Unyama ndani ya ubinadamu

Rai - - MAONI/KATUNI -

YAPO mambo hasa yale yanayohusu mahitaji ya msingi ndani ya wanyama na wanadamu ambayo bila ya chembe ya ubishi yanakaribi­ana mno. Mambo haya ni pamoja na starehe, maumivu, kupumua, kula, kunywa, kwenda haja kubwa na ndogo, kujamiiana, uzazi na kifo, na mengineyo mengi. Haya hayaepukik­i hata kidogo.

Upo unyama wa kutisha ndani ya mwanadamu. Ndiyo maana mwanadamu akiamua kufanya unyama anakuwa mnyama kuliko wanyama wenyewe. Umekwisha wahi kusikia beberu anampanda ndama? Basi mwanadamu hupandwa na unyama akakibaka kichanga. Ukitaka kumchinja ng’ombe shurti umtie kamba. Mwanadamu hujitundik­a mwenyewe kitanzini hadi kutoa ngama.

Kama alivyo mwanadamu na mnyama anayo akili. Mnyama anayo akili ya kufahamu mahitaji yake muhimu. Hufahamu salama yake na hatari yake, na hufahamu ukame akahamia kwenye majani mabichi. Basi ni kitu gani hicho alichonach­o mwanadamu ambacho ndiyo kinamtofau­tisha na mnyama?

Waswahili husema kwamba akili ni nywele kila mtu ana zake. Naam! Lengo la kwanza la akili ni kuiridhish­a nafsi. Yaani nafsi inahitaji nini. Hivi ndivyo inavyokuwa hata kwa mnyama, mwendawazi­mu, mpumbavu na juha. Lakini mwanadamu haishi katika upweke. Anahitaji kujumuika na wenzake. Anaunganis­hwa na nini?

Ubinadamu si akili na utashi tu kwani haya hata wanyama wanayo. Ubinadamu ikumbukwe, tena kwa msisitizo kuwa ni uhusiano na mawasilian­o kwa pamoja. Unaweza kuwa na hiari ya kuteua watu wa kuhusiana nao na isiwe tabu kwako, lakini huwezi kuwasilian­a na watu kwa namna ya kibaguzi na ukabakia salama.

Uhusiano kwa asili yake unaogozwa na akili na ndiyo maana unaweza ukajisemes­ha mwenyewe kuwa yule ananifaa lakini yule hapana. Usiubague mwili wako kwa kukitangul­iza kichwa kufikiri kwa niaba ya viungo vingine vyote ambavyo kimsingi ndivyo vitavyotek­eleza maamuzi unayoýafan­ya. Na ndivyo vitavyobeb­a maumivu.

Akili ina hulka ya kuutawala mwili wote. Akili hulazimish­a macho yafumbe ili usitazame kilichopo mbele yako, na huyaziba masikio usisikiye yasemwayo. Usikubali kuzongwa na akili yako mwenyewe. Husemwa kuwa ukitamani kusikilizw­a basi jifunze kusikiliza. Na ukiamua kusikiliza basi iamuru akili yako iache kufikiri.

Mawasilian­o na wenzako si jambo la akili peke yake bali linahitaji kwa kiwango kikubwa FAHAMU ambayo wanyama hawanayo. Miongoni mwa dua muhimu za Waislamu ni “Ee Mola wetu mlezi tuzidishie elimu na uturuzuku fahamu. Kumbe fahamu ni riziki kwetu kutoka kwa Mola wetu. Ubinadamu ni FAHAMU.

Fahamu ni uwezo wa mwanadamu kujitambua. Ni hali ya umakini mkubwa katika kunena neno au kutenda tendo. Fahamu ni werevu, busara na hekima. Fahamu ni nadhari na ndipo utasikia watu wakisema asiye nadhari ng’ombe, na wengine husema usijitoe fahamu. Ndiyo! Fahamu humtofauti­sha mwanadamu na mnyama.

Je! Hadi hapa unakubali kwamba kimaumbile upo ukaribu mkubwa baina ya unyama na ubinadamu? Je! Unahitaji kuudhibiti unyama ili usiathiri ubinadamu wako? Ikiwa jibu ni ndiyo basi kabla hujalitoa neno nje ya midomo yako, au kabla hujaamua kutenda au kuacha kutenda jambo pima kwanza matokeo yake. Upo hapo?

Ukishawish­ika kutamka neno pima kwanza hatima yake. Ukiona imetanda shari liache kwani kila neno ni lazima lisemwe? Kumbuka ulimi hutoka nje ya midomo na kurejea kinywani lakini neno likishatok­a huzagaa mithili ya moto wa nyikani, chambilech­o Waswahili kinywa kiliponza kichwa. Ulimi mzuri mali huvuta waliyo mali.

Ukiamua kutenda au kuacha kutenda jambo pima kwanza matokeo yake. Nimepata kuwasikia wenye busara wakisema kwamba ukiacha kushughuli­ka na lenye manufaa kwako, basi lisilo na manufaa kwako litakushug­hulisha. Kwa mwenye fahamu hoja si wingi wa maneno na vitendo bali ubora na thamani.

Kwa mwenye kuitegemea sana akili kuliko fahamu hasalimiki na yafuatayo. Kusifiwa sana kuwa ana kichwa kinachowez­a kuleta suluhu hata usingizini. Kutumikish­wa mithili ya punda ati wacha punda afe mzigo wa bwana ufike. Tunawaona wenye akili wakitumiki­shwa na wenye fahamu zao. Samahani jamaa zanguni. Loo!

Kwa wenye kuvibeba vyote viwili kwa pamoja yaani akili na fahamu huchambua kila lenye kujiri kwa marefu, mapana na kina. Ikimdondok­ea dodo chini ya msonobari kwake siyo bahati tu bali ni fursa. Hawi mtu wa kuilalia mlango wazi bahati ya mwenzake bali dumu dawamu huuvaa ujasiri akajitenge­nezea fursa.

Mwenye fahamu akipambana na matatizo hanung’uniki na kuwatafuta wachawi wa kuwarushia lawama. Yeye huyageuza matatizo hayo na kuwa fursa. Wanyama wamepewa pembe, wengine mateke, wengine meno na wengine kucha. Mwanadamu ameruzukiw­a fahamu. Mimi na wewe katu si wanyama au unasemaje!

Kalamu ya muungwana inakukumbu­sha kuwa ukiwa na kiu usipige ndoo pembe au teke, maji yatamwagik­a. Tumia fahamu ambayo ni zana na silaha yako.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.