Tuwalinde wafanyabiashara wa DRC

Rai - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

MOJA ya kazi nzito na ngumu alizopata kuzifanya Rais Dk. John Magufuli katika kipindi chake cha miaka mitatu ni kuwarejeshea imani wafanyabiashara hasa wa nje kuendelea kuitumia bandari ya Dar es Salaam, kusafirisha na kupokea mizigo yao.

Alifanya hivyo baada ya wafanyabiashara wengi hasa kutoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo –DRC, Rwanda na nchi nyingine jirani zilizokuwa zikitumia bandari hiyo kupungua.

Kupungua kwa wafanyabiashara hao kulitajwa kusababishwa na kero, urasimu, wizi na rushwa vilivyokuwa vikifanywa na baadhi ya waliokuwa watumishi katika bandari hiyo, ambao sasa wameshang’olewa.

Moja ya jitihada za Rais Dk. Magufuli ni kuufumua uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) pamoja na kutana na viongozi wa baadhi ya mataifa yanayotumia bandari ya Dar es Salaam kwa nia ya kuwajengea imani.

Ukweli ni kwamba kati ya mwaka 2015/16 hali ya kibiashara ndani ya bandari hiyo haikuwa nzuri, mizigo ilidaiwa kupungua kwa kasi siku hadi siku.

Haraka Rais Dk. Magufuli akamwalika Rais wa DRC, Joseph Kabila ili pamoja na mambo mengine awe msaada wa kuwashawishi wafanyabiashara wan chi yake kutumia bandari ya Dar es Salaam.

Oktoba 3, 2016 Rais Kabila alitua nchini kwa ziara rasmi ya kiserikali ya siku tatu, Rais Dk. Magufuli alimpokea mgeni wake katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Mizinga 21 ilipigwa na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa ajili yake na baadaye kushuhudia burudani ya vikundi vya ngoma.

Oktoba 4, 2016 Rais Dk. Magufuli alifanya mazungumzo rasmi na Rais Kabila pamoja na kuweka jiwe la msingi la jengo la TPA.

Katika hafla ya kuweka jiwe la Msingi la jengo al TPA, Rais Dk. Magufuli alimwambia wazi mgeni wake kuwa sasa matatizo madogomadogo yaliyokuwa bandarini hapo yamekwisha na waliosababisha yote hayo wameondolewa, hivyo ni vema akawahamasisha wafanyabiashara wan chi yake kuendelea kuitumia Bandari ya Dar es Salaam.

Rais Dk. Magufuli alisema awali bandari hiyo lilitawaliwa na rushwa na wakati mwingine mizigo ya watu ilikuwa inapotea, vitendo vilivyo kuwa vinafanywa na wafanyakazi ambao hawakujali maslahi ya taifa.

Hata hivyo Dk. Magufuli alisema usafirishaji wa mizigo kutoka DRC umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka kwa asilimia 10.6.

“Mwaka jana (2015) makontena yaliyopita hapa yalikuwa zaidi ya 15,927, lakini biashara kati ya Tanznaia na DRC pia imekuwa ikiongezeka, kwa sababu mwaka 2009 biashara kati ya nchi hizo zilikuwa bilioni 23.

“Mwaka jana (2015) imefikia bilioni 396.3 sasa kwa kuzingatia mwelekeo huo, na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na DRC na urafiki uliopo kati ya DRC na Tanzania nilifikiria mtu wa kuweka jiwe la msingi ni Joseph Kabila.”

Rais Kabila alishukuru heshima hiyo na kuahidi kuwa nchi yake itaendelea kuboresha biashara hasa katika sekta ya usafirishaji na sasa hakuna haja ya kupiga debe kwa wafanyabiashara kuja kutumia bandari hiyo kwani yanayofanyika ya uboreshaji yatawavutia na changamoto itabakia kuwa uwezo wa badari.

“Ukweli ni kwamba miaka minne mitano iliyopita, biashara ilikuwa imeshuka na kulikuwa na sababu ambazo wewe mwenyewe (Rais Magufuli) umezitaja , wafanyabiashara wetu na hasa makampuni ya serikali waliona kuna matatizo ndani ya bandari ya Dar es Salaam, lakini miezi michache iliyopita wameona mabadiliko na mambo ni shwari zaidi.”

Ukweli ni kwamba baada ya jitihada hizi za Rais Magufuli, mambo yalibadilika na tija ilionekana kwani mizigo iliongezeka bandarini.

Kwa bahati mbaya sana sasa kunaonekana kuwapo kwa dalili za makusudi ama za kimkakati zenye nia na lengo la kuturudisha tulipotoka.

Maroli yaliyobeba bidhaa za wafanyabishara wan je hasa DRC, sasa yanalazimika kusubiri kwa kati ya siku saba mpaka 15 ili kupata ridhaa ya kuanza safari.

Idadi kubwa ya maroli imekwama Misugusugu, Kibaha mkoani Pwani, kukiwa na hoja kuwa maroli hayo yanasubiri maofisa wa serikali kuyasindikiza, huku ikielezwa kuwa magari hayo yamefungwa vifaa maalum vya kuwafuatilia.

Huenda uamuzi huu una nia na dhamira njema, lakini ukweli ni kwamba unaweza kuharibu na kuvuruga kabisa jitihda za Rais za kuwarudisha wafanyabiashara wa DRC.

Madereva wanalalamika kwa kukaa muda mrefu Misugusugu, wakisubiri wasindikizaji kutoka Serikalini, hudumu zilizopo katika eneo hilo ambalo hadi kufikia juzi Jumanne lilikuwa limekusanya zaidi ya madereva na wasaidizi wao 70 ni mbovu zisizo ridhisha.

Kama hilo halitoshi hata hoteli hakuna, hali inayowafanya watu hao kulala kwenye maeneo hatarishi yanayowasukuma kuhatarisha afya zao.

Chuki Shabani, Mwenyekiti wa Wamiliki wa Maroli wadogo na wa Kati, ameweka wazi kuwa hali hiyo kama itaachwa iendelee inaweza kutowesha imani za wafanyabiashara wa DRC.

“Namwomba Kamishna wa TRA alitazame upya suala hili, hii ni hatari sana kwa mustakabali wa uhusiano wa kibiashara kati yetu na DRC, haiwezekani mfanyabiashara asubiri mzigo wake kwa muda mrefu halafu aendelee kufanya biashara na wewe.

“Lakini pia hili eneo si salama kwa watu kukaa kwa muda mrefu, ni vema kukawa na utaratibu mzuri wa magari kutoka bandarini yakiwa na uhakika wa kufika hapa (Misugusugu) na kuondoka, kwa maana maofisa wasindikizaji waandaliwe kabisa na kama hawapo hakuna haja ya kuruhusu magari kuja hapa,”alisema.

Tayari Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo ameshasema kuwa suala hilo linashughulikiwa kikamilifu, Chuki anasema kuwa Serikali haipaswi kuchelewesha kushughulikia suala hili kwa sababu tunazo kila sababu za kuwalinda wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali nje na ndani ya nchi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.