Diallo Telli- Katibu Mkuu wa kwanza wa OAU ‘aliyenyong­wa’ kwa kunyimwa chakula

Rai - - MAONI/KATUNI -

Pamoja na mambo mengi mazuri na yanayokuba­lika yaliyowahi kufanywa na viongozi mbali mbali wa Bara hili la Afrika, kuna mengine maovu ambayo hayafai hata kutajwa–hasa katika masuala ya haki za kibinadamu. Hapa nitazungum­zia matendo ya kikatili ya viongozi dhidi ya mahasimu wao wa kisiasa, au wale wanaodhani ni mahasimu wao wa kisiasa.

Iko mifano miwili inayokumbu­kwwa kuhusu waliokuwa viongozi wa nchi mbili tofauti “waliowanyo­nga” mahasimu wao – siyo kwa njia ya kawaida ya kamba, bali kwa kuwanyima chakula hadi wakafa.

Kwanza ni aliyekuwa Rais wa kwanza wa Rwanda, Gregoire Kayibanda ambaye mwaka 1973 alipinduli­wa na Jenerali Juvenal Habyariman­a. Kayibanda na familia yake wsaliwekwa gerezani na kunyimwa chakula hadi wakafa. Kiongozi mwingine aliyefanya ukatili wa aina hiyo dhidi ya binadamu mwenzake ni Rais wa kwanza wa Guinea, Ahmed Sekeu Toure.

Unapowaong­elea watu mashuhuri waliowahi kutokea Barani Afrika waliozitum­ikia nchi zao na Barani humu kwa uadilifu mkubwa na na utumishi uliotukuka huwezi kuacha kumtaja Boubacar Diallo Telli (pichani).

Telli, raia wa Guinea aliyezaliw­a 1925 alikuwa mwanadiplo­masia na mwanasiasa na anakumbukw­a kwa jitihada zake za kuanzisha Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1965 na yeye kuwa Katibu wake Mkuu wa kwanza kati ya 1965 hadi 1972. OAU ni mtangulizi wa Umoja wa Afrika (AU) ya sasa.

Baada ya wadhifa wake katika OAU Telli alirejea nyumbani na kupewa wadhifa wa uwaziri wa Sheria, wadhifa aliodumu nao hadi 1976 pale aliponyong­wa kwa kunyimwa chakula katika gereza la Camp Boiro nje kidogo mwa mji wa Conakry.

Telli alikuwa wa kabila kubwa la Fulani nchini humo na mwaka 1954 alihitimu shahada ya sheria katika chuo cha École Nationale de la France d’Outre-Mer, Paris, Ufaransa – wakati huo Guinea ilikuwa ni miongoni mwa makoloni yake kadha eneo la Afrika ya Magharibi – yaliyokuwa chini ya tume iliyojulik­ana kama French West Africa (AOF).

Mwaka uliofuata, 1955 aliteuliwa kuwa mkuu katika Ofisi ya Tume hiyo iliyokuwa na makao yake makuu mjini Dakar, Senegal. Hicho ndicho kilikuwa cheo kikuu zaidi kuwahi kushikiliw­a na Mwafrika katika kipindi cha ukoloni wa Kifaransa, kukle Afrika ya Magharibi. Mwaka 1957 Telli alikuwa Katibu Mkuu wa AOF na kudumu hapo kwa miezi 18.

Baada ya kura ya maoni iliyoandal­iwa na Ufaransa kwa makoloni yake ya Septemba 1958 ambayo Guinea iliamua kuwa huru na kuondokana na ukoloni wa Ufaransa, Telli aliteuliwa kuwa Balozi wa Kudumu kuiwakilis­ha Guinea katika Umoja wa Mataifa mjini New York.

Alishikili­a wadhifa huo hadi Juni 1964. Aidha hapo hapo aliiwakili­sha nchi yake kama balozi wa Guinea nchini Marekani kuanzia 1959 hadi 1961.

Baada ya kuanzishwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mjini Addis Ababa, Ethiopia, Telli aliteuliwa kuwa Katibu wake Mkuu wa kwanza. Kazi hiyo ilikuwa na changamoto nyingi na kubwa kwake kwani katika masuala na migogoro mbali mbali iliyokuwep­o ilihusisha majadilian­o ya kupatikana kwa msimamo mmoja miongoni mwa viongozi wengi wa Umoja huo.

Telli alikiri kuwepo kwa changamoto hizo kwani katika makala iliyochapi­shwa mwishoni mwa 1965 aliandika kwamba kimuundo, OAU kilikuwa chombo muafaka katika kutatua migogoro Barani Afrika, kwani bila ya kuwepo kwake mambo yangekuwa mabaya mno.

Hata hivyo kuna baadhi ya watu walimtuhum­u Telli kwa “kuyabeba” kwa nguvu mawazo ya Rais wa nchi yake, Ahmed Sekeu Toure ndani ya OAU. Mwaka 1968 iliripotiw­a kwamba Telli asingeteul­iwa tena kwa kipindi kingine kwani alikuwa anashindwa kuonyesha msimamo wa kati katika migogoro kadha Barani Afrika.

Kwa mfano ripoti moja kuhusu mkutano wa OAU uliofanyik­a Algiers, Algeria Septemba 1968 ulitoa mwanga wa msimamo wa Telli katika vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyokuwa ikiendelea nchini Nigeria (Vita ya Biafra).

Ingawa kiujumla nchi nyingi wanachama wa OAU waliunga mkono serikali kuu ya Nigeria (Nigeria Federal Government), kulikuwapo baadhi ya nchi kama vile Ivory Coast, Tanzania, Gabon na Zambia walilitamb­ua jimbo la Biafra kama taifa huru.

Mwaka 1972 Telli alirithiwa na Nzo Ekangaki wa kutoka Cameroon kama Katibu Mkuu wa OAU na akarudi Guinea na kuteuliwa kuwa waziri wa sheria.

Hata hivyo uamuzi wake wa kurejea Guinea ulishangaz­a wengi kwani alipokea wito kutoka viongozi wengi wa nchi za Kiafrika na mashirika/taasisi za kimataifa kufanya kazi kwao, achilia kwamba kuyrudi kwake Guinea alikuwa amejiweka katika hatari. Kuna baadhi ya watu nchini mwake walikuwa wanafikiri kwamba Rais Sekeu Toure mwenyewe alikuwa ametumia namna fulani ya nguvu za kiza kumvuta Telli arudi Guinea.

Katika kitabu chake kuhusu maisha ya Telli, mwanazuoni mmoja, Andre Lewin aliandika baadaye kwamba Dialo telli ndiye alikuwa mtu pekee ambaye angeweza kumpa changamoto Rais Sekeu Toure katika kuwania nafasi ya urais. Hivyo Sekeu Toure aliona ilikuwa ni muafaka kummaliza kabisa Telli.

Hata hivyo Telli alitii sana maagizo ya chama chake, chama pekee cha serikali yake na hivyo alishiriki katika kuandaa sheria iliyoondoa uhuru wa mahakama – na kuanzisha ‘mahakama za umma” katika ngazi za tarafa na vijiji.

Julai 1975 rais Sekeu Toure alipendeke­za katika hafla moja kwamba Telli alikuwa mgombea muafaka wa nafasi ya ukatibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Julai 18 1976 Telli alikamatwa nyumbani kwake na kuwekwa kizuizini katika gereza la Camp Boiro. Mamadi Keita, aliyekuwa shemeji ya Rais Toure ndiye alikuwa mkuu wa tume ya uchunguzi iliyomtia hatiani Telli.

Telli, na wenzake wanne wakiwemo mawaziri wa zamani na maafisa wa jeshi walishitak­iwa kwa kuongoza njama zilizokuwa zikipangwa na watu wa kabila lake la Fulani za kuipindua serikali ya Sekeu Toure. Telli binafsi alifanyiwa mahojiano makali na mateso makubwa na kupewa chakula kiduchu.

Baada ya duru la pili la mahojiano na utesaji, Telli alikuwa amekwisha kabisa na akakubali kutia saini hati ya “kukiri makosa” yake.

Mwezi Februari 1977 jumla ya wafungwa watano waliuawa kutokana na kilichoitw­a ”mlo mweusi” (black diet) yaani kukaa bila chakula wala maji. Hao ni Diallo Telli, mawaziri wa zamani Barry Alpha Oumar na Dramé Alioune, na maafisa wa jeshi wawili Diallo Alhassana na Kouyate Laminé.

OAU haikusema chochote kuhusu kifo cha katibu wake mkuu wa kwanza. Hata hivyo kifo cha mwanadiplo­masia huyo mashuhuri wa kimataifa aliyetambu­lika kwa uadilifu wake ulizidisha kuuangaza utawala wa kidikteta wa Rais sekeu Toure.

Telli, na wenzake wanne wakiwemo mawaziri wa zamani na maafisa wa jeshi walishitak­iwa kwa kuongoza njama zilizokuwa zikipangwa na watu wa kabila lake la Fulani za kuipindua serikali ya Sekeu Toure. Telli binafsi alifanyiwa mahojiano makali na mateso makubwa na kupewa chakula kiduchu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.