Tanzania tunayoitamani tutaifikia kwa ushindi mkubwa

Rai - - MAKALA - NA ERICK SHIGONGO

Hata siku moja sitathubutu kubeza yaliyofanywa na serikali za awamu nne zilizopita katika nchi yetu, ingawa mimi ni miongoni mwa watu wanaoamini kwamba mabadiliko yanayotokea katika nchi yetu, kwa macho yangu nimeshuhudia mambo ambayo huko nyuma sikuzoea kuyaona; Nidhamu katika utumishi wa umma, udhibiti wa matumizi ya fedha za umma, uchapakazi, ujenzi wa miundombinu, ununuzi wa ndege, ujenzi wa reli ya ‘standard gauge’, elimu bure na upatikanaji wa dawa katika hospitali na zahanati na mambo mengine mengi ambayo yote siwezi kuyataja hapa.

Hii ni ishara kwamba safari yetu kuelekea nchi ya ahadi inazidi kusonga, hatimaye tutafika, hebu fumba macho yako hapo ulipo uifikirie Tanzania miaka michache ijayo; upo katikati ya Jiji la Dar es Salaam unashuhudia treni ya abiria inapita kwa kasi juu ya daraja maeneo ya Kamata kuelekea Morogoro, safari ya saa moja na nusu! Unapita ufukweni eneo la Aga Khan, hapo unashuhudia daraja refu la kilomita tatu hadi Oyster Bay, usiku linawaka taa; bila ubishi Dar es Salaam inafanana kabisa na Hong Kong.

Bwawa la Stiegler’s Gorge liko tayari, nchi yangu Tanzania sasa inajitosheleza kwa umeme na hata kuuza nchi za nje, viwanda vingi vimejengwa na vinalipa kodi ya kutosha kwa maendeleo ya taifa, mauzo yetu ya bidhaa nje ya nchi yameongezeka kuliko tunazoingiza, huko Mwanza nako daraja limejengwa kati ya Busisi na Kigongo ambako hivi sasa watu wanavuka kwa pantoni.

Nchi nzima imeunganishwa kwa barabara, wakulima wanapata ruzuku ya kilimo kila mwaka na mazao yao yana masoko, kilimo sasa hakitegemei mvua ya Mungu, umwagiliaji umetawala na maisha ya Watanzania wengi wanaotegemea kilimo yamebadilika, ingawa maskini bado wapo kwani hata huko Marekani kuna watu wanaishi chini ya madaraja.

Kiwango cha elimu kimeongezeka kama ambavyo pato la taifa ni kubwa kutokana na gesi asilia, hakika maisha ya Watanzania yamebadilika baada ya kipindi kigumu cha mpito walichopitia chini ya utawala wa Rais John Magufuli. Hii ndiyo Tanzania ninayoiota, ninayoitamani, nchi ya ahadi ambayo ili tuifikie lazima tukubali kupita katika maumivu makali leo kwa faida ya kesho na Magufuli ndiye Musa wetu mwenye jukumu la kutupeleka huko.

Mwenye macho haambiwi tazama, mambo mengi mazuri yanafanyika katika Tanzania, ukipita mitaani kama ambavyo huwa napita mimi hutakosa kusikia kauli kama “Rais huyu anafanya kazi kubwa, anajenga madaraja, amenunua ndege, dawa zinapatikana hospitali, lakini…” hiyo lakini ya kumalizia ndiyo itakuja na mlolongo wa malalamiko mengi yanayoonyesha kwamba pamoja na madaraja kujengwa kwa faida yao, si ya rais wala serikali, bado wananchi wana ugumu mioyoni mwao.

Wananchi kukubali kwamba “Rais huyu anafanya kazi kubwa…” ni ishara kwamba utawala bora upo, wanaridhirishwa na yanayoendelea nchini, lakini kuna mahali fulani mioyoni mwao hapajaguswa bado, siku pakiguswa hapa kila mtu atakubali kwamba mambo mema yamefanyika.

Taasisi ya Mo Ibrahim inayoangalia utawala bora katika Afrika imetoa ripoti hivi karibuni kwamba nchi ya Tanzania imepanda kwa nafasi tatu katika utawala bora kutoka nafasi ya 17 hadi ya 14, jambo hili linapotamkwa na taasisi inayoaminika kutoka nje ya nchi ni ishara ya taifa na uongozi wake kukubalika.

Pamoja na hayo yote, swali ninalojiuliza kichwani mwangu kila siku ni kwamba kwa nini kuna mema mengi yanayofanyika hapa nchini tofauti na awamu zilizopita mpaka taasisi za nje kuona lakini bado Watanzania hatuoni? Shida iko wapi? Tatizo ni sisi wananchi au watawala? Maana matarajio yangu yalikuwa kwa jinsi rais anavyofanya mambo mazuri kwa ajili ya nchi angekuwa anashangiliwa kila kona.

Jibu la swali hili ninalipata katika kitabu kiitwacho ‘Unlimited Power’ kilichoandikwa na mwandishi na mhamasishaji maarufu duniani Anthony Robins ambacho ninakisoma hivi sasa, kwenye ukurasa wake wa 388, mwandishi huyo anaandika juu ya nguvu na uwezo wa ushawishi, ya kwamba mwanadamu ana uwezo wa kushawishi au kukubali kushawishiwa.

Kitu hiki kushawishi ndicho kinachofanywa na kila mtu kila siku, uwe unahubiri Injili unachofanya ni kuwashawishi watu waifuate imani yako, uwe mwanasiasa kile unachokifanya ni kuwashawishi watu waifuate itikadi yako, uwe unafanya biashara unachofanya ni kuwashawishiw watu wanunue bidhaa yako, basi! Dunia ya leo ni dunia ya ushawishi, kampuni ya sigara ambayo hutengeneza bidhaa inayoua watu kwa kansa inatumia kiasi kikubwa cha fedha kila mwaka kuwashawishi watu waone sigara ni kitu kizuri. Mwanadamu akishashawishiwa na kukubali, kufuata ushawishi huo kichwani mwake huhitaji gharama kubwa! Mara nyingi watu huendelea kubaki na ushawishi huo vichwani mwao wakiwa wamejijengea ukuta akilini, hawataki kusikia habari nyingine zaidi ya ile waliyosikia mwanzo.

Mtu aliyewahi kuwa jambazi au kushikwa ugoni na mke wa mtu miaka ya nyuma, atakapobadilika na kuamua kuwa muumini wa Injili, bado watu watasema “Jambazi yule, mzinzi yule, amhubiri nani? Nikimkuta mbinguni mtu yule nitasema siy hapa, nitaomba nionyeshwe mbingu nyingine” yote haya ni kwa sababu ushawishi ulishaingia vichwani kabla, kuuondoa na kuwafanya watu wamwamini tena mtu huyo ni kazi ngumu ingawa inawezekana.

Kuna ushawishi ulifanikiwa kupandikizwa vichwani mwa Watanzania kabla ya Rais John Pombe Magufuli kuingia madarakani, umekaa humo na unaendelea kupandikizwa kila siku na wataalam wa kubadilisha mambo; hawa wanawatia watu upofu wa kuona mambo mazuri, wao siku zote wanaona mabaya tu.

Ni kama mtu anapokuwa anaongea Kiingereza mbele ya Waswahili, mahali atakapoongea kwa usahihi hawatasema chochote, ila atakapotamka ‘lice’ akimaanisha wali badala ya ‘rice’ hapo ndipo utasikia kila mtu akiguna na kusema “Jamaa haelewi kabisa lugha ya Kiingereza!” Hata maana nzima ya hotuba iliyokuwa inatolewa hataiona, hata kama ujumbe ulikuwa ni mzuri kiasi gani.

Watanzania walio wengi wameharibiwa kabisa namna ya kutazama mambo sababu ya ushawishi wa wanasiasa, wamefanywa wawe watu wa kutazama ubaya tu katika jambo linalotendeka, rais atajenga madaraja, ataunganisha nchi kwa barabara, atasomesha watoto bure, atajenga reli ya kisasa, lakini bado hawatona, watasema tu “Rais huyu anachapa kazi lakini…” ukifuatilia sana hiyo lakini… inatokana na msimamo wa kiitikadi unaotokana na ushawishi uliopandikiwa vichwani na wanasiasa.

Siasa ni mchezo wa ushawishi, mwenye uwezo mkubwa wa kushawishi ndiye atakayeshinda na kujipatia kura nyingi kisha kuongoza nchi, jimbo au kitongoji! Ushawishi maana yake ni kusema chochote kuonyesha wewe ni bora kuliko mwenzako, hii inakufanya usiongelewe uzuri wowote unaofanywa na mwenzako badala yake tochi yako inaelekezwa kwenye ubaya.

Hiki ndicho kinachofanywa na wanasiasa wengi katika kutafuta ushawishi; kuzungumzia ubaya wa mshidani, huwaingia akilini walio wengi yaani wapiga kura na kuwafanya wawe na makengeneza ya kuona mema yanayofanywa hivyo kuwa na chuki dhidi ya mshindani.

Ndiyo maana serikali itafanya kila kitu vizuri, lakini sababu washindani walishapandikiza chuki vichwani mwa wapiga kura, bado wananchi hawataipenda serikali, itawagawia hadi chakula lakini bado watasema “Wanatushawishi ili tuwape kura kipindi kijacho” walishajenga ukuta akilini mwao, hawataki taarifa yoyote iingie, sababu walishashawishiwa.

Sababu ya pili inayofanya Watanzania, hasa Wasukuma, kuonyesha chuki hata kama wanafanyiwa mambo mema ni kauli! Kauli yoyote unayotoa mbele ya Mtanzania hubaki moyoni mwake kwa muda mrefu mno na anaweza akacheka mbele yako sababu kuna kitu anapata lakini moyoni amejaa chuki kupindukia ambayo utaishuhudia mbele ya safari. Tajiri mmoja huko kwetu alikuwa anagombea uongozi akishindana na mwananchi mwenye uwezo mdogo kifedha, kwa sababu ya utajiri wake akawa anawagawia watu vitu huku akiwatolea kauli mbaya, wananchi wakawa wanapokea vitu hivyo usoni wakiwa na tabasamu, yeye akaamini sababu ya utajiri wake angeshinda uchaguzi.

Siku ya mwisho kura zilivyopigwa tajiri alishindwa na maskini, hakuamini! Kilichomponza tajiri si kingine ni kauli zake, alikuwa mkarimu kupita kiasi akisaidia maskini, tunajifunza nini hapa? Somo hapa ni kwamba, pamoja na matendo yetu mema tunayofanya kwa wananchi yapasa yaambatane na kauli njema ambazo hazitajenga taswira kwamba serikali ni kali kupindukia.

Simaanishi kuwa kauli zinazotolewa ni mbaya, bali jinsi zinavyowasilishwa, si katika mtindo ambao Watanzania wameuzoea, matokeo yake wanatafsiri vibaya na kuanza kuiona serikali katika taswira isiyo sahihi, kinachotakiwa kufanyika hapa ni kuboresha, kama lengo ni kumwita mtu unaweza kusema “Njoo” badala ya kusema “Kuja hapa” lengo ni moja lakini uwasilishaji ndiyo tofauti, taswira atakayoijenga mtu kichwani baada ya kuambiwa “Kuja hapa” badala ya “Njoo” ndiyo itakayofanya asiuone kabisa wema wa mtoa kauli.

Nionavyo mimi nchi yetu inaye rais mwema, anayechukia ufisadi, anayefikiria wanyonge kila kukicha na nina uhakika halali usingizi kwa ajili yao, sioni dalili ya yeye kujitajirisha, kumbukumbu zinaonyesha kwamba si fisadi na nia yake kwa taifa ni njema, ameipandisha Tanzania katika viwango vya utawala bora Afrika.

Sababu mbili nilizozitaja hapo juu; ushawishi wa wanaompinga ambao tayari ulishaingizwa kwenye akili za watu na kauli ndizo zinazofanya watu kuwa na upofu wa kuyaona mema yanayotendwa, kama hivyo ndivyo basi kinachoweza kufanyika ni kubadilisha tu kauli zetu huku tukiendelea kutenda mema na pia wananchi kujengewa uwezo wa kupembua pumba na mchele pale ushawishi unapoletwa mbele yao. Mambo haya yakifanyika, na Watanzania wakashikamana pamoja, safari kuelekea kwenye Tanzania tunayoitamani itafikia mwisho kwa ushindi mkubwa.

Reli ya kisasa

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.