Wakati na nafasi ni vya kujihadhari navyo

Rai - - MAONI/KATUNI -

Dalili zote zinaonyesha kuwa unavipitia vifo vingi bandia kabla ya kifo chako halisi hakijakufikia. Kwa nini unatamani kufa katika wakati unaotakiwa kuishi? Unakata tamaa katika jambo lipi hasa. Unajitia machungu na woga kwa minajili gani. Ukiitaka nusura huna budi kujitambua iwapo unachoogopa ni kuishi au unayaogopa maisha?

Umeamka ukiwa na afya mwilini na akili timamu? Unayatambua mahitaji yako ya msingi ya leo na unazo nguvu za kutosha za kwenda kuhemea mahitaji hayo? Unao uwezo wa kula na kunywa bila ya msaada wa daktari? Huko ni kuishi na ni sehemu ya uhai. Kutambua unachokihitaji na si lazima unachokitaka na kukitamani, kukichuma na kukitumia ndiyo kuishi. Umekatishwa tamaa na mambo haya?

Wapo wenzetu wanalishwa chakula kwa kutiwa mipira puani. Wapo wenzetu hushikwa mkono wanapotembea kwa kuwa macho yao hayaoni. Wapo wenzetu hadi waguswe bega ndipo wageuke kwa kuwa ni viziwi. Na wapo wenzetu wanatambaa kwa kuwa ni walemavu wa viungo. Wewe unakata tamaa ya kuishi kwa sababu unatembea kwa miguu yako, unaona kwa macho yako na kusikia kwa masikio yako? Afanaleki!

Nikikutazama vizuri nakuona kuwa unapenda kuishi. Siyo kweli kuwa unatamani ufilie mbali ili ati ukapumzike na adha za kuishi. Kwa hakika kuishi hakuna adha za kiasi hicho. Inawezekana wewe unasumbuliwa na maisha na wala siyo kuishi. Pengine unatamani kuishi kwa wakati usiyokuwa wako na kwa nafasi isiyokuwa yako.

Kwetu sisi wanadamu kuishi ni kujitambua. Ulikuwa unabebwa ulipokaribishwa duniani ukiwa kichanga. Ukibahatika utabebwa tena siku ya kuagwa duniani ndani ya jeneza. Leo upo hai unaishi hayupo wa kukubeba. Amka na upambane ili uishi utakuwa na amani. Maisha ni bahari ya sote.

Ukitaka uwe na amani ya moyo ni lazima kwanza utanabahi kuwa kilicho haki yako kwa Mola wako ni kuishi. Lakini utaishi maisha ya namna gani si suala la haki bali hiari na mukhtari. Ila na utambue kuwa si kila maisha unayoyataka na kuyatamani utayapata ili moyo uburudi. Maisha yamesheheni mizungu.

Maisha ni mtazamo na fikra zako katika kuiogelea dunia. Hawakukosea waliyosema kuwa dunia ni bahari kubwa iliyokusanya raha na karaha. Humo mna vitoweo ambavyo ukivila hupata lishe kemkem. Na humo vimo vitoweo vinavyoweza kuwa jeneza lako na kaburi lako. Hayo ndiyo maisha.

Kuishi kwetu kunapatikana ndani ya uhai wetu. Tunaishi tangu tukiwa viganjani mwa mama zetu hadi tunapoingia matumboni mwa ardhi. Na maisha yetu yamo ndani ya mawazo yetu tukatamani turuke ilihali hatuna mbawa, tukatamani tusikike panapohanikiza zogo, na tukatamani nafasi hata pasipoenea wayo. Maisha ni kulewa bila ya pombe.

Unakutana na vijana wawili ambao wameajiriwa pamoja, siku moja, ujira mmoja na wanaishi eneo moja. Mmoja anasema maisha ni mazuri na mwengine anasema maisha ni magumu kupitia maelezo. Ni dhahir isiyo shaka kuwa tatizo hapa siyo maisha bali ni mtazamo kuhusu maisha. Mawazo ya mtu yanataka nini ndani ya maisha.

Nirejee kwako ndugu yangu. Tatizo lako halina uhusiano na kuishi kwako. Tatizo lako limo ndani ya aina ya maisha. Mtazamo wako na mawazo yako kuhusu maisha vinakuhamisha kutoka katika uhalisia wa maisha yako ya leo na kukurejesha katika maisha yaliyopita yakaenda zake. Wakati hausimami.

Wewe ndugu yangu ni yule yule na haya maisha ni yale yale. Yaamrishe mawazo yako yaende na wakati. Maisha ya kuendekeza vitu na watu ni maigizo yasiyo na tija kwako. Kwani wapo wapi waliyokuwa wanakuzunguka na kukumwagia sifa. Hawajafa bali wamekukimbia. Achana na yaliyopita, ishi Ieo, sasa.

Unaungulika moyo kwa sababu ya nafasi! Wewe ni mtu na nafasi si chochote. Ndani ya kuta nne, sakafu na dari ni nafasi au uwazi ambào si lolote si chochote hadi ijazwe. Pakiwekwa kitanda ni chumba, pakiwekwa samani ni ukumbi, pakiwekwa matundu ni chooni. Wewe ndiye mwenye thamani na siyo nafasi zinazokaribia kukutoa roho.

Zinduka ndugu yangu urejeshe thamani ya utu wako. Nafasi ambazo ulikuwa nazo si shani. Iwapo ulikuwa mume bora au mke mwema ni nafasi tu, hata leo unaweza kuwa hivyo maadamu ndoa bado ruksa. Ikiwa ulikuwa na madaraka au mafanikio ya biashara hizo nazo ni nafasi tu. Nafasi haina thamani kama huitumii. Itumie nafasi uliyonayo sasa.

Urais hauongozi nchi iwapo hayupo Rais. Udereva hauendeshi gari iwapo hayupo Dereva. Kwa maneno mengine, urais na udereva ni nafasi tu ambazo thamani yao ni mimi na wewe. Nafasi huleta faida inapomilikiwa na mwanadamu. Ndugu yangu imiliki nafasi uliyonayo sasa na utaishi kwa amani.

Utumie vizuri wakati uliyonao sasa na hakika hutajuta. Kuutumia vizuri wakati uliyonao sasa utakuwezesha kuyasahau yaliyopita na kuwasamehe waliyokukwaza, na bila ya shaka utajitambua na kujenga msingi imara wa kesho yako. Chini ya jua la Mwenyezi Mungu hakuna KESHO bila kwanza kuwepo LEO. Itumie LEO vizuri kabla haijageuka kuwa jana.

Kalamu ya muungwana inakupenda na kukuhurumia sana ndugu yangu. Nafahamu mwangaza wa ghafla gizani husumbua macho lakini nivumilie. Nia yangu ni kukuangazia njia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.