Wakuu wa mikoa, wilaya wazingatie sheria na taratibu

Rai - - MAONI / KATUNI -

TUNAUNGA mkono kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika, Ummy Mwalimu (Afya) na Selemani Jaffo (Tamisemi) ya kukemea tabia iliyoibuka kwa viongozi wa mikoa na wilaya ya kuwaweka watumishi wa umma ndani kwa sababu ambazo haziendani na Sheria ya Tawala za Mikoa.

Sheria hiyo pamoja na marekebish­o yake ya mwaka 2002, imegeuzwa kama fimbo ya kuwachapia watumishi bila kufuata utaratibu. Baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya wamekuwa wanatumia vibaya madaraka hayo kwa kuwakandam­iza watu.

Ipo mifano ambapo mkuu wa wilaya aliwahi kuwaweka rumande watumishi wa Idara ya Ardhi kwa sababu tu walichelew­a kufika kwenye mkutano wake. Mwingine alimweka ndani mtumishi wa Idara ya Afya bila kumpa hata nafasi ya kujieleza.

Mifano iko mingi, itoshe tu kwamba wateule wengi wa Serikali ya Awamu ya Tano, wanaonekan­a wazi kwamba wamelewa madaraka na wanataka waogopwe na wasipingan­e nao hata katika mambo yanayohusu taaluma zao. Baadhi ya viongozi wanawadhal­ilisha watumisi kwa kuwafokea na kuwakejeli watumishi hadharani, kitu ambacho ni kinyume kabisa cha kanuni na utaratibu.

Tunajua kwamba wengi wa wakuu hao ni wageni na ndiyo mara yao ya kwanza kushika madaraka hayo. Aidha tunaelewa mapungufu yanayotoka­na na mfumo usiozingat­ia taaluma za watumishi na kuwaweka watu katika nafasi ambazo hazihusian­i na taaluma zao.

Wakati umefika sasa kwa Serikali kufikiria upya kujenga kada ya watawala, badala ya kuteua watu ambao hawajui kabisa mambo ya utawala na wala wajasomea. Lakini wakati tukisubiri hayo kutokea, pawepo basi utaratibu wa kuwapa wateule hao semina elekezi ili kuondokana na kiburi kwamba wao wanaweza kufanya chochote bila kuulizwa na mtu yeyote.

Lakini jambo jingine ambalo pia linapaswa kukemewa ni wakuu wa polisi katika maeneo husika ambao wanapokea amri za wakuu wa wilaya na mikoa bila kuhoji. Kwa mfano, polisi wanamriwa kuwaweka rumande watumishi kwa sababu wameshindw­a kujieleza mbele ya wakuu hao, hivyo wanatekele­za amri kwa sababu tu imetoka kwa wakubwa.

Polisi wasikubali kuwalaza watu rumande ambao hawajafung­uliwa jalada lolote. Kama ikibidi wakuu wa wilaya na mikoa waandike amri ya kuwaweka watu ndani badala ya kutamka tu — ili endapo kunatokea tatizo, wasilaumiw­e kwamba wao (polisi) ndiyo wakosaji. Hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye amepewa madaraka na Katiba ya kumweka mtu kizuizini, ni lazima asaini karatasi rasmi sio kutamka tu.

Tanzania sio nchi ya ki-imla. Ina Katiba na Sheria zake. Wakuu wa wilaya na mikoa wanapswa kuzisoma sheria hizo ili wajue ukomo wa mamlaka zao. Sheria ya Tawala za Mikoa, inawapa madaraka ya kumweka mtu ndani iwapo tu mtu huyo ni tishio kwa amani na usalama wa eneo husika na si vinginevyo.

Utawala bora ni kuwasikili­za watu watoe dukuduku zao, na watumishi wanaolalam­ikiwa wapewe nafasi ya kujieleza na kusikilizw­a. Mara nyingine watu hupanga njama ya kumkomesha mtu fulani kwa sababu za kibinfsi na wakuu wanakuwa wepesi kuamua kwa kufuata ushahidi wa mdomoni.

Tujenge Tanzania yenye kuheshimia­na na kushirikia­na, ili kila mtu ajisikie anaishi katika nchi yake kwa amani na furaha.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.