Alimaye kondeni, hujulikana kwa Moshi

Rai - - MAONI / KATUNI - NA FAUSTIN SUNGURA

WIKI iliyopita nilielezea kwa kina mazingira ya kutekwa kwa bilionea kijana, Mohamed Dewji (43), mnamo asubuhi ya Alhamisi ya Oktoba 11, 2018. Endelea…

Jamii ya watu makini, kuanzia siku hiyo haikuwahi kuwa na mashaka yoyote juu ya afya na usalama wa Mohamed Dewji, jamii ya watu makini na hata ile ya wale weledi wa mambo, haikuwa kutilia maanani kauli ya Kamanda wa kanda maalum ya Dar es salaam, Afande Lazaro Mambosasa kuwa polisi wanaendelea kumtafuta Mohamed Dewji.

Kama ni kweli kuwa Mohamed Dewji aliendelea kutoonekana, bila shaka vyombo vya usalama vingemhoji Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, aeleze alikopata taarifa za kupatikana kwa Mohamed Dewji.

Jamii ya watu makini inajua ya kuwa, Mohamed Dewji alipatikana tangu tarehe 11/10/2018 kama ilivyotangazwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam; Mhe Paul Makonda, na kwamba baada ya kupatikana, polisi walikuwa wanafanya mambo yao ya kiupelelezi juu ya tukio hilo, lakini siyo tena kumtafuta mtu ambaye yupo nyumbani kwao.

Ninaamini, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Mhe; Paul Makonda kusema kuwa Mohamed Dewji ameshapatikana, polisi walijielekeza vibaya na kuwachanganya wananchi na wale wasiojua mambo ya itafiki walibaki wanaelea wasijue lipi ni lipi.

Ninaandika makala haya, pamoja na kutaka tuzo yangu halali, lakini pia kutaka mamlaka za nchi kuchukua hatua kwa baadhi ya maafisa wa serikali waliokuwa wanapingana na kauli ya Msemaji Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam.

Jamii ya watu makini, inapopitia taarifa za familia ya MO za juu ya alivyopatikana mtoto wao, inaliona taifa hili kudumbukia katika hatari juu ya afya na ustawi wa taifa makini katika miaka mizuri ijayo.

Mpango mzima wa kuuhabarisha umma juu ya kupatikana kwa Mohamed Dewji haukuzingatia na wala kujali kuwa taifa hili mbali na kuwa na watu wengi wavivu wa kufikiri, bado kuna watu wachache makini na ambao wanafuatilia mambo ya nchi hatua kwa hatua na hususani kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam aliyoitoa tarehe 11/10/2018 tena mbele ya afisa wa polisi.

Aidha, kwa maelezo haya na ambayo shahidi wangu ni afisa wa serikali (mkuu wa mkoa wa Dar es salaam), ninarudia kusema kuwa Mohamed Dewji alikuwa nyumbani kwa familia yake na kwa sababu hiyo, nimeweza kusema alikokuwa MO na hivyo ninastahili tuzo yangu ya shilingi Bilioni moja.

Mpaka hapo Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda atakapotakiwa kueleza ukweli na kukiri kwa umma kuwa aliliyoyasema awali kuwa si sahihi, vinginevyo; ninahitaji tuzo yangu ya Sh Bilioni moja kutoka kwa familia ya Mohamed Dewji.

Siyo jambo la afya ya ustawi wa nchi na raia wake, kuendelea kuwatia watu hofu kuwa watekaji wameizidi maarifa serikali na hali serikali ilifanya kazi nzuri ya kupongezwa kwa kumpata Mohamed Dewji mikononi mwa watekaji na kumkabidhi kwenye familia yake akiwa salama kama alivyosema Msemaji wa Mkoa wa Dar es salaam.

Aidha, jamii ya watu makini inataka kujibiwa swali hili; Je ni Afisa gani wa serikali kati ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na Kamanda wa polisi kanda maalum ya Dar es salaam, alikuwa anasema ukweli juu ya kupatikana kwa Mohamed Dewji (alipatikana tarehe 11/10/2018 au alipatikana tarehe 20/10/2018)

Mwisho lakini bado kwa umuhimu ule ule, makosa ni sehemu ya maisha, wale waliofanya makosa katika sakata zima la Mohamed Dewji na hasa kuendelea kuundanganya umma kuwa MO hajapatikana, si vema wakatumia ofisi za umma kupambana na ukweli.

Aliyepata kuwa Rais wa kwanza Mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela alipata kusema wakati wa jioni moja ya madaraka yake kwamba; “msinipime kwa mafanikio yangu, bali kwa makosa niliyoyafanya na baadae nikajirekebisha”.

Uli Hoeness, alipata kuwa Rais wa kilabu cha Buyern Munich cha nchini Ujerumani, alihukumiwa na mahakama ya Munich ya nchini Ujerumani kwa kosa la kukwepa kulipa kodi, alipewa haki ya kukata rufaa. Siku aliporudi mahakamani hapo kwa taratibu za kukata rufaa; aliushangaza umma mahakamani hapo.

“baada ya mazungumzo na familia yangu, nimeikubali hukumu ya mahakana (w) ya Munich juu ya masuala yangu ya kodi; ninasumbuliwa sana na nafsi yangu kwa kosa la kukwepa kulipa kodi,sitaki kukata rufaa, nitaenda jela kwa miaka mitatu na nusu”. Haya ni maneno ya Uli akionesha kujutia kosa lake lakini pia kutaka haki yake.

James Augustino Aloysius, raia wa Ireland aliyeishi kati ya mwaka 1882-1941 alipata kusema wakati mmoja wa jioni ya maisha yake “makosa ya mtu ndiwo mlango wake wa ugunduzi”.

Bill Clinton, rais wa 42 wa Marekani, naye alipata kusema wakati wa utawala wake, “ukiwa na maisha marefu, ni lazima utafanya makosa, lakini ukijifunza kutokana na makosa hayo, utakuwa mtu mwema”

Nimewarejea watu hawa kama njia ya kuonesha ustaarabu kwa watu wanaofanya makosa, kufanya makosa siyo mwisho wa maisha, lakini watu wema na wastaarabu huyafanya makosa yao kuwa mwanzo wa ukurasa mwingine wa maisha katika miaka yao mizuri ijayo.

Nimeandika makala haya, mbali na kusomwa na watu wa kawaida na wale wasio wa kawaida, nikiamini ya kuwa, taifa kama taifa litafaidika na baadhi ya yaliyomo katika makala haya, uongozi ulio madarakani kwa kila ngazi na nafasi yake, hautaichukulia makala haya kama kitu cha mpito bali kuifanyia kazi pale panapohusika.

Siyo jambo la afya kwa usalama na ustawi wa taifa huru, jamii kuambiwa kuwa mtu fulani ametekwa na majambazi, na siku hiyo hiyo serikali kupitia kwa mmoja wa maafisa wake akasema mtu huyo amepatikana, kesho yake afisa mwingine wa serikali hiyo hiyo akasema mtu huyo hajapatikana bado anatafutwa, halafu jambo hili likafanywa kama jambo la mzaha kwa maafisa wote wawili kuendelea kushika nyadhifa zao kana kwamba wananchi wote ni wajinga au ni wavivu wa kufuatilia mambo ya serikali yao.

Aidha, siyo jamba la afya kwa usalama wa raia katika nchi yao, familia moja kwa sababu tu ya nafasi yake katika jamii, kuvumisha uvumi kuwa ndugu yao ametekwa na ‘majambazi’, familia hiyo ikamalizana na ‘majambazi’ hayo hata wakamwachia ndugu yao; halafu familia hiyo ikalificha genge hilo bila ya kujua kuwa kesho litaleta tena madhara kwa familia nyingine; halafu jambo kama hili likafanywa kama jambo la mzaha.

Ninapofika jioni ya makala haya; ninachukua fursa hii adimu kuwashukuru wale wote waliosoma makala haya; lakini pia kuwaomba; kama mimi nilivyochukua hatua, nao pia wachukue hatua chanya kwa kadiri ya haki inavyoruhusu.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi kati ya mwaka 20002008, na mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini; Polisya Sikumbula Mwaiseje, alipata kusema wakati mmoja wa semina ya viongozi; “kuna uongozi wa aina tatu, kuna uongozi wa kuchaguliwa, kuna uongozi wa kuteuliwa na mwisho ni ule wa kujitokeza”.

Naye, aliyepata kuwa mwanafalsafa maarufu wa China ya kale, na aliyeishi katika karne ya sita (6), Lao Tzu; alipata kuelezea kwa kina ni nini maana ya kiongozi, mtu huyu pia ni muasisi wa falsafa inayohimiza binadamu kuishi maisha rahisi na ya kawaida inayoitwa Taoism.

Lao Tzu alisema “Kiongozi bora na mwema ni yule ambaye watu hawatambui mara moja kwamba yu miongoni mwao, ni yule ambaye majukumu yake yakiisha kukamilika na malengo yake yakisha kutimia, watu watasema; “tumepata mafanikio haya kwa juhudi zetu wenyewe”

Ni matarajio yangu, kwa falsafa za Mwaiseje na Lao Tzu, makala haya yamepata kusomwa na viongozi na hivyo, yatatendewa haki kwa kadiri ya nafasi ya kila kiongozi. Lakini pia ninataka tuzo yangu ya bilioni moja.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa namba 0769-668 284

Siyo jambo la afya ya ustawi wa nchi na raia wake, kuendelea kuwatia watu hofu kuwa watekaji wameizidi maarifa serikali na hali serikali ilifanya kazi nzuri ya kupongezwa kwa kumpata Mohamed Dewji mikononi mwa watekaji na kumkabidhi kwenye familia yake akiwa salama kama alivyosema Msemaji wa Mkoa wa Dar es salaam.

Paul Makonda

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.