NI DUNIA YA WATU NA VIATU

Rai - - MBELE - 0784-307271

Kwani mbele ya watu na mimi mtu? Katika dunia hii inayothamini vitu, mtu asiye na kitu huyo naye ana utu? Huyo ni kiatu tu cha kuvaliwa na watu wenye nyendo zao ili wanusurike na mbigili. Nenda zako usinizidishie machungu. Hivi ndivyo rafiki yangu wa tangu utotoni alivyonilaki nilipomtembelea.

Husewa kuwa yapo makundi matatu ya watu. Lipo kundi linaloishi ndani ya dunia ya Mungu ambao huishi na subira, na hakika kwao wao kukata tamaa na rehema za Mungu ni haramu mutlaki. Hawa ni wale wenye kutambua kuwa walikuja duniani kupitia matumbo ya mama zao wakiwa hawana pesa wala mali. Hawa ni watu.

Lipo kundi la watu linaloishi ndani ya dunia ya vitu ambao kwao wao utu ni kitu. Toba! Hawa huamini kwamba maisha yaliyokamilika ni yale ya mtu kumiliki mali, vitu na watu. Eti asiye na mali ni dhalili, asiye na kitu si malikitu, na asiye na watu huyo hana maisha bali ni msindikizaji wa wenye kuishi. Hawa nao watu.

Na kundi la tatu ni lile linaloishi ndani ya dunia ya watu yenye vimungu watu, ambao badala ya kusubiri waliyokadiriwa na Mungu hungojea wanayoahidiwa na miungu watu wao. Ni dunia yenye mseto wa watu wenye kutakabari na wenye kustahabu udhalili. Utu wangu japo bura yangu sibadili kwa rehani. Na hawa pia watu.

Usidiriki ndugu yangu kupima thamani ya utu wako kwa kulinganisha na maisha ya ndugu yako, rafiki yako, jirani yako au yeyote awaye utu wako ulioumbwa nao na kuzaliwa nao ni mali yako peke yako. Kuutia thamani utu wako kwa kutenda yenye murua au kuufuja utu wako kwa kuendekeza dunia ni hiari yako mwenyewe.

Tena usidiriki ndugu yangu kuizima thamani ya utu wako kwa kujilinganisha na maisha uliyoishi nyuma. Majani yenye rangi ya kijani kibichi mtini hunyauka, hupauka na kupukutika matawi yakabakia utupu, bali mti hubakia mti ukasubiri wakati wa matawi kuotesha majani machanga. Kila jambo na muda wake.

Masuala ya faraja na dhiki, furaha na huzuni, raha na karaha hutanda ndani ya nafsi yako, ikaathiri hisia zako na kuviza fikra zako. Kujinasua na jela ya masaibu huna budi kuizindua nafsi yako sasa. Usisumbuke na sababu za mikwaruzo, ganga kidonda sasa, utalea kovu kesho. Jela ya nafsi huathiri hisia na fikra ukaikaribia wazimu.

Machozi ya vicheko na vilio vya wenzako wanaokuzunguka hayana uwezo wa kukunasua na jela ya masaibu. Kuhudumiwa na nduguzo au rafiki zako kwa masaibu ya idhara na idhilali zinazokukumba si ufumbuzi kwako. Yageuze yaliyo mbali nawe ishughulika na yanayokusumbua sasa. Hatua kwa hatua utanasuka.

Mimi na wanangu tuliamua ndani ya miezi mitatu mfululizo kumshika mkono ndugu yangu. Tulishirikiana naye kusafisha karibu ekari moja ya shamba lake na tulifanikiwa kuchimba kisima kifupi chenye maji baridi na ya kutosha. Tulimfuta bwana shamba wa kijiji naye akatuitika.

Ndani ya miezi sita bustani ya ndugu yangu ikapewa jina na kuwa Bustani Darasa. Wachuuzi walikuwa wanafuata mbogamboga pale pale bustanini. Mkewe karejea na sasa wamehamia bustanini pao. Si mambo ya mbogamboga tu bali sasa ipo mifugo ya kuku wa kienyeji na bata tele tele. Ndugu yangu siye yule tena.

Sina nia ndugu yangu ya kukuzidishia machungu. Lakini sikubaliani na wewe kuwa eti wewe haupo hapa duniani kuishi ila umekuja kuwasindikiza kuishi. Ala! Maneno gani hayo! Ikiwa mwenyewe umeshindwa kutambua tatizo linalokukwamisha mfuate nduguyo au rafikiyo.

Kalamu ya muungwana imekuonyesha njia tu bali uamuzi wa kusafiri na lini utasafiri ni wako ndugu yangu. Wewe ni mtu si kiatu. Tambua tatizo lako usonge mbele.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.