Msaada wa Kisheria ni muhimu kwa watoto waliopo katika ukinzani kisheria

Rai - - MAONI / KATUNI - NA WILLBROAD MATHIAS

SHERIA ya Msaada wa Sheria ni kati ya Sheria ambazo zinatumika kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Sheria hii namba 1 ya mwaka 2017 ambayo inatumika Tanzania bara

SHERIA ya Msaada wa Sheria ni kati ya Sheria ambazo zinatumika kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Sheria hii namba 1 ya mwaka 2017 ambayo inatumika Tanzania bara pekee ina lengo la kuwatambua wasaidizi wa kisheria, kuboresha utoaji wa msaada wa sheria na kufuta sheria ya Msaada wa Sheria (Makosa ya Jinai) Sura namba 21

Chimbuko la sheria hii lilitokana na uhitaji mkubwa wa kuwa na sheria nchini itakayoongoza kisheria namna ya utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa wahitaji ili waweze kufikia haki.

Sheria hii ilitungwa na bunge mnamo Januari 31, 2017 na ikapitishwa rasmi na kusainiwa na mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Februari 21 , 2017 na kisha ikatangazwa kwenye gazeti serikali namba 9 la mwaka 2017 na kuanza kutumika rasmi Julai mosi , 2017 kwa mujibu wa tangazo la serikali namba 20 la mwaka 2017.

Pia sheria hii imetungwa kukidhi matakwa ya mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo nchi yetu imesaini na kuridhia kuhusu haki za binadamu ikiwemo haki ya kupata msaada wa kisheria.

Kuanzishwa kwa sheria kumesaidia kwa kiasi kufulani kuikomboa jamii ambayo ilikuwa inakabiliwa na changamoto kubwa hivyo kujikuta ikinyimwa haki kutokana na kutofahamu sheria.

Mbali na kukosa ufahamu kisheria pia jamii imekuwa ikishindwa kupata msaada huo aidha pengine kwa kutokuwa na uwezo wa kupata wanasheria wa kuwasimamia wakisaka haki zao kutokana na hali duni kiuchumi. Miongoni mwa jamii hiyo ni pamoja na watoto waliopo kwenye ukinzani kisheria ambao wamekuwa wakijikuta wakisota katika vyombo vya dola bila kupata msaada wowote. Sheria hiyo pia ndiyo iliyochangia kuzaliwa Chama Cha Wanasheria Wanawake Tanzania ,TAWLA ambao walijielekeza kutetea haki za Wanawake na Watoto.

TAWLA inajishughulisha na kutetea na kulinda haki za Wanawake, watoto wanaishi katika mazingira hatarishi,kutetea haki za ardhi,kuongeza ufahamu juu masuala ya ajira kwa watoto na kushughulikia mahabusu za watoto waliopo katika ukinzani kisheria.

Kwa misingi hiyo chama hicho cha TAWLA ambao ni miongoni mwa wadau hao ambapo pamoja na mambo mengine kinasema msaada kisheria kwa watoto hususan waliopo katika ukinzani kisheria ni muhimu kama ilivyo kwa wana jamii wengine na hivyo inafaa upatikane kama inayoelezwa katika kanuni za mwenendo wa Mahakama za Watoto.

Kuhusu msaada huo kisheria TAWLA wanasema, kwa mujibu wa Kanuni za Mwenendo wa Mahakama ya Watoto za mwaka 2014 kanuni namba 14 kifugu cha kwanza kinaeleza wazi kwamba Mtoto ambaye ni mhusika katika shtaka la jinai au shauri la madai atakuwa na haki ya kupata huduma ya kisheria na misaada mingine inayofaa.

Wanasheria hao wanasema pia kifungu cha pili cha kanuni hiyo namba 14 (2) kinaeleza pia pale ambapo mtoto ambaye ni mhusika katika shauri hana uwakilishi wa kisheria, mwakilishi wa kisheria, uwakilishi huo utatolewa kwa mtoto bila gharama yeyote kwa wakati utakaohitajika.

“Pia Kanuni namba 15 kifungu (1) kinaeleza wazi kwamba pale ambapo mtoto hana uwezo wa kugharamia uwakilishi wa kisheria na haiwezekani kutoa huduma ya kisheria bure ya kwa mtoto, na mzazi au mlezi hana uwezo wa kutoa uwakilishi unaofaa kwa mtoto, hakimu anayeendesha shauri atahakikisha kwamba mtoto anayeshtakiwa kwa kosa la jinai anapewa msaada unaofaa kwa kupatiwa mlezi anayeteuliwa na Mahakama,”wanasema TAWLA.

Wanasheria hao wanasema pia kanuni namba 15 kifungu cha pili kinasema kwamba Mahakama itamweleza mtoto aliyerejewa chini ya kanuni ndogo ya (1) kwamba anaweza kuchagua kuwakilishwa na mzazi au kuiomba kuchagua mlezi aliyeteuliwa na Mahakama au kuiomba Mahakama imteue mtu huyo.

TAWLA wanafafanua kwamba pale ambapo mtoto ni mhusika katika shauri la madai au anahusika na shauri la kinga ya mtoto, atawakilishwa na mlezi aliyeteuliwa na Mahakama, na atakuwa na haki ya kuwakilishwa kisheria.

Wanasheria hao wanasema kwamba pia kanuni hiyo kipengele cha nne kinaeleza kuwa ili kumsaidia mtoto ambaye yupo katika ukinzani kisheria Mahakama itamruhusu yeye ambaye ni mwathirika au ambaye ni shahidi katika shtaka la jinai na anayetoa ushahidi mbele ya Mahakama kusaidiwa na mlezi anayeteuliwa na Mahakama.

“Pia kipengele cha tano kinaeleza wazi kwamba Mahakama kwa maombi yaliyorejewa chini ya Kanuni ndogo (4), inamteua mlezi pale ambapo uteuzi huo ni kwa maslahi ya mtoto,”wanafafanua TAWLA.

Wanasheria hao wanaeleza kuwa kanuni hiyo pia inaelekeza kwamba Mahakama itamruhusu mlezi aliyeteuliwa na kumsaidia mtoto katika mahojiano ya mashahidi kuwasilisha ushahidi wa kimaandishi au ushahidi mwingine kwa niaba ya mtoto na kuielezea Mahakama kuhusiana na mtazamo, matarajio na maslahi ya mtoto.

Wanasema pale ambapo mlezi wa kuteuliwa na Mahakama wanatofautiana na mtoto anaweza kuomba kuruhusiwa kuchagua mlezi mwingine au Mahakama imchagulie mlezi mpya.

“Mahakama pia inaweza, kwa hiari yake yenyewe au kufuatia maombi yaliyofanywa na ofisa ustawi wa jamii, kumuondoa mlezi wa

Mahakama anayetenda kinyume na maslahi ya mtoto, na itamtaka mtoto kuchagua mlezi mpya au kumteua mlezi mpya wa Mahakama,”wanasema wanasheria hao wanawake.

TAWLA wanasema ili kuhakikisha mtoto anapata haki yake kwa kutumia kanuni hiyo, Hakimu Mfawidhi kwa kushauriana na Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii wa Wilaya ambayo Mahakama ipo ni lazima ahakikishe kwamba, wilaya ina idadi ya kutosha ya walezi wa kuteuliwa na Mahakama wenye sifa na uwezo wa kumsaidia mtoto.

Wanasema katika kipengele namba 10 cha kanuni hiyo Mahakama inatakiwa kuweka pia orodha ya walezi wa kuteuliwa na Mahakama waliopo katika Wilaya husika ili waweze kutambulika kwa mujibu wa sheria ili kuwanusuru watoto hao waliopo katika ukinzani kisheria wastumbukie mikononi mwa wasio husika.

Wanashauri endapo kanuni hii ya Mwenendo wa Mahakama za Watoto itazingatiwa itakuwa rahisi kuwasaidia walengwa na kupunguza idadai ya watoto ambao wanashikiliwa magerezani na mahabusu na kuwajengea mazingira salama.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.