AFRIKA INAHITAJI AINA GANI YA

Rai - - MBELE - NA ROCKY AMINI

KIONGOZI mwema ni yupi? Je ni yule anaewasikiliza wananchi wake na kuwajali? Ni yule anayewatangulia wananchi wake mbele na kuwaacha mita kadhaa nyuma yake? Ni yule anayekuwa katikati yao (wananchi wake) huku akiangaza pande zote ambako wananchi wake wanapatikana kwa kutumia jicho la tatu katika kuchunga vizuri na kuwaongoza wananchi wake vizuri?.

Kiongozi mwenye mustakabali mwema na taifa lake lazima awe na kicho ya uongozi juu ya kila afanyalo. Huyu atafanya kazi kubwa ya kuangalia huku na kule yote haya kuangaza usalama wa wananchi wake. Usalama unapokosekana ushirikiano na mshikamano wa ki-uongozi lazima huvunjika, hii hupelekea kukosekana kwa mshikamano wa pande mbili (tabaka tawala na tawaliwa) katika uongozi.

Mwangaza wa Afrikaa na ule wa uhuru katika Bara la Afrika ulianza kutokea baada ya viongozi wetu kutafuta dira au mwelekeo wa Afrika katika msitakabali wake. Hawa walipendelea kuwa katikati ya taifa lao na kusikiliza shida na matatizo mbalimbali ambayo yalikuwa yanawakumba wao pamoja na wananchi.

Uongozi sio kuongoza tu, bali kuongozwa. Lazima ukubali kuwa sehemu ya tabaka zote mbili yaani, tawala na tawaliwa, wewe ni jamii ya wananchi. Kiongozi siku zote lazima akubali mwelekeo wa wananchi wake na kutafuta dira ya ukombozi ambayo mwananchi mwenyewe anaona sehemu ambako kuwako kwake kunafaa.

Lazima kiongozi atoe mwafaka juu ya aina yoyote ya kimtazamo na mwonekano wa jamii yake. Leo hii viongozi mashujaa kama Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania, Kwameh Nkrumah wa Ghana, Patrice Lumumba wa Kongo na wengineo wasingetoa mchango wao wa mawazo, basi leo hii tusingekuwa na mijadala mbalimbali na tungo nyingi juu ya mawazo yatakayo Afrika iliyo moja na huru. Hawa ndio waanzilishi wa uzalendo katika mataifa mbali mbali barani Afrika.

Afrika leo hii ingekua na dira gani katika mambo ya uongozi endapo ingekosa viongozi wazalendo waliopigania kwa hali na mali swala la kuleta uhuru bara zima la Afrika? Ni wazi kuwa leo hii tusingekuwa na mijadala isemayo, “Tulinde maslahi ya Tanzania na watu wake”. Tusingekuwa na umoja nchi huru za ki-Afrika. Taswira ya kusema tulinde maslahi ya Taifa la Afrika kamwe yasingekuwepo kama jinsi sasa hivi dira ya kuwa na taifa la Afrika inavyo-ongelewa na wanafikara kote barani Afrika. Kwa vyovyote vile mawazo ya viongozi hawa shujaa yangekosekana basi taswira ya Mwafrika na Uongozi isingekuwako enzi na enzi.

Kila mwananchi anafaa kuwa kiongozi, lakini sio kila mwananchi anaweza kuwa kiongozi bora. Kuongoza ni kuwa na hamasa inayosukumwa na kweli ipatikanayo ndani ya kiongozi bora. Sehemu kubwa ya maisha ya mwanadamu yamejawa na msukumo aidha wa kuongoza ama wa kuongozwa.

Asiyekubali kuongozwa hawezi kuongoza vema. Shirikisho la wananchi huundwa mara nyingi na kiongozi yeyote awaye. Kama ilivyo ada katika kuongoza lazima awe na uwezo wa kukubali kuongozwa pia. Tunaposema kiongozi mzuri lazima yeye pia aweze kuongozwa inamaana kwamba swala la kuongoza au kungozwa ni jambo la kila mwananchi katika jamii. Mwananchi ndiye anayeunda shirikisho la jamii na taifa kubwa kwa ujumla.

Kwa vyovyote vile mwananchi ndiye anayeunda shirikisho la jamii na serikali yake kwa ujumla. Kama ni hivyo basi,ni dhahiri kuwa mwananchi yeyote yule aidha anayeongoza au anayeongozwa huunda shirikisho lake mwenyewe. Shirikisho hili la uongozi lazima liwe na mtazamo wa dira imulikayo kwa taifa zima. Katika mantiki ya kwamba, kila mwananchi aliye shirikisho la taifa na jamii kwa ujumla ana wajibu wa kuthamini na kulinda maslahi ya kuwako kwake, aidha katika sehemu ya kuongozwa ama kuongoza. Pengine anawajibikaje?

Mwananchi anayependa maendeleo ya jamii yake ni lazima ahoji na kukosoa pale ambako anaona uongozi wake haumtendei haki. Hii ni katika upande wa mtawaliwa. Huyu ndiye anayetakiwa kushika majukumu makubwa katika kuleta ukombozi ndani ya jamii yake hasa katika karne ya sasa ambayo viongozi waliowengi wamesahau wajibu wao wa kiutendaji kwa jamii zao.

Hivyo walio wengi (tabaka tawala) wanajikuta wakiishia kukandamiza sehemu hii ya wananchi. Kwa vyovyote vile lazima mwananchi afanye jukumu la kukosoa na kurekebisha uongozi wake wa juu. “Je tunaikosoa serikali?”, lazima tujiulize. Mwananchi yeyote asiyekemea na kurekebisha serikali yake pale inapokosea kwa vyovyote vile huyu hafai kuigwa katika ukombozi ambao walio wengi wanautegemea na kuutarajia katika jamii nzima na taifa kwa ujumla.

Kukosekana kwa ushirikiano baina ya wananchi na viongozi wao hupelekea jamii kwa ujumla kukosa mwelekeo na msitakabali wa maisha yote ya wananchi. Hii itatupelekea wapi? Kwa vyovyote vile lazima tuingie katika taifa linalojipinga lenyewe katika kuwako kwake, kwa jina linguine, contradictory nation.

Tumeisaidiaje jamii ya aina hii katika kuikomboa kutoka katika dimbwi la namna hii? Je katika muktadha huu hatuoni kama tutajigawa tayari sisi kwa sisi? Dira ya mwafrika katika neno hai lazima ipotee na dhana ya Afrika moja haiwezi kamwe kuendelea kuwako katika uhalisia wa vitendo, bali uhalisia wa maneno.

Hakuna ujinga ulio mzigo mkubwa kama wa namna hii wa kuendelea kuwa na ushabiki wa kiimani na itikadi zisizokuwa na manufaa yenye mawanda mapana kwa Taifa lolote hapa duniani na barani Afrika. Lazima tutafakari mambo haya ya kuwako kwa mwafrika na uongozi katika dira na neno hai. “Je, Tuko tayari kufuatilia umuhimu wa kuwako kwetu katika ufanisi wa kushirikiana kiuongozi na maamuzi ambayo yatatupelekea kupata viongozi bora na wenye uzalendo barani Afrika?” Kwa mawasiliano: 0752767997, 0687302487 Email: rockyamini94@gmail.com

Mwalimu Nyerere akiwa na Nelson Mandela wakati wa uhai wao.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.