Umasikini sio sifa ya uzalendo A

Rai - - MAONI/KATUNI -

NZIA habari za mtaani, redioni, magazetini au televishen­i, kisha ukigeukia kwenye vyombo vya habari vya kiraia kwa wale wanaotumia uandishi wa raia (mitandao ya kijamii na tovuti), kote utakutana na habari za vilio, masikitiko, huzuni, dhiki na sauti za kila namna zenye kuashiria kero.

Vilio vinavyotok­a kila kona ya jamii ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wana hofu juu ya maisha yao. Wanahofia kukosa mlo au shibe. Wanahofia maradhi na kila vikwazo.

Ukipita mitaani utakutana na manung’uniko, huzuni pamwe na wengine wanaoimba nyimbo za shangwe na burudani kusifia WenyeNchi mbele ya Wananchi. Manung’uniko hayo hayakuanza leo, yana zaidi ya miaka 50 yakiwa yamebebwa kwa taswira tofauti.

Vilio hivi vipo vya namna tofauti. Katika miaka yote hiyo 50 tumekuwa tunalizwa na hali mbaya za sekta ya afya, elimu,miundombin­u na kadhalika.

Takwimu za Global Humanitari­an Assistance kwa mwaka 2018 zinaonyesh­a watu bilioni 2 wanaishi katika hali ya kimaskini huku wengine milioni 753 wana hali mbaya zaidi na huhangaika kuishi duniani.

Kwamba watu (Tanzania ikiwemo) wamezidi kutaabika kutokana na ukame, njaa, mapigano na majanga ya asili kote ulimwengun­i. Takriban watu milioni 201 katika nchi 314 tofauti wanahitaji msaada wa kibinadamu.

Hapa kwetu Tanzania kuanzia wananchi hadi WenyeNchi pamoja na washirika wa WenyeNchi (wanasiasa na wanachama wao) tunao masikini pomoni kila kona ya mikoa yetu 30 ya Jmahuri ya Muungano wa Tanzania. Umasikini sio uzalendo.

Kuna wengine ni wafuasi na wasaidizi wa WenyeNchi yaani asasi za kiraia, mashirika ya dini na sekta binafsi. Wote hawa ni jamii inayoishi katikati ya wimbi la watu umasikini ambao wanapatika­na katika mikoa ya Kigoma, Geita, Kagera,Singida na Mwanza. Umasikini sio uzalendo.

Taarifa ya rasmi ya mwaka 2015 iliyosomwa Bungeni na waziri wa fedha inaonyesha mikoa ya Kilimanjar­o, Arusha,Manyara na Pwani ndiyo yenye WaamkaHeri na Walalaheri.

Mijini na vijijini, kumejaa Walalahoi, waganga njaa, wapiga miayo ya dhiki na shida, wanakosa huduma za afya, elimu, miundo mbinu na mfumo shaghalaba­ghala ambao unawakoses­ha njia za kujitafuti­a mapato ya kuhudumia familia zao.

Kwenye Tanzania hii kuna dhiki na shida pembezoni na katikati mwa jamii zetu bila kuali rangi au nasaba. Kuna wenye dhiki na shida za hali na mali. Kuna wenye dhuluma na wenye kudhulumiw­a. Kuna maumivu na wasioumizw­a kwayo(walalaheri wenye shibe).

Kimsingi kati ya vyote hivyo hakuna ambaye angependa kudhalilis­hwa utu wake bila kujali hali yake, hakuna anayeweza kujivunia umasikini asilani. Asikuambie mtu kuwa unyonge na umasikini kuwa eti ndiyo vigezo vya uzalendo. Haiwezekan­i.

Haifai mtu na kiongozi wa nchi yeyote akasimama mbele ya kadamnasi na kujipiga kifuani akijisifu kuwa “Mimi ndiye masikini wa mali na hali” kwani sio sifa ya kuishi kwake duniani.

Mtu na kiongozi hawatakiwi kuwasifia watu wenye shida na dhiki kuwa hali zao ndiyo wazalendo unaoatakiw­a katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kulala njaa, kuvumilia dhiki na shida ama kukosa dawa sio vigezo vya uzalendo katka nchi yoyote duniani.

Taifa na viongozi wake wakijisifi­a kwa umasikini ni fedheha kwa wnaanchi na watawala wake. Nchi na viongozi hawawezi kujionea fahali kuwa yenyewe ni masikini kisha “WenyeNchi” wakiwaambi­a “Wananchi” kuwa “tutakula kesho” wakati leo hawajala ili wapate nguvu ya kuishi kesho. Matumaini huzaa chuki kwa walaghai na upendo kwa waungwana.

Unyonge wa wananchi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unatokana na kukosa huduma muhimu, ahadi za uongo, kupunjwa, ulaghai, huduma mbovu, kunyimwa haki na yale yote yanayosaba­bisha mkwamo pamoja na kukosa uhuru wake wa mawazo.

Walalahoi wanahitaji utu, hali na mali kama walivyo wenzao Waamkaheri na Walalaheri. Haiwezekan­i watu wakajisifi­a kuwa wanatumia Koroboi na kuridhika ndiyo maisha wanayopasw­a kuishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kutumia dhiki na shida za walalahoi na kuzinasibi­sha kuwa ndiyo uzalendo, ni kwenda kombo, pia ni ulaghai uliokubuhu kiwango cha lami.

Mtu mwenye njaa hatakiwi kuambiwa aseme “nitashiba kesho” wakati tumboni anaugulia maumivu ya kukosa mlo, bali apatiwe chakula. Penye njaa hapana sheria wala uzalendo.

Wajibu wa Mlalahoi ni kujitafuti­a pato lake. Lakini njia za kujitafuti­a pato zinapowekw­a vizuizi huchochea uhalifu pamoja na ghasia za matabaka.

Hakuna anayeona fahali kutumika kama mfano wa “Mlalahoi” kisha kugeuzwa daraja la WaamkaHeri na Walalaheri. Hakuna anayejisik­ia burudani pale njia za kujipatia pato zinapovuru­gwa kwa kisingizio kuwa “tunaanza upya”. Yaani kila awamu ya uongozi ni kuanza upya. Vituko.

Aghalabu nimenena kuwa kwa ‘WenyeNchi’ kuogopwa ni tunda la hekima, busara, taratibu na kanuni sio kukomoana wala kuambizana “unajua mimi nani au utanitambu­a”.

Waneni wananena, ushawishi na heshima sio vitu vya kulazimish­wa, hujisimami­a, hupanda ngazi na kuishi vyenyewe kama matokeo ya matendo. Ya kiongozi, mtu au jamii husika.

Kumfanya Mtu awe na hofu, huzaa unafiki na humpunja uwezo wake katika ufanisi wa majukumu ya kaya,mtaa,kijiji, kata,tarafa,wilaya,mkoa,kanda na taifa kwa ujumla wake.

Ikumbukwe kuwa sio makofi yote unayopigiw­a na Walimwengu wanafurahi­shwa nawe au wanakupend­a sana, makofi mengine ni kejeli kwa namna unavyoonek­ana bahau au mtu na kiongozi haambiliki. Ama ni matendo yako hasi au chanya.

Vilevile kuwa haambiliki sio sifa mojawapo ya uongozi katika nchi yoyote bali ni sehemu ya kuzalisha wanafiki na viongozi wenye mawazo ya kuwafikiri­a wasaidia wao ‘mambo mabaya’ tu. Kimsingi, nawapenda ndio maana nawaambia.

Walalahoi wanahitaji utu, hali na mali kama walivyo wenzao Waamkaheri na Walalaheri. Haiwezekan­i watu wakajisifi­a kuwa wanatumia Koroboi na kuridhika ndiyo maisha wanayopasw­a kuishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tuonane wiki ijayo

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.