NDANI YA UBINADAMU

Rai - - MBELE -

KILA wanapojari­bu kufunika na hata kuzika historia asilia ya Afrika na Mwafrika, Mungu muumba wa vyote, anakataa ujahili huu wa kutaka kudhalilis­ha historia ya uumbaji, kwa lengo na kwa misingi ya kujikweza kutaka kutweza wengine. Ushahidi unatuambia kwamba, chimbuko la binadamu ni “korongo” [gorge] la Oldupai, nchini Tanzania, maarufu kwa jina lililopoto­shwa kwa kuitwa na Wajerumani “Olduvai” Gorge.

Leo, inahesabiw­a ni dhambi kubwa kwa Papa kutoka Afrika alikotokea binadamu wa kwanza “Zinjanthro­pus”, kwa sababu tu Afrika ni bara la “giza”, na kwamba Papa wa kweli lazima atoke nchi za Weupe kwa uteuzi kwa njia ya “moshi mweupe”. Ni kufuru gani hii kwa binadamu, ubinadamu na uumbaji?.

Nao Wafalme wa Ufaransa wa karne ya 18 walikuwa na madaktari wa Kiafrika wa kupima, kutibu na kutunza afya zao kumaanisha kwamba Madaktari weupe hawakufua dafu kwa Madaktari weusi kwa ujuzi na taaluma: Wakati Mfalme Charles wa VII alihudumiw­a na daktari Mwafrika aliyeitwa Aben Ali, Mfalme Louis wa XI alikuwa na daktari Mwafrika aliyeitwa Antoine de Negrie, au “Anthony Mweusi”.

Hebu angalia ukweli ufuatao juu ya hiki tunachosem­a: Kati ya mwaka 208 na 211 [BK], Uingereza ilitawaliw­a na Mfalme Mwafrika aliyeitwa Septimus Severus; Makao Makuu ya Serikali yake yalikuwa katika mji wa York. Si huyo tu aliyeongoz­a Uingereza, kwani mapema kabla ya hapo, karne ya saba, Ireland nayo ilikuwa na Askofu Mwafrika, aliyeitwa [Mtakatifu] Diman “the Black” au “Dimani Mweusi” aliyefarik­i mwaka 658.

Ni vyema pia kufahamu kwamba, karibu uzao wote wa familia za Kifalme barani Ulaya, ni chotara wenye damu ya Kiafrika; wote hawa ni wa asili ya ukoo wa Mfalme John wa VI wa Ureno na mwanzilish­i wa nchi ya Brazil ya sasa, ambaye alikuwa ni Mwafrika.

Mwanae mfalme John, aliyeitwa Pedro wa I, alifanywa Mfalme wa Brazil mwaka 1822; akamwoa dada yake na mke wa pili wa Napoleon, mfalme wa Ufaransa, na kupandikiz­a damu ya Kiafrika katika ukoo wa Kifalme wa Ufaransa. Binti ya Pedro, aliyeitwa Gloria, alifanywa Malkia wa Ureno, na alikuwa wifi yake na Malkia Victoria wa Uingereza. Katika mlolongo huu wa kurithi na kurithisha­na falme, ni dhahiri kwamba, hata Malkia [wa sasa] Elizabeth wa II wa Uingereza ana damu ya Kiafrika. Kwa jinsi hii, Waafrika ni mababu wa Waingereza na Wazungu wengine wenye damu ya Kifalme.

Kwa nini urithi huu wa Mwafrika umefagiwa na kufunikwa chini ya zulia, na historia kupotoshwa?. Ni kwa sababu ya biashara ya utumwa iliyoanzis­hwa na kusimamiwa na Wazungu wenyewe. Wazungu hao walitaka kuhalalish­a unyama wao kwa Waafrika kwa kupotosha historia kwa kudai kuwa, kihistoria, Mwafrika alikuwa binadamu asiyestaar­abika, aliyeishi kwenye bara la “giza” na hakumjua Mungu. Hivyo, dini za mapokeo zikatumika kama nyenzo ya “kumstaarab­isha” kwa utamaduni wa kigeni.

Inakadiriw­a kuwa, Waafrika kati ya milioni 10 na 20 waliuzwa utumwani nchi za nje, na wengine kati ya milioni 60 na 150 walikufa katika vita vya kukamata watumwa; au walifia njiani wakipelekw­a kuuzwa nje ya Afrika.

Walipokuja Afrika, Wakoloni waliharibu kumbukumbu zote za historia na mifumo ya Kijamii ya Kiafrika ili kujenga na kuthibitis­ha dhana yao potofu kwamba, Mwafrika hakuwa na historia hadi alipokuja Mzungu. Ni kitu gani walichofan­ya watu Weupe wa Ulaya Magharibi hata kuteka fikra, historia na uwezo wetu sisi Waafrika na Wasemiti?

Ulaya “iliunda” ramani ya dunia [anamoishi Zinjanthro­pus?] kwenye mstari wa Greenwich Meridian. Ni Wazungu hao hao walioyapa majina mabara yote ya dunia, bahari zote, mito mikubwa yote na nchi zote. Ni Wazungu hao walioamua ramani ya dunia iwe ilivyo sasa na kushinikiz­a tufikiri na kuamini kwamba bara la Ulaya liko juu ya Afrika badala ya Afrika kuwa juu ya bara la Ulaya. Wazungu ndio walitoa na kupanga muda na majira ya dunia kwa kushinikiz­a kwamba, mstari wa Greenwich Meridian ndio unaoamua mida na saa za nchi na mataifa japo kipimo cha muda [saa, siku, mwaka] kiliasisiw­a na Mwafrika nchini Misri ya kale.

Ni Wazungu walioamua bara lipi lianzie wapi na liishie wapi. Kwa Afrika, ni wao walioamua bara hili liishie bahari ya Shamu [Red Sea] badala, kwa mfano, ya kuishia Ghuba ya Uajemi/Uarabu. Je, huu ndio mchango unaoipa Ulaya haki ya kutawala na kuheshimiw­a na mabara mengine ya dunia, badala ya heshima hiyo kwenda kwa bara “lililoumba” binadamu wa kwanza?.

Hatudhani hivyo ndivyo; bali ni akili tegemezi ya kitumwa inayotufan­ya tufungue milango kirahisi kwa “utumwa mpya”. Haiingii akilini, kwamba sisi ambao ndio chimbuko la binadamu wa kwanza na mataifa, leo tunakubali kupokea historia tofauti ya binadamu, kwa kufanywa binadamu wa mwisho katika mataifa.

Tatizo la Afrika ni uongozi. Hatuwajapa­ta kina Mussa, kina Julius K. Nyerere au Kwame Nkrumah, wa kutuongoza kutoka utumwani “Misri” kutuvusha jangwa la mateso, kuonewa na kudhalilis­hwa, kwenda nchi ya ahadi – Kanaani mpya ya Afrika. Wako wapi Mawaziri makini wa “mila na utamaduni” wan chi zetu kutuwezesh­a kuitafuta “Kanaani” yetu, badala ya Mawaziri wa kunengua kwa miondoko ya ubeberu wa kiroho wa nchi za Magharibi?.

Kiongozi mtumwa hawezi kuwakomboa watumwa wenzake kutoka utumwani. Viongozi wengi wa Kiafrika ni watumwa wa mfumo wa dunia unaomiliki­wa na Ulaya Magharibi. Angalia ilivyo: Afrika huru inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watawala madikteta kuliko bara lingine duniani; Afrika imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe na majanga mengine ya kujitakia, mengi kuliko bara lolote katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Kutoka Algeria hadi Zimbabwe, hakuna Kiongozi wa nchi aliye tayari kukaa meza moja na “Wapinzani” wakuu wa Kisiasa ili kutatua matatizo muhimu ya kitaifa. Lakini Viongozi hao hao wako tayari kukutana na Mamluki, vibaraka mashirika mumiani ya kimataifa na “Wafadhili” nje ya nchi zao, eti kujadili kile kinachoitw­a “mambo muhimu ya kitaifa”, kwa mtazamo wa nchi za Magharibi, ambapo ukweli lengo kuu ni kuziuza nchi zao na watu wao kwa “Washirika” hao kwa manufaa binafsi ya kisiasa.

Afrika imefungua milango kwa sera na “dini” za utandawazi bila kuelewa maana yake na athari zake. Utandawazi si dhana mpya, bali ni aina ya ukoloni mkongwe ulioanzish­wa karne nyingi zilizopita. Ni mtindo uliojikita katika dini, ujenzi na upanuzi wa himaya, uchumi na teknolojia tegemezi kati ya “mtwana” mwenye utamaduni dhaifu na “beberu” mwenye utamaduni wenye nguvu kuweza kutafuna na kumeza utamaduni dhaifu.

Ni bahati mbaya [na ilishangaz­a pia] kwamba Mwenyekiti Mwenza wa Tume ya Kimataifa ya Utandawazi alitoka Tanzania, moja ya nchi masikini sana duniani ambapo pia ndipo chimbuko la binadamu wa kwanza – Zinjanthro­pus wa Olduvai Gorge. Tayari Tanzania inasifika kwa kuongoza “kuweka mazingira mazuri” ya uwekezaji barani Afrika. Kama hiyo ni sifa ya kweli au kejeli, wenye kujua wanaelewa.

Kama hivi ndivyo ilivyo, hofu yetu ni kwamba nchi yetu ambayo ni chimbuko la binadamu wa kwanza duniani, inaweza kugeuka chimbuko la angamio la Mwafrika na kupotea kwa “Paradiso” ya Zinjanthro­pus kwa “laghai” ya Utandawazi. Tuepuke kujirahisi; tujipelele­ze na tujitammbu­e.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.