Salah ‘kuizika’ rekodi ya Okocha Mchezaji Bora Afrika 2018?

Rai - - MAKALA JAMNOIVIEMBA -

NI kinyang’anyiro cha kuiwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa mwaka huu, ambapo mshindi anatarajiwa kutangazwa Desemba 14.

Mastaa wanaotoana jasho safari hii ni Medhi Benatia (Morocco), Kalidou Koulibaly (Senegal), Sadio Mane (Senegal), Thomas Partey (Ghana), na Mohamed Salah (Misri).

Mchakato wa kuwapigia kura nyota hao ulianza Novemba 17 na utafikia tamati Disemba 2, na siku 12 baadaye wadhamini Shirika la Utangazi la Uingereza (BB) litamwanika aliyeibuka kidedea.

Ikumbuke kuwa mwaka jana ni Salah wa Liverpool ndiye aliyeshinda akiingia kwenye orodha ya mastaa JayJay Okocha, Michael Essien, Didier Drogba, Yaya Toure na Riyad Mahrez waliowahi kuibeba hapo awali.

Inatoka uk 24

Endapo atafanikiwa kuichukua tena, basi atakuwa mchezaji wa kwanza kuitetea tangu Jay-Jay Okocha wa Nigeria alipofanya hivyo mwaka 2002.

Salah (26), ameshahusika moja kwa moja katika upatikanaji wa mabao tisa msimu huu pale Liver, akifunga sita na kutoa ‘asisti’ tatu.

Ukiuzungumzia msimu uliopita, aliipeleka Liver fainali ya Ligi ya Mabingwa, akachukua tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA) na ile ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (FWA).

Kwa mujibu wa kiungo na nahodha wa zamani wa Liver, Steven Gerrard, ‘kwa sasa Salah ndiye mchezaji bora kwenye sayari hii’.

Je, nyota huyo ataweza kuitetea tuzo yake na kufuta utawala wa rekodi ya Okocha iliyodumu kwa miaka 16 sasa? Benatia (Juventus), Koulibaly (Napoli), Partey (Atletico Madrid), na mwenzake katika kikosi cha Liver, Mane watamwacha afanye hivyo?

Benatia (31), ambaye ndiye nahodha wa timu ya taifa ya Morocco, ni mmoja kati ya mabeki bora duniani kwa sasa na ni mchezaji muhimu kwenye safu ya ulinzi ya Juve.

Msimu uliopita, aliiongoza kulibeba kwa mara ya saba taji la Serie A, akaipa ubingwa wa Coppa Italia, na aliiongoza kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kama hiyo haitoshi, mwaka huu akawa sehemu ya kikosi cha Morocco kulichocheza Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998.

Staa mpya wa Juve, Cristiano Ronaldo anamzungumziaje Benatia? “Ni mchezaji bora kabisa,” anasema Mreno huyo.

Ukija kwa Koulibaly mwenye umri wa miaka 27, huwezi kuitaja safu ya ulinzi ya Napoli bila kumzungumzia Msenegal huyo.

Akiwa sehemu muhimu ya kikosi hicho, msimu uliopita Koulibaly aliisaidia Napoli kushika nafasi ya pili nyuma ya Juve waliotwaa ubingwa wa Serie A.

Nguvu na urefu wake si tu umekuwa ukiliwezesha lango la Napoli kuwa salama kwa mipira ya vichwa, pia ni tatizo kwa mabeki wa timu pinzani.

Hivi sasa ni mmoja kati ya mastaa wanaozungumziwa zaidi kwenye soko la usajili, ambapo Barcelona, Chelsea na Manchester United zimeonesha nia ya kuihitaji huduma yake.

Mane, mshambuliaji wa zamani wa Southampton, ameingia kwa miaka mitatu mfululizo. Alikuwepo wakati Yaya Toure akiibeba (2015), akazidiwa na Riyad Mahrez (2016), na kisha mwaka jana akabwagwa na Salah.

Kwa mwaka huu pekee, Mane (26) ameshazipasia nyavu mara 21, takwimu za mabao aliyoifungia Liver na timu yake ya taifa ya Senegal.

Ukiacha huyo, wafuatiliaji wa La Liga wanamfahamu vizuri Partey. Ndiye nguzo muhimu kwenye eneo la kiungo la Atletico.

Ni mara yake ya kwanza kuwania tuzo hii ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Afrika. Ameingia baada ya kuiongoza Atletico kumaliza katika nafasi ya pili msimu uliopita na akaipa taji la Ligi ya Europa.

HASSAN DAUDI NA MITANDAO Salah

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.