Vichai: Bilionea aliyefariki na kuacha simanzi EPL

Rai - - MBELE - NA HASSAN DAUDI NA MITANDAO

WIKI iliyopita ilimalizika vibaya si tu kwa mashabiki wa klabu ya Leicester City, bali pia kwa wapenzi wa kandanda England, Ulaya na ulimwenguni kote. Baada ya kutoka kuishuhudia timu yake ya Leicester ikitoka sare ya bao 1-1 na West Ham, bilionea wa Leicester raia wa Thailand,

WIKI iliyopita ilimalizika vibaya si tu kwa mashabiki wa klabu ya Leicester City, bali pia kwa wapenzi wa kandanda England, Ulaya na ulimwenguni kote.

Baada ya kutoka kuishuhudia timu yake ya Leicester ikitoka sare ya bao 1-1 na West Ham, bilionea wa Leicester raia wa Thailand, Vichai Srivaddhanaprabha, alipanda helikopta yake kurejea nyumbani lakini ghafla ilianguka nje ya uwanja wao wa King Power.

Ni kawaida kwa tajiri huyo aliyeacha mke na watoto wane kutumia helikopta yake hiyo aina ya Augusta AW169 kufika uwanjani hapo kila Leicester inapokuwa ikicheza.

Akiwa na utajiri wa Dola za Marekani bilioni 3.3, jarida la Forbes la Marekani lilimtaja kushika nafasi ya saba katika orodha ya matajiri huko Thailand.

Kuthibitisha kifo chake, taarifa ya Leicester ilisema: “Kwa hali ya huzuni kabisa, tunathibitisha kuwa mwenyekiti, Vichai Srivaddhanaprabha, alikuwa mmoja kati ya watu watano waliopoteza maisha.”

Jina lake katika soka la England lilianza kuchomoza mwaka 2010, alipotumia kiasi cha Pauni milioni 39 (zaidi ya Sh bil 114 za Tanzania) kuinunua Leicester.

Hata hivyo, kilichowafanya wengi kutaka kumjua zaidi ni kitendo chake cha kuiwezesha kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu ya England mwaka juzi, akifanya hivyo miezi michache baada ya timu hiyo kunusurika kushuka daraja.

“Aliifanya (Leicester) kuwa klabu kubwa Ligi Kuu England,” alisema SvenGoran Eriksson, kocha wa kwanza kuajiriwa na Vichai baada ya kuinunua Leicester.

Pia, aliwaacha hoi mashabiki wa soka wa England kwa kumpa kila mchezaji gari la kifahari aina ya BMW i8, ambalo kwa kipindi hicho moja liligharimu Pauni 100,000 (zaidi ya Sh mil 290 za Tanzania), ikiwa ni zawadi ya kuchukua ubingwa.

“Vichai alikuwa mmoja kati ya watu wazuri ambao ungependa kukutana nao. Mara nyingi ungemuona akitabasamu na kucheka.” anasema Jamie Vardy, mshambuliaji wa Leicester aliyekuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa ubingwa msimu wa 2015-16.

Ukiacha historia yake hiyo EPL, kifo chake kimewagusa wanasoka wengi wenye asili ya Afrika, kwani Leicester City ndiyo timu pekee yenye idadi kubwa ya wachezaji wanaotokea barani humo.

Nyota wa timu ya taifa ya Nigeria, Wilfred Ndidi, anafichua kuwa bosi huyo alikuwa akisafiri hadi Urusi kumtazama akiiwakilisha Super Eagles katika kila mchezo wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu zilizomalizika miezi michache iliyopita.

Mbali na Ndidi, sehemu ndogo tu ya wanasoka wengine wa Afrika waliotuma salamu zao rambirambi ni Kelechi Iheanacho, Rachid Ghezzal, efender, Yohan Benalouane, Fousseni Diabate, Riyad Mahrez, na Ahmed Musa.

Ilikuwa ni nadra kumsikia au kumuona Vichai akizungumza na waandishi wa habari na badala yake mara nyingi kazi hiyo ilifanywa na mtoto wake wa kiume, Aiyawatt, ambaye ndiye makamu wa rais klabuni hapo.

Mmoja kati ya watu ambao hawatamsahau ni Jose Ragoobeer, mkazi wa mjini Leicester, ambaye anasema alipofiwa na mke na watoto kutokana na mlipuko wa bomu, bilionea huyo ndiye aliyemsaidia.

Kwa upande wao, mashabiki wa Leicester wataendelea kukumbuka kitendo cha Vichai kuwapa bia za bure kila walipokuwa wakiishangilia timu yao kwenye uwanja wa nyumbani.

Aidha, wakati akisherehekea kutimiza umri wa miaka 60 miezi miezi sita iliyopita, mashabiki 60 walijipatia tiketi za bure za kutazama mitanange ya EPL.

Naye mkongwe wa Leicester ambaye kwa sasa ni balozi wa timu hiyo, Alan Birchenall, alisema kuondoka kwa Vichai ni pigo kubwa kwao. “Tusingeuchukua wala kuukaribia ubingwa kama si yeye,” alisema.”

Kuondoka kwake kunaiacha Leicester katika mikono salama ya familia yake kwani watoto wake wote wanne, wakiwamo wawili wa kike, wanashikilia nyadhifa za juu ndani ya klabu hiyo.

Igawa wengi wanaifahamu zaidi Leicester, Vichai ameondoka akiwa pia ni mmiliki wa klabu ya soka ya OH Leuven inayoshirikia Ligi Daraja la Kwanza nchini Ubelgiji.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.