NI NANI ATAITWA KWA BASHIRU BAADA YA MEMBE?

Rai - - MBELE - NA NDAHANI MWENDA

Kati ya vitu ambavyo vitakuja kuiondoa madaraka CCM, ni CCM yenyewe. Tangu mwaka 1995 hadi 2015 CCM imekubwa na mpasuko mkubwa ambao kadri ya siku zinavyokwenda mpasuko huo unadhidi kujidhihirisha kuwa upo na umezidi kuwa mkubwa zaidi ya tulio--nje tunavyodhani.

Mwaka 1995 kulikuwa na mpasuko mkubwa, waliotarajiwa kupokea kijiti kutoka Mzee Ali Hassan Mwinyi hawakuyanyaka madaraka, hivyo vita yao iliendelea hadi mwaka 2005 kundi la Jakaya Kikwete na swahibu wake mkubwa walipoyanyaka madaraka. Kundi hili linaaminika kuwa ndiyo lilikuwa na nguvu hata mwaka 1995, sema kwa kipindi hicho CCM ilikuwa bado ina mtu mwenye nguvu (si ya pesa) mwenye kuweza kuzima ‘uasi’ ndani ya chama, nae si mwingine ni Julius Nyerere!

Julius Nyerere licha ya kung’atuka madaraka Mwaka 1985 ndani ya chama na serikali bado alikuwa na nguvu ya kuzima hoja za kundi lolote ambalo aliona linakwenda kinyume na maadili ya CCM.

Kwa sasa CCM haina mtu kama Nyerere, waliopo wote hawawezi ikosoa serikali wala chama wazi wazi kinaookosea lakini Julius Nyerere aliweza, alikosoa na kuandika hata vitabu. Rejea kitabu chama cha Tujisahihishe! Julius Nyerere ndiye chanzo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, John Malecela kuacha ngazi ya Uwaziri Mkuu.

Tukirejea juu ya kundi la Jakaya Kikwete na Edward Lowassa kuyanyaka madaraka, baada ya muda kidogo kundi hili lilichonganishwa (kwa madai ya wengi) na hivyo kufikia mwaka 2008 lilivunika baada ya Edward Lowassa kujivua Uwaziri Mkuu, wajuvi wengi wa siasa wanadai kuwa, kundi hili lilichonganishwa kwasababu aliyekuwa Rais alikosa nguvu/sauti hivyo nchi ikawa ngumu kutawalika (sijui kama ni kweli), hivyo njia iliyobaki ilikuwa ni kuwagombanisha tu ili nchi iweze kutawalika, hapo mpasuko ulijionesha wazi wazi ndani ya CCM lakini vinara wa kundi hilo hawakutoka hadharani kutuhumiana.

Hadi kufikia mwaka 2010 kundi la Jakaya Kikwete na Edward Lowassa alikuwa limegawanyika katika vipande viwili, moja lakini yakifanya kazi moja ya kugombea madaraka ya nchi hii, akiwa Monduli JK alimnada EL katika kampeni na kudai kuwa kilichotokea ni ajali ya kisiasa, hivyo JK aliondoa uvumi wa yeye kutopika chungu kimoja na swahibu wake Edward Lowassa. Lakini pia inadaiwa kuwa huko ndani kulikuwa na vita kubwa baina ya hawa maswahiba ndiyo maana baadae iliibuka kampeni ya “Vua gamba’

Makundi ya Jakaya Kikwete na Edward Lowassa kuelekea Uchaguzi wa mwaka 2015 yalikuwa na wafuasi wengi Kwasababu makundi haya yalikuwa na nguvu kubwa kiasi cha kuviziana yenyewe kwa yenyewe. Karibia mwezi Mei 2015, EL na kundi lake walidaiwa kuanza kufanya kampeni za Urais mapema kinyume cha utaratibu.

Hadi kufikia Julai 2015 ilikuwa bado haitabiriki kama ni nani atapeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi ule ambao inaaminika kuwa ulikuwa na ‘Joto kali’ lakini hadi kufikia mwisho wa Agosti si kundi la Jakaya Kikwete wala la Edward Lowassa lilipeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi huo, inadaiwa Edward Lowassa jina lake hata halikufika Dodoma na yeye baada kuona kila dalili wapambe wake walihakikisha 2015 anaogombea Urais kwa njia yoyote ile, hivyo waliibukia mlango wa pili (Upinzani) kutimiza adhami yao ya kugombea Urais.

Inadaiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete alitaka kumfanya Benard Camillius Membe kuwa mgombea lakini kutoka na kumkata swahibu wake, alishauriwa hata BM asipite maana ingedhihirika kuwa anakinyongo na Edward Lowassa hivyo kilichotokea ni kuibuka kwa mtu ambaye wengi hawakudhania ndiye akapewa bendera, si mwingine ni Dk. John Magufuli!

Ikumbukwe Rais John Magufuli amekuwa Naibu Waziri, Waziri kwa miaka 20 hivi lakini yeye hakuwa jihusisha na haya makundi, yeye alidumu kwa sababu tu ya muonekano wake wa kiuchapa kazi, hivyo kwa kifupi JPM si mzoefu sana na siasa za CCM ingawaje yumo CCM kwa miaka 20+

Hivyo baada ya kuyapata madaraka JPM amekuwa akihaha kuunda kitu kipya wenyewe wanatoa #CCM mpya, tafsiri yake ni kwamba anaondoa wale wote walikuwa CCM enzi za Ben na JK na kuweka watu wake, hilo lipo kwa wanasiasa wote duniani, iwe kwenye vyama vya siasa ama Serikalini, huwezi kuwa na watu wasiokutii, ukitaka mwanasiasa ujijege kisiasa tengeneza watu watu wako watakaokutii.

Hivyo katika haraka za kutengeneza uhalali wake kisiasa ndani CCM na serikalini amekuwa akiibua watu wapya kila uchwao, wengine kwa kuwatafuta yeye mwenyewe na wengine kwa kujipendekeza wao wenyewe tu!

Na katika harakati hizi yameibuka makundi mengi yanayojifanya kumtetea JPM iwe ndani ya chama ama serikali hata nje ya chama na Serikali, kuna wanaojituma na wengine kutumwa kutokana na maneno yao na mambo wanayoyasema bila kificho.

Mmoja wapo ni Mkurugenzi wa Kampuni ya CZI, Cyprian Musiba. Huyu toka Februari 2018 amekuwa akitoa tuhuma mbalimbali dhidi ya watu mbalimbali. Alianza kwa kutoa orodha ya watu hatari hatukusikia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vikimhoji juu ya tuhuma hizo

Pia hivi karibuni ameibua tuhuma mzigo kwa madai kuwa kuna kundi jingine linafanya mpango wa kumhujumu JPM na Serikali yake, safari hii Cyprian Musiba amewataja watu Waziri nchi kama Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Rostam Aziz, Benard Membe, Zitto Kabwe, January Makamba, Mohammed Dewji, Yusuph Makamba, Abdulrahman Kijana na wengine!

Kama ilivyo kawaida kuna waliompuuza Cyprian Musiba na kuja walio sema katumwa ama anaumiwa, mtu pekee ambaye amekuwa akimjibu Musiba ni Zitto Kabwe tu, huu ukiwa wa wengine unaonekana kusumbua Musiba na waliomtuma kama inavyodaiwa.

Lakini baada ya tuhuma hizi, wengi wamekuwa wakidai kuwa ndani CCM kuna mpasuko na wanaoleta taharuki ni Kachero Benard Membe ambaye licha ya tuhuma zote hizo amekuwa hajibu.

Hapo jana Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally ameibuka na madai kuwa anamhitaji BM Ofisini kwake kwasababu licha ya kutumiwa amekuwa hajibu, hivyo pia anadai BM hajaonana na Katibu Mkuu wa CCM kama watia nia wote wa Urais wa mwaka 2015 walivyofanya, na hapo ndipo maswali mengi yanaibuka kuwa “Dk. Bashiru Ally Katibu Mkuu CCM-Taifa ametegua (amethibitisha CCM inamtumia Musiba katika kuchafua watu) kitanzi alichotega Cyprian Musiba?” Kama inavyodaiwa na wengi! Sote hatujui, BM ameitikia wito wa Katibu Mkuu Dk. Bashiru Ally lakini ametoa sharti kuwa siku atakapo kwenda kwa KM na Cyprian Musiba awepo ili athibitishe tuhuma dhidi yake kwasababu yeye ni mtuhumiwa hawezi thibitisha.

Lakini hadi sasa kukutana huko kwa Benard Membe na Katibu Mkuu wake kunaonekana kama kuotoa mbawa kwasababu masharti aliyoyaweka Bernard Membe Dk. Bashiru Ally (Katibu Mkuu CCM -Taifa) ameyakataa na amedai kuwa huo si utaratibu wake wa kukutana na wanachama wake labda Bernard Membe aseme yeye si mwanachama tena wa CCM. Lakini pia swali linakuja, Je wakati Katibu Mkuu anasemea kwenye vyombo vya habari juu ya kumtaka Bernard Membe aende Ofisini kwake huo ndiyo utaratibu wa chama kuita wanachama wake?

Nini kitatokea, Bernad Membe ataonywa ama Cyprian Musiba ndiyo ataonywa baada ya kushindwa kuthibitishwa tuhuma dhidi ya maana CCM M wenzake Bernard Membe? Je, baada ya Bernard Membe nani natafuta Ofisini kwa Bashiru Ally, Jakaya Kikwete ama Abdulrahman Kinana? Ikumbukwe hawa wote wametuhumiwa na Cyprian Musiba!

Bernad Membe na Dk. Bashiru Ally (kulia)

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.