Kipi kianze kati ya uhuru wa siasa na uchumi?

Rai - - HABARI -

MIONGO sita ya uhuru Afrika bado inatafuta njia sahihi ya maendeleo, haijapata. Uchumi wake unazidi kusambaratika; demokrasia inayoyoma, umasikini umetia fora. Ukweli, Afrika ya leo ni masikini kuliko zama kabla ya uhuru.

Kuna dhana katika siasa na maendeleo inayojulikana kama “Politics of Developmentalism”; yaani “Siasa za Umaendeleo”, kwa maana ya “Maendeleo kwa gharama yoyote, hata kama ni kwa kifo cha demokrasia, ikibidi. Siasa za namna hii zinaweka mbele agenda ya “Maendeleo” kwa njozi za matokeo badala ya mikakati na vitendea kazi vinavyopaswa kutumika ili kuyafikia. Waingereza wana neno wanalotumia “The end justifies the means”.

Hapa suala la mipango na utaalam halipewi nafasi ila “kauli mbiu” [slogans] kama “kilio cha vita”. Wanasiasa dhaifu na wasiojua kuongoza huficha udhaifu wao na kudumu madarakani kwa kauli turufu na ukali uliopitiliza katika kusukuma agenda ya “maendeleo”.

Tahadhari na ushauri wa kweli utolewao na wataalam lakini usiowafurahisha wanasiasa hao huchukuliwa kama “upinzani”, dharau au hujuma kwa mchakato wa “maendeleo”. Matusi na misamiati ya kuwadhalilisha hushushwa na kuangushwa kwao kwa “uchungu wa nchi” wa kujifanya “Msaliti”, “Mpinga maendeleo”, “anatumiwa” na hivyo si mwenzetu; ashughulikiwe.

Hofu hutanda miongoni mwa wanataaluma, wazalendo na wakereketwa wa kweli wa maendeleo ya nchi. Dira ya maendeleo ya kweli hupotea; tija husambaratika; demokrasia hufa; udikteta na siasa hukalia kiti cha mbele.

Tumejionea haya zama za mfumo wa Chama kimoja na uchumi uliopangwa bila kupangika. Sasa tunajionea sera za uchumi za “njia panda”, ama kwa mfumo wa siasa huru na uchumi huria kuongoza mchakato wa “maendeleo”, au “siasa hodhi na turufu” zenye kuua demokrasia [Politics of Developmentalism] kufanya kazi hiyo. Je, tuna la kutumainia?.

Kwa Tanzania, kama zilivyokuwa nchi nyingi za dunia ya tatu karne ya ishirini, mlango wa uhuru ulifunguka kwa kishindo, huku Watawala wapya hawajui njia gani ya maendeleo wafuate ili kuweza kuneemesha nchi zao. Viongozi hao walikabiliwa na uchaguzi wa moja kati ya dhana mbili za maendeleo: “Uhuru wa kisiasa” na “Uhuru wa kiuchumi”, kipi kianze kati ya viwili hivyo. Utata huu bado unaendelea kuzitesa nchi hizi hadi leo, huku uchumi, uhuru, amani na utulivu vikiendelea kuparanganyika.

Kama usemi wa wahenga kwamba, “huwezi ukatumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja” ni wa kweli, je inawezekana uhuru wa kisiasa na uhuru wa kiuchumi kwenda pamoja wakati mmoja kwa mafanikio? Kama sivyo, kipi kianze?

Maoni yetu ni kwamba vyote viwili ni muhimu kwa maendeleo lakini haviendi pamoja na kwa wakati mmoja. Ni sawa na uhusiano wa yai na kuku. Hivi, kati ya yai na kuku kipi kilianza?

Tunaambiwa tufuate na kuiga njia za nchi zilizoendelea; je ni kweli zilipita njia tunayopita hivi sasa? Ni ipi iliyo sahihi kwa maendeleo, kati ya injili ya kuimarisha kwanza uchumi wa ndani au Utandawazi?. Kwa hali ilivyo hapa kwetu, nini kitangulie kati ya hivyo viwili?. Je, ni sahihi kufanya tunavyofanya, kwa manufaa ya maendeleo?.

Ni ukweli usiopingika kwamba, wakati uhuru wa kiuchumi umepiga mbio kwa kasi maradufu, kama inavyojidhihirisha kwa ubinafsishaji na umilikishaji wa uchumi wa taifa kwa wageni badala ya kuwamilikisha wananchi [chunga ulimi wako, usiseme “uzawa”], uhuru wa kisiasa unachechemea ukiwa umefungwa minyororo kwa makusudi. Matokeo yake ni wananchi kuporwa kauli na nafasi ya kufikiri na kukosoa kwa mema, na meli kwenda mrama kwa nahodha kupotea dira kwa jeuri ya kutoguswa.

Kwa mfano, Katiba yetu ya mwaka 1977 iliyodumaa, mbali na mabadiliko kidogo yaliyoruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa, sehemu kubwa ya Katiba hiyo inabakia kama ilivyokuwa enzi za utawala wa Chama kimoja. Chaguzi zote si huru na za haki: rushwa na “takrima” kutamalaki kiasi kwamba fedha inanunua madaraka na madaraka yananunua utajiri. Chaguzi zinapotawaliwa na rushwa, uhuru wa kisiasa hufa na demokrasia hugeuka kejeli kwa umma. Katika mazingira hayo, sauti ya “Viongozi” ndiyo husikika pekee, wengine wote huwa “wavivu” wa kufikiri kwa kunyimwa nafasi.

Wakati uhuru wa kiuchumi unaruhusu mtu atambe apendavyo kadri “akili” yake inavyomruhusu, leo, kwa mfumo wetu wa siasa, mtu huyo huyo haruhusiwi kugombea nafasi ya uongozi ila kwa kupitia Chama cha siasa tu. Na kwa kuwa “vigogo” wanaopata madaraka kwa nguvu ya fedha na utajiri wanajuana kwa “mizengwe” kama Waarabu wa Pemba wajuanavyo kwa vilemba vyao, mtu wa kawaida hana nafasi wala uhuru wa kuwania madaraka na uongozi kwa kukosa “dau”.

Hii ndiyo sababu hoja ya “mgombea binafsi” inapigwa nyundo kila mara inapojaribu kuinua kichwa. Na hata kama maskini huyo atagombea kwa tiketi ya Chama na akapokonywa ushindi halali kwa nguvu ya fedha, hawezi kuitetea haki yake kwa sababu hatakuwa na shilingi milioni 5/= zinazotakiwa kufungulia kesi ya kupinga matokeo.

Sababu hizi zinatufanya tuamini kwamba uhuru wa kisiasa umepigwa ngwara kwa kutoa kipaumbele kwa uhuru wa kiuchumi kwa manufaa ya “walio nacho” dhidi ya “wasio nacho”. Hatudhani katika mazingira ya aina hii, tunaweza kupata maendeleo ya kweli kwa raia wote. Uhuru wa kisiasa unawawezesha watu kushiriki katika ngazi zote za jamii yao, na kwa kufanya hivyo jamii nzima hunufaika na mchango wao wa mawazo.

Utawala wa kidemokrasia hauwezi kuwa safi siku zote, hata iweje. Kwa hiyo, ni kwa njia ya kuishirikisha jamii na kwa pande kinzani katika jamii kufikia mwafaka kwa maendeleo ya nchi. Vijembe na kejeli kama vile “Wapeni vidonge vyao, wakitema, wakimeza ni shauri yao”, ni ukiritimba wa mawazo usiojenga; ni uhasama adui wa demokrasia unaokaribia “unyang’au”. Je, ni kweli kwamba uhuru wa kisiasa unachangia kukua kwa uchumi wa taifa?

Kuna kambi mbili kinzani zinazojitokeza kwa jibu la swali hili. Kambi ya kwanza ni ile inayodai kwamba uhuru wa kisiasa ni sharti moja kubwa katika maendeleo ya kiuchumi; kwamba taifa huru lenye watu huru kisiasa, lina nafasi nzuri ya kupanga na kuongoza uchumi wake bila ya kuingiliwa kwa manufaa ya watu wake, kuliko taifa linalotawaliwa na taifa lingine kisiasa. Kwa hili, ukweli wa usemi kwamba “siasa ni uchumi”, lakini “uchumi sio siasa” unajidhihirisha wazi.

Kambi hii inaunga mkono kauli mbiu ya Rais wa Kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah, kwamba “Utafuteni kwanza ufalme wa kisiasa, na mengine yote mtazidishiwa” [“Seek ye first the political kingdom and the rest shall be added unto you”].

Kambi ya pili inadai kwamba, uchumi wa nchi unaweza kupangika vizuri na kuendelea vema iwapo hautaingiliwa na siasa na wanasiasa. Inadai kwamba Serikali lazima ijiondoe kabisa katika kupanga na kuongoza uchumi kwa kuiacha nguvu ya soko itawale; na pia kwamba uhuru wa vikundi [umma] na Vyama vya Wafanyakazi usiruhusiwe kuhoji mwenendo wa uchumi, soko na uzalishaji; wala kusiwe na kuhoji manufaa ya mwenendo huo kwa umma. Kwa kambi hii, maendeleo ya “miradi” huchukua nafasi ya kwanza badala ya maendeleo ya “watu”. Mjadala huu bado ni hai na tata. Tunaambiwa tupite njia waliyopita wahenga wetu wa maendeleo ili tushikane nao mikono ndani ya “ufalme” wa utandawazi. Ni njia ipi iliyo sahihi kati ya hizi mbili?.

Utata huu unaweza kuondolewa tu kwa kuangalia historia ya baadhi ya nchi zilizopitia njia hiyo ya maendeleo, lakini hata hivyo maandishi ukutani yanaonyesha si ya kutarajia wala kutegemewa sana.

Kama usemi wa wahenga kwamba, “huwezi ukatumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja” ni wa kweli, je inawezekana uhuru wa kisiasa na uhuru wa kiuchumi kwenda pamoja wakati mmoja kwa mafanikio? Kama sivyo, kipi kianze?

ITAENDELEA WIKI IJAYO

Katibu wa Itikadi na Uenezi - CCM, Humphrey Polepole

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.