Wauza ‘gongo’ wanapojitangazia jamhuri yao

Rai - - HABARI - NA HASSAN DAUDI

KWA miaka mingi, mapambano ya Serikali dhidi ya wafanyabiashara na watumiaji wa pombe haramu ya ‘gongo’ yamekuwapo, ingawa ukweli usiopingika ni kwamba hayana mafanikio ya kujivunia.

Ndiyo, kwa maeneo mengi, hasa yenye wakazi wa kipato cha chini, ni ngumu kusema Serikali imefanikiwa kuidhibiti biashara hiyo kwa kiwango cha kuridhisha.

Mbaya zaidi, tofauti na hapo zamani, biashara hiyo hivi sasa imekuwa ikifanyika bila kificho, nikimaanisha kuwa ‘gongo’ imeendelea kuuzwa na kutumiwa mitaani kana kwamba hakuna vita dhidi yake.

Licha ya kwamba yapo maeneo mengi yanayosifika kwa biashara hiyo, Macho Yameona yanaitaja bila woga Kwa Mama Zakaria, Kinondoni, Dar es Salaam.

Ieleweke kuwa ukiachana na athari za kiafya kwa watumiaji, kuna changamoto nyingi zinazowakumba wakazi wa maeneo yanayozungukwa na vilabu vya pombe hiyo, nikiwazungumzia wale wasiotumia.

Nianze na kero zitokanazo na kelele na lugha za matusi za walevi, tena wakifanya hivyo nyakati za usiku, ambapo watu wengine huwa wamelala baada ya uchovu wa shughuli za siku nzima.

Pia, kwa namna moja au nyingine, asilimia kubwa ya vijana walio maeneo ya karibu na vilabu hivyo wamekuwa wakiingia katika ulevi, sababu kubwa ikiwa ni urahisi wa upatikanaji wa pombe hiyo.

Hapo sitazungumzia athari kwa watoto wadogo kutokana na lugha za matusi ambazo huzisikia kila uchwao kutoka kwa walevi ila itoshe kusema kisaikolojia wanaandaliwa kuwa sehemu ya jamii hiyo iliyolowea katika ulevi.

Swali ni je, nini kinachokwamisha juhudi za mapambano dhidi ya pombe haramu hiyo? Binafsi sina shaka kuwa Serikali haijanyoosha mikono katika vita hiyo.

Hata hivyo, kama ninavyoamini kuwa haijashindwa kuitokomeza biashara hiyo, nachelea kusema jitihada za Serikali katika harakati za kukabiliana na pombe hiyo zimekuwa zikihujumiwa.

Kwanza, jamii yenyewe imekuwa ikishindwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Jeshi la Polisi kuwafichua wafanyabiashara wa gongo. Ni sawa na kusema Serikali imeaachiwa mzigo huo mzito.

Hakuna namna ya kuepuka ukweli kwamba chimbuko la biashara hiyo ni katika jamii tunamoishi, kwamba wafanyabiashara ni aidha ndugu, jamaa au marafiki zetu.

Ikiwa jamii itakuwa tayari kuikataa biashara hiyo, basi Jeshi la Polisi litakuwa likipata taarifa za kutosha juu ya maeneo yenye vilabu hivyo vya gongo na mwishowe wahusika kutiwa nguvuni.

Kinyume chake, kama ambavyo jamii imekuwa na kawaida ya kuwaficha waovu wengine kama wezi na wabakaji, iko hivyo pia katika hili la gongo, jambo linalochelewesha udhibiti wa biashara hiyo.

Kwa mantiki hiyo basi, Polisi wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kuibua wafanyabiashara hao na haishangazi hata kidogo kuona wakizidiwa nguvu.

Aidha, binafsi sina chembe ya hofu kusema wapo baadhi ya polisi wamekuwa wakishirikiana na wafanyabiashara haramu wa pombe hiyo, hivyo kuwa kigingi katika juhudi za Serikali kulimaliza tatizo hilo.

Katika kile ambacho huenda pia kimekuwa kikififisha ushiriki wa jamii katika vita hiyo, imekuwapo kawaida ya baadhi ya polisi kupewa hongo ili kuvifumbia macho vilabu vya gongo.

Kwamba ndani ya muda fulani, baadhi ya polisi hupewa ‘chochote kitu’ ili tu wasiwe kizingiti katika uendeshaji wa biashara hiyo.

Ni katika Jamhuri hii, chini ya uwepo wa Jeshi la Polisi, ndani ya enei maarufu la Mwananyamala kwa mama Zakaria, kama ilivyo katika maeneo mengine, wafanyabiashara wa gongo wanajitangazia jamhuri yao, wakionekana kuwa wajanja kuliko chombo hiki cha usalama na sheria za nchi.

Labda kwa kulijua hilo, wananchi wengi wamekuwa wakihofia kulisaidia Jeshi la Polisi kwa kujua kufanya hivyo hakutakuwa na msaada wowote.

Huenda ni moja kati ya sababu ya kesi nyingi za wafanyabiashara wa gongo kutofika mahakamani kama zilivyo za maovu mengine.

Itoshe kwa leo kukuandikia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.