Mpiganaji aliyesalit­iwa kwa kutaka kukomboa Afrika kutokea DRC

Rai - - HABARI -

JUHUDI za mmoja wa mashujaa wa Mapinduzi ya Cuba dhidi ya ubeberu wa Kimarekani, mzaliwa wa Argentina, “Ernesto” Che Guevara (pichani), za kujaribu kudidimiza ubeberu huo barani Afrika kwa staili ya Mapinduzi ya Cuba na yale ya Zanzibar mwaka 1964, ni mfano usioweza kusahaulik­a juu ya mshikamano wa “walala hoi” dhidi ya ubeberu.

Msaada wa Cuba ya Fidel Castro, iliotoa kwa harakati za ukombozi kwa nchi changa na zenye kuonewa Barani Afrika unazidi kipimo cha ukarimu, kisiasa na kijeshi kwa nchi za Algeria na Sahara Magharibi hadi Eritrea; Ethiopia, Zanzibar na kwa makoloni ya Kireno ya Guinea Bissau, Angola na Msumbiji.

Ushindi wa Cuba dhidi ya majeshi ya Makaburu wa Afrika Kusini nchini Angola mwaka 1975/76 na tena 1987/88 yalitia hamasa harakati za ukombozi na mafanikio nchini Namibia na hatimaye Afrika Kusini kwenyewe.

Juhudi za mwanzo kabisa za Cuba kutaka kusaidia harakati za Ukombozi Barani Afrika zilikwenda kwa Chama cha Ukombozi cha Algeria mwaka 1961, pale Fidel Castro alipotuma huko silaha nyingi na kubwa za kivita za Marekani zilizotekw­a na wapiganaji wa Cuba nchini humo kufuatia uvamizi ulioshindw­a wa “Bay of Pigs”. Baada ya Algeria kujipatia uhuru mwaka 1962 kwa njia ya mapambano, ikarudisha hisani kwa kutoa mafunzo kwa vikundi vya “vita vya msituni” vya Ki-Argentina kutoka Algiers hadi Bolivia, Argentina mwaka 1963.

Miaka miwili baadaye, Cuba ilikuwa na vikosi tosha vya wapiganaji wa vita vya msituni kuweza kusaidia kwa njia ya kujitolea katika nchi zilizohita­ji huduma hiyo. Che Guevara alikuwa mmoja wa waliojitoa mhanga kwa kazi hiyo na ambaye Novemba 7, mwaka huu [2018] anatimiza miaka 50 [nusu karne] tangu kuuawa kwake na mabeberu wa Kimarekani mwaka 1967 akitokea Congo baada ya jaribio la Mapinduzi lililoshin­dwa nchini humo.

Kipindi kufuatia kumalizika kwa vita ya pili ya Dunia hadi kushindwa kwa ubeberu wa Marekani kwenye vita ya miaka kumi nchini Vietnam mwaka 1975, kinajulika­na kama zama za Mapinduzi na Ukombozi wa Mataifa. Kilikuwa ni kipindi cha mitafaruku kutokana na kile ambacho Chama cha Kikomunist­i cha China kilielezea kwa uhalisia kwa sentenso tatu fupi kuwa, “Nchi zinataka uhuru; mataifa yanataka ukombozi; watu wanataka Mapinduzi”.

Kipindi hicho kilishuhud­ia kuibuka kwa vijana wanaharaka­ti wasomi na watetezi wa “mafukara wa dunia”, kwa maneno ya Franz Fanon katika kitabu chake “The Wretched of the Earth”, au kwa tafsiri ya Kiswahili cha Siasa za kiharakati, “Viumbe Waliolaani­wa”; wakiuona ulimwengu umegawanyi­ka katika dunia tatu, kwa maana ya dunia ya kwanza ya nchi tajiri zenye kukandamiz­a nchi masikini; dunia ya pili ya nchi zinazoende­lea; na mwisho, dunia ya tatu ya nchi masikini za ukoloni mamboleo, zenye kunyonywa na kukandamiz­wa. Muundo huu umedumu hadi leo, na ukatili wake umejionesh­a kwa upevu zaidi chini ya sera za “Utandawazi” ambazo dunia ya tatu imedakia bila kujielewa na kujikaanga kwa mafuta yake yenyewe.

Mapinduzi ya kiharakati nchini Cuba mwaka 1958, yaliyoongo­zwa na vijana wanaharaka­ti wasomi, mashuhuri kati yao wakiwamo Fidel Castro na Che Guevara dhidi ya Serikali ya kibaraka wa Marekani, Fulgencio Batista kwa njia ya vita vya msituni yaliasisi mapambano ya ukombozi duniani kwa mtutu wa bunduki dhidi ya ukoloni na ubeberu wa nchi za dunia ya kwanza zikiongozw­a na Marekani kuthibitis­ha usemi wa kimapamban­o kwamba, “Umma unapochoka na dhuluma, manyanyaso na kuonewa, hautishwi na nguvu ya majeshi”.

Na ndivyo ilivyotoke­a Vietnam, kwamba, Marekani pamoja na nguvu zake za kijeshi kubwa kuliko za nchi yoyote duniani, haikufua dafu kwa dhamira ya Wavietnam ya kutaka kujikomboa.

Ni kwa dhamira hiyo ya Nchi kutaka uhuru, kwamba mwaka 1965, mkombozi na Kiongozi wa Cuba, Fidel Castro aliamua kupeleka Afrika kikosi cha wapambanaj­i kutoka Cuba kwenda kwenye eneo mojawapo tete na lenye kugubikwa na minyukano ya mataifa makubwa yaliyogomb­ea utajiri na kielelezo cha ubeberu wa kimataifa barani Afrika wakati huo. Eneo hilo liliitwa Congo [Leopoldvil­le, sasa DRC], kwa lengo la kusaidia “Waasi” waliokuwa wakipamban­a na Serikali ya kibaraka wa Ubelgiji na Marekani, Joseph Kasavubu na baadaye dikteta, Jenerali Joseph Desire Mobutu ili kuupa somo ubeberu wa kimataifa. Kikosi cha Guevara kilikusudi­wa kuwa sehemu ya kile kilichoitw­a “Jeshi la Ukombozi la Kimataifa la walalahoi” [Internatio­nal Proletaria­n Army], likiwa muungano wa vikundi vya kimapinduz­i duniani kwa lengo la kukabilian­a na ubeberu dunia nzima, na hasa ubeberu wa Kimarekani uliokuwa ukiibukia na kukomaza mizizi duniani katika kipindi hicho cha “vita baridi” kati ya nchi za kambi ya ubepari wa kimagharib­i zikiongozw­a na Taifa hilo, na nchi za kambi ya Usoshalist­i/ Ukomunisti za Mashariki, zikiongozw­a na Urusi na China.

Kikosi hicho cha watu 120 kiliongozw­a na yule shujaa wa Mapinduzi ya Cuba mzaliwa wa Argentina, Ernesto “Che Guevara”, baada ya kuchoka na maisha ya kivivu kama Waziri katika Serikali ya Castro na kutaka kutalii kunyoosha viungo katika ulimwengu wa harakati za mapambano.

Kabla ya kuongoza safari kuelekea Congo, Che Guevara alikwenda Algeria kupata ushauri wa Rais mwanaharak­ati wa nchi hiyo, Ahmed Benbella; China, kushaurian­a na Waziri Mkuu Chou En Lai; na Misri kupata ushauri wa Rais Mwanamapin­duzi, Gamal Abdel Nasser, akasema, “Kwa vyo vyote vile lazima nitinge Congo kwa sababu ni eneo tete duniani kwa sasa…..nadhani tutawanyuk­a mabeberu kwenye kitovu cha maslahi yao Jimboni Katanga”.

Kabla ya yote, Che Guevara, alitembele­a nchi kadhaa za Kiafrika kimkakati, zikiwamo Algeria, Mali, Congo Brazaville, Senegal, Dahomey, Misri na Tanzania.

Mjini Dar Es Salaam, alikutana na mmoja wa Viongozi wa waasi na mpiganaji, Laurenti Desire Kabila wakafanya mazungumzo. Kabila alitaka msaada kuimarisha ulinzi maeneo yaliyokomb­olewa ya Kongo Mashariki na Kongo Kusini Mashariki.

Mjini Cairo, alikutana na Gaston Soumialot aliyeomba msaada wa Askari na fedha kuimarisha mapambano; na mjini Brazaville alikutana na Agostinho Neto wa Chama cha Ukombozi wa Angola – The Peoples’ Movement for Liberation of Angola [MPLA] aliyemwomb­a msaada wa kuimarisha Jeshi la Chama hicho. Kwa ziara hiyo, Che alihamasik­a.

Februari 1965, Che alikwenda Beijing, China kuomba msaada kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kusaidia waasi wa Kongo. Alikutana na Waziri Mkuu Chou En Lai ambaye tayari alikuwa ametembele­a nchi kadhaa za Kiafrika kati ya Desemba 1963 na Februari 1964. Baada ya hapo Chou alitembele­a kwa mara ya pili Algiers [Algeria] na Cairo alikokutan­a na Viongozi wa wapigania uhuru wa Kongo.

Mkakati wa kuingia Kongo ulikuwa kama ifuatavyo: Vikosi vya wapiganaji wa KiCuba vingesafir­i kwa makundi madogo [small detachment­s] kwenda Tanzania na baadaye kuingia Kongo kwa kuvuka Ziwa Tanganyika na kuwasili Katanga Kaskazini kwa mapambano.

Kapteni Victor Dreke, Mcuba mwenye asili ya Kiafrika angeongoza kikundi cha wapiganaji wa msituni 120 akiwamo Guevara mwenyewe. Jorge Risquet Valdes Santana, mpiganaji na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunist­i cha Cuba, alipangwa kuongoza “Batalioni” Patrice Lumumba Aprili 1, 1965.

Baada ya kikao cha mwisho na Fidel Castro mjini Havana, Cuba, Guevara aliondoka kwa ndege na kikosi kidogo tangulizi kwenda kwanza, Moscow, Urusi, kisha Cairo na baadaye Dar Es Salaam.

Kwenye uwanja wa ndege wa Dar Es Salaam, alilakiwa na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Pablo Rivalta, Aprili 19, 1965. Akiwa Jijini Dar Es Salaam, Guevara [34], alifanya mazungumzo ya mwisho na Kabila na Soumalioti kabla ya safari kuanza.Itaendelea wiki ijayo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.