu miaka ya 1970 Morocco haikubadil­i sera zake dhidi ya watu wa Saharawi. Imeendelea kuikalia Saharawi mpaka leo.

Watu wenye umri wa miaka 40 hadi 60 hivi wakati wanasoma walimabiwa kuwa wale wapigania uhuru wa POLISARIO ni ndugu zetu.

Sasa tulishauka­na msimamo wetu wa miaka takribani 50 iliyopita. Tukamkarib­isha mkoloni, Mfalme Mohammed VI. Akapigiwa mizinga 21 na kumtandiki­a zulia jekundu (Red Carpet). Tukamkarib­isha Ikulu na kumpa dhifa (kula na kunywa naye), kwa kisingizio cha Diplomasia ya Uchumi. Hivi kwa msaada gani ambao yule alitupa? Ahadi ya kujenga uwanja wa mpira kule Dodoma? Wenzetu Misri, Algeria na Tunisia bado wamesimami­a msimamo wao ule ule hadi leo!

Sasa napata wakati mgumu kujua anajisikia­je huko aliko Mwalimu Julius Nyerere! Sijui anajisikia­je Dk. Salim Ahmed Salim, Abdulraham­an Babu, Brigedia Jenerali Hashimu Mbita, au Ami Mpungwe ? Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje iliyotolew­a baada ya taarifa za ujio wa Mfalme wa Morocco iliushanga­za ulimwengu wa kidiplomas­ia— eti bado msimamo wetu dhidi ya watu wa Saharawi upo pale pale!

Hivi Mwalimu Nyerere angeweza kumkaribis­ha Pik Botha Ikulu, akanywa naye mvinyo, halafu kesho amwambie Nelson Mandela na ANC yake, kwamba tupo pamoja. Angeelewek­a? Sidhani kama Mwalimu Nyerere angempokea Joseph Kasavubu, ampigie mizinga, kisha aseme: Patrice Lumumba Watanzania tupo nyuma yako!

Angeanzaje kumpigia mizinga 21 Ian Smith, kisha aje kwa Robert Mugabe na ZANU-PF, aseme tupo pamoja ? Tungeweza kumkaribis­ha Mfalme Farouk, halafu tuje kwa Gamal Abdi el Nasser tuseme tupo naye na akakubali ?

Tusingewez­a kuwaunga mkono Golda Myer ama Yitzhak Rabin hapa nyumbani, kisha tuende kwa Yassin Arafat na PLO, tuseme tupo nanyi na tukaelewek­a.

Kaka yangu Ezekiel Kamwaga alisema kuwa akiondoka Mfalme Mohammed VI, tumwalike Benjamin Netanyahu, na kisha tuseme msimamo wetu juu ya uhuru wa Wapalestin­a upo pale pale.

Huwezi kula na kunywa na mchafu na ukasema wewe ni msafi, hakika si msafi hata chembe. Uovu si kuutenda tu, bali hata kushirikia­na na mwovu, nawe utakuwa muovu tu!

Nadhani wote kama taifa tulipaswa tupinge ziara ya huyu Mfalme wa Morocco, inatuletea sifa mbaya. Morocco inataka kurejea kwenye AU, ili ipate uungwaji katika sera zake za kuikalia Saharawi.

Kubadili sera yetu ya mambo ya nje kwa kisingizio cha diplomasia ya uchumi, ni dhahiri sasa Tanzania inajali vitu na si utu tena!

Ndiyo maana hadi leo najiuliza. Je, Mwalimu Nyerere angempokea Joseph Kasavubu aliyeungan­a na wakoloni kukandamiz­a haki za Wakongoman­i, halafu amgeukie Patrice Emery Lumumba amwambie tupo pamoja?

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.