Waamuzi, ratiba gonjwa lilelile TPL

Rai - - MAKALA JAMDIEISEMBA - NA AYOUB HINJO

SOKA ni mchezo unaohusisha hisia kwa kiasi kikubwa kuliko kitu chochote kile, ndio kwa maana ili uwe shabiki wa soka lazima kuwe na hisia za mchezo huo husika.

Tena kwa wale mashabiki vichaa wa soka hawaoni kazi kuweka maisha yao katika wakati mgumu ili mradi tu timu yake pendwa iweze kufanikiwa.

Duniani mpaka sasa mchezo wa soka ndio wenye mashabiki wengi zaidi kuliko mwingine wowote, kama ni takwimu basi zitakuwa juu zaidi kiasi ambacho si rahisi kuelezeka.

Pamoja na yote soka ni mchezo ambao unaongozwa kwa sheria kama ulivyo kwenye michezo mingine tofauti duniani.

Huku ikitambulika kuna sheria 17 za mchezo huo maarufu zaidi duniani ndio maana kumekuwa na mtu ambaye anasimama kati kuzitafsiri sheria hizo pindi timu mbili zinapokutana.

Mtu huyo anatambulika kama mwamuzi ambaye husaidiwa na washika vibendera (linesman) ambao mara nyingi hutoa msaada kwa mambo ambayo msimamizi wa kati huwa ngumu kuyaona.

Lakini tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu mpaka sasa kumekuwa na lawama nyingi sana kwenda kwa waamuzi kushindwa kusimamia sheria 17 za soka kikamilifu.

Hata kwa waamuzi huko Ulaya na sehemu nyingine zilizoendelea kisoka huamini sheria ya kuotea ‘offside’ ni ngumu zaidi hasa katika kuitafsiri.

Kwa upande wangu naamini hivyo pia, unaweza kudhani mchezaji ameotea lakini ukifatilia kwa ukaribu hakufanya hivyo na kinyume chake pia.

Ukakasi umekuwa mkubwa zaidi ukizingatia hivi karibuni tu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) walitoa maamuzi ya kuwafungia baadhi ya waamuzi waliofanya vibaya katika mizunguko ya mwanzo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL).

Tatizo kubwa ambalo lipo hapa nyumbani ni waamuzi wetu kushindwa kutoa maamuzi sahihi kwa wakati husika.

Si kwenye kuotea tu kama video nyingi huko mitandaoni zinavyoonyesha bali hata kwenye maamuzi mengine wamekuwa wagumu na kukiuka sheria zinavyowataka kufanya.

Kwa namna moja au nyingine hizo ni dalili mbaya kwa soka la nchi hii ambayo imeshindwa kupiga hatua kubwa katika mchezo huo kutokana na mambo ambayo yanaendelea ndani yake.

Kuna ile tabia ambayo imezoeleka ya waamuzi kushindwa kuchukua hatua eti kisa ni kosa la kwanza kwa mchezaji, kwa hiyo ataishia kuonywa tu, yapo makosa ya kutoa onyo na mengine si lazima hata kama ni mara ya kwanza kwa mchezaji aliyefanya tukio. Lakini mwamuzi

atashindwa kutoa kadi kwa kutokana na hofu ya kuharibu mchezo husika, hivi kwa mifano iliyo hai mwamuzi aliachaje kutoa penalti katika mchezo wa Mwadui dhidi ya Azam uliopigwa Uwanja wa Mwadui Complex.

Razak Abarola alifanya kosa ambalo hata kichaa pamoja na kutokuwa na akili timamu angetambua upuuzi alioufanya mwamuzi yule kwa kushindwa kuwapa Mwadui penalti waliyostahili.

Mifano ipo mingi lakini wakati mwingine waamuzi wa kati wanshindwa kupata msaada kutoka kwa wasaidizi wao ambao nao hufanya makosa ambayo hayastahili kutokea.

Kuna mambo mengi yakuudhi na kukatisha tamaa yameuzunguka mpira wetu ambao umeshindwa kuwa na thamani mbele ya macho ya wengi wanaoutazama.

Waamuzi kufanya makosa si jambo la kuzungumziwa kila siku lakini kwa hapa nchini limekuwa jambo la kawaida masikio mwa wadau wa soka ambao wanaamini wanachangia kushusha thamani ya soka la Tanzania.

Mara nyingi huwa naangalia jinsi timu zetu zinavyocheza dhidi ya timu za kimataifa ambazo mara nyingi husimamiwa na waamuzi kutoka nje, tazama jinsi wachezaji wanavyolalamika kwa kudhani wanaonewa.

Walishakosa msingi mzuri kutoka katika ligi yao kwa hiyo kila kit aka homilies kinyume na wanavyotaka wao wanaamini wanaonewa na utakuwa mjadala mkubwa kwa wao kushindwa kupata matokeo dhidi ya wapinzani wao.

Kwa hatua na muda ambao tupo hatupaswi kuwa na malalamiko juu ya waamuzi wetu lakini kutokana na kushindwa kufanya kazi yao kwa uhakika inapelekea hilo kutokea.

Hivi karibuni katika mchezo wa Prisons dhidi ya Yanga kulikuwa na maamuzi ya utata kutoka kwa mwamuzi aliyechezesha mchezo huo, nafikiri kila mmoja aliona na kukemia kile kilichotokea.

Kwa kipindi cha karibuni hakuna msimu uliopita bila kusikia waamuzi kufungiwa, hilo litaendelea mpaka lini? Hatupaswi kulalamika juu ya hilo ila msingi ambao tuliujenga umetufikisha hapa.

Mashabiki wanalipa viingilio kwenda uwanjani au kwenye mabanda ya kuonyesha picha za video kuangalia mpira wakiwa na matumaini makubwa lakini mara nyingi waamuzi wameshindwa kutenda haki kwenye viingilio hivyo.

Huo ni upande mmoja tu, kwingine kwenye upangaji wa ratiba wa ligi yetu kumekuwa na mtihani mkubwa sana.

Kila msimu lazima kuwe na malalamiko ya ratiba ambayo wakati mwingine hayana tija, unaweza kuona timu moja ikawa na michezo minne na zaidi ya viporo.

Achana na hiyo hivi karibuni Yanga walicheza michezo zaidi ya 10 katika Uwanja wa Taifa bila kutoka kwenda ugenini, hata kama mingine alikuwa mgeni kwenye uwanja huo lakini si hivyo ambavyo ipo.

Mwanzoni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara ratiba ilipangwa vizuri kwa kila timu kucheza michezo mitatu ugenini na nyumbani.

Ilikuwa ratiba nzuri kulingana na kukosa mdhamini wa ligi ingesaidia kwa timu wenyeji kukusanya fedha kabla ya kwenda mikoani lakini ghafla ilivurugwa na kuwa ndivyo sivyo.

Kila kitu tunachofanya tunapenda kujilinganisha na Ulaya ambako wameendelea kisoka na kiuchumi, basi kama ni hivyo tufanye hata 50% ya kile tunachokiangalia kutoka kwao itasaidia.

Rais wa TFF, Wallace Karia

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.