Viwanja vya michezo shuleni vinatumiwa vibaya

Rai - - HABARI - NA HASSAN DAUDI

SAFU ya Macho Yameona ianze kwa kuwatakia kila la heri wanafunzi wa Kidato cha Nne wanaoendelea na mitihani yao ya kuhitimu ngazi hiyo ya elimu.

Hakika Mungu atawaongoza huko muendako na hatimaye kuungana na wasomi wengine katika taaluma za uhandisi, udaktari, ualimu, uandishi wa habari na nyinginezo zilizo kwenye ndoto zenu.

Pia, haitakuwa busara kuwasahau waalimu na wazazi wao. Pongezi ziwafikie kwa jitihada na uvumilivu wenu mkubwa kwa kipindi chote cha safari ndefu ya miaka minne.

Baada ya hayo, leo macho yameona mazoea yaliyojengeka kwenye viwanja vya michezo katika shule za msingi, ambavyo si tu wanafunzi wamekuwa wakivitumia, bali jamii kwa ujumla.

Kuliweka sawa hilo, nitatolea mfano Uwanja wa Shule ya Msingi Mwanyamala ‘B’ iliyoko Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, ambako ndiko ninakoishi.

Aidha, mfano huo unaweza pia kuigusa Shule ya Sekondari ya Makumbusho, ambayo pia mbali ya uwanja wake wa michezo kutumiwa na wanafuzi, pia umekuwa ukiwafaidisha wakazi wa eneo hilo.

Nimekuwa muhudhuriaji mzuri wa viwanja hivyo, si kwa kufanya mazoezi pekee, pia kuzitazama timu za soka, ndondi, riadha na michezo mingine zinavyojifua asubuhi na jioni.

Nikiwa sipingani na wazo la uwepo wa viwanja vya michezo shuleni, natilia shaka utaratibu uliopo, nikiamini hauna afya kwa taaluma.

Ndiyo, kutokana na ukaribu wa viwanja hivyo na madarasa, sidhani kama utaratibu wa wakazi wa eneo hilo kuruhusiwa kufanya mazoezi wakati wanafunzi wakiwa darasani hauathiri utendaji kazi wa walimu.

Pia, wasiwasi wangu ni kwamba huenda umakini wa wanafunzi katika kupokea wanachopatiwa wakati wa somo husika hukutana na changamoto kubwa kutokana na kelele za wanaoendelea na mazoezi.

Lakini tusisahau pia kwamba wakati mwalimu akiwa ‘bize’ ubaoni, kuna uwezekano wa kupoteza asilimia kubwa ya wanaomsikiliza kwa kuwa sehemu ya wanafunzi watakuwa wameelekeza umakini wao katika kile kinachofanyika uwanjani.

Kwa upande mwingine, likiwa ni jambo la fedheha zaidi kwa waalimu mbele ya wanafunzi wao, lugha za matusi zimekuwa sehemu ya mazungumzo ya kawaida katika viwanja hivyo.

Kwamba sasa, mwanafunzi wa shule ya msingi si tu anajifunza kutoka kwa mwalimu wake wa Hisabati, Kiingereza na Sayansi, pia anaweza kuwa ‘tajiri’ wa maneno machafu kwa kadri anavyotumia muda mwingi akiwa shuleni.

Aidha, lipo suala la utumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya aina ya bangi katika maeneo hayo ya viwanja vya michezo vya shule vinavyotumiwa na wakazi wa eneo husika.

Ukiweka kando ukweli kwamba hiyo inawaweka hatarini wanafunzi kwa kuwa wanaweza kuanza kutumia mihadarati hiyo, pia wanaweza kushawishika kuuza.

Nikizizungumzia shule za msingi, wanafunzi wengi ni wenye umri mdogo, ambao kisaikolojia, hujifunza kwa kuiga, hakuna ubishi kuwa wanaweza kuvutwa na fedha nyingi wanazoona zikipatikana katika biashara hiyo haramu.

Vilevile, kama nilivyokiri hapo awali, kwamba nimekuwa nikihudhuria katika viwanja hivyo, niseme tu kwamba wanafunzi wa kike, nikiwazungumzia wa elimu ya sekondari, wamekuwa wakiteseka zaidi.

Ndiyo, ni kawaida kuitwa na kutongozwa kila wanapokatiza katika viwanja hivyo wakiwa wametumwa na walimu wao na mbaya zaidi haishangazi kuona wakiambulia kauli chafu na za kejeli pale wanapokataa.

Macho Yameona haioni sababu ya tabia hiyo kuendelea kuwa kirusi katika mfumo wa elimu, kwamba juhudi za makusudi zinatakiwa kuchukuliwa kwa kuzuia viwanja hivyo kutumika wakati wa masomo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.