Wanaume kuanza kunyonyesha 2023

Rai - - MAKALA AFRIKA - NA HASSAN DAUDI

HEBU vuta picha mmoja kati ya wafanyakazi wenzako wa kiume anakwambia kesho atachelewa kufika ofisini na unapomuuliza sababu anakwambia atakuwa anamnyonyesha mtoto wake.

Au wakati unamsubiri kaka yako mliyekubaliana kukutana katika kituo cha daladala, anakupigia simu na kukuomba usikasirike kwani hatafika.

Unapomuuliza sababu, anakupa jibu linalofanana na lile, eti ameona amsaidie kumnyonyesha mkewe kumnyonyesha mtoto wao wa kike!

Bila shaka hilo linaweza kukushangaza kwa sasa lakini nikwambie tu kuwa haitakuwa hivyo miaka mitano ijayo, yaani litakuwa nijambo la kawaida kabisa kwa mwanaume kunyonyesha.

“Kifaa maalumu kitakachomwezesha mwanaume kunyonyesha kitakuwa kimeshawafikia wengi duniani kote,” kwa mujibu wa taarifa ya wataalamu waliobuni wazo hilo.

Hakika hiyo inaweza kuwa habari njema kwa wanawake wengi duniani, ambao huubeba mzigo wa kunyonyesha kwa takribani miaka miwili baada ya kujifungua.

Wagunduzi hao wamedai kuwa kwa kipindi chote cha ujauzito wa mwenza wake, baba mtarajiwa atakuwa akitumia dawa aina ya Domperidone ambazo huchochea ongezeko la homoni zinazoziwezesha chuchu kuzalisha maziwa.

Je, ni wakati gani mwanaume ataanza kutumia dawa hizo ambazo matumizi yake kwa sasa ni kuwasaidia wanawake wasio na maziwa ya kutosha ya kunyonyesha watoto wao?

“Ikiwa imebaki miezi sita kabla ya mwanamke wake kujifungua, ndipo mwanaume ataanza kujiandaa kwa kunywa Domperidone mara nne kwa siku,” inafafanua taarifa ya wanasayansi hao.

Mmoja kati ya wataalamu walioibua wazo hilo, Marie-Claire Springham, alisema teknolojia hiyo ni nzuri, hivyo anaamini wapenzi wataikimbilia hapo baadaye.

“Sioni sababu ya wenza kutoifuafa teknolojia hiyo,” anasema Springham katika mahojiano yake na gazeti kongwe nchini Uingereza, Daily Mail.

Akisisitiza ni wakati wa wanaume kuwasaidia wake au wapenzi wao katika jukumu hilo la kunyonyesha, msomi huyo mwenye umri wa miaka 24 aliongeza:

“Unajua kuna wanawake huwa wanapata tabu kunyonyesha. Sasa hii ni kama kuwaonea huruma, kwamba wanaume wanaweza kuwasaidia.”

Kwa namna njia hiyo itakavyofanya kazi, mrija utakaotoka katika chuchu za mwanaume ndiyo atakaoutumia mtoto kunyonya maziwa ya baba yake.Kwa kuwa inaaminika itachukua muda mrefu kwa mwili wa mwanaume kukubaliana na mabadiliko hayo, anashahuriwa kutumia dawa mara nne kwa siku pindi ujauzito wa mpenzi au mkewe utakapofikisha miezi sita.

Lakini sasa, bado kuna shaka juu ya ubora wa maziwa atakayozalisha mwanaume. Hapo swali ni je, yatakuwa na virutubisho vinavyofanana na vile anavyovipata mtoto kutoka kwa mama yake? Huenda hilo litakuwa limeshapata ufumbuzi kufikia 2023. Pia, kuna wasiwasi kuwa njia hiyo inaweza kuzifanya chuchu za wanaume kuongezeka ukubwa, hata kufanana na za wapenzi, wake, au dada zao.

Kama itakuwa hivyo, ni wazi inaweza kuharibu mwonekano wa kijana wa kiume aliyeamua kumsaidia mpenzi au mkewe kunyonyesha.

Aidha, wanasayansi wanaamini teknolojia hiyo ina uhusiano mkubwa na jamii zetu, hasa katika jitihada zinazoendelea za usawa wa kijinsia.

Mbali na hilo, wanasema itaibua mijadala mingi katika kila ya dunia na huenda zikazaliwa gunduzi zingine zitakaleta njia mbadala za wanaume kuwasaidia wanawake wao kunyonyesha.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.