Walimu ‘feki’wasababishia hasara ya mamilioni Moshi

Rai - - MBELE - NA SAFINA SARWATT, MOSHI

IDADI kubwa ya walimu waliotimuliwa kazi kwa sababu mbalimbali kubwa ikiwa ni kuwa na vyeti feki vya elimu, imekisababishia hasara ya mamilioni ya fedha Chama cha Ushirika wa akiba na mikopo kwa walimu wa Moshi vijijini

(M.R.T.SACCOS).

SACCOS hiyo iliyoanzishwa mwaka 1998 inadaiwa kuwa ilikuwa ikijiendesha kwa mafanikio makubwa na kuwakwamua

waalimu, tofauti na hali ilivyo sasa.

Akizungumza na RAI, Meneja wa M.R.T Saccos, Bosco Simba alisema kuachishwa kazi kwa baadhi ya wanachama wao kwa sababu mbalimbali zikiwamo za vyeti feki kumewasababishia hasara kubwa.

Alisema walimu hao walioachishwa kazi kwa ujumla wao walikuwa na mikopo ya zaidi sh. 43,210,508, ambazo ni fedha za mtaji wa chama.

Aliweka wazi kuwa kutokana na deni hilo uongozi wa Saccos kwa kushirikiana na kamati za mikopo wamechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwafuatilia wadaiwa hao ili kupata ufumbuzi.

“Tumewafuatilia wadaiwa hao lakini mpaka sasa bado hatujapata muafaka kutokana kwamba kwa sasa hawana kazi hivyo tunasubiri kauli ya serikali, lakini pia tumelipeleka kwa Afisa Ushirika, “alisema Simba.

Mbali na chama kutikiswa na walimu feki, lakini pia kustaafu kwa baadhi ya walimu nako kumekuwa sehemu ya changamoto kwa Saccos hiyo.

“Maombi ya mkopo kwa kila mwezi yamekuwa yakipungua hali inayosababisha mzunguko wa fedha kutokuwa mzuri na hivyo kusababisha kushuka kila mwezi.

“Wanachama wengi kwa mwaka wa fedha 2017/ 2018 wamestaafu kwa lazima baada ya kutimiza umri wa miaka 60, hali hii imeongeza kupungua kwa makato mengi,”alisema.

Kwa upande wake mjumbe wa bodi ya chama hicho, Robert Materu alisema kuwa, wanachama wao wengi ambao ni walimu bado hawaitumii fursa ya kukopa kwenye Saccos yao.

“Wanakimbilia kukopa kwenye mikopo yenye riba ya juu, hali hiyo inawasababishia kushindwa kurejesha mikopo hiyo na kujikuta wakiweka kadi zao za benki kama dhamana.

“Baadhi ya wanachama w amekuw a wakiendelea kurubuniwa na taasisi nyingine za kifedha kwa kuwakopesha mikopo yenye riba kubwa hali inayowafanya kushindwa kurejesha na wengine kuwekeza kadi za benki kama dhamana ya mkopo, wakati wakikopa na kurejesha vizuri huku wala hawakutani na balaa hilo,”anasema Materu.

Chama hicho kilianzishwa rasmi mwaka 1998 kwa usajili KLR 528 kuendena na sheria na kanuni ya vyama vya ushirika nchini Tanzania.

Aidha, usajili huu ulifanyika chini ya usimamizi na uongozi wa chama cha walimu Tanzania wilaya Moshi vijijini, ambao walitoa viingilio kwa wanachama waanzilishi wapatao 98 lengo likiwa nikuwasaidia walimu kuondokana na hali duni ya kiuchumi.

Hali kadhalika tangu kuanzishwa kwa chama hicho cha ushirika wa akiba na mikopo wa waalimu wa Moshi vijijini mkoani Kilimanjaro, kimejiendeleza na kujiimarisha kwa kukuza mtaji wake wa ndani na kuongeza idadi ya wanachama kila mwaka ambapo kwa miaka 20 iliyopita kimefanikiwa kuwa na wanachama 2813.

Simba alisema kuwa dira na maono ni kuwa ushirika endelevu utakaohakikisha utoaji huduma za kifedha kwa wananchama wake, uhamasisha, kuendeleza, kuimarisha na kuwajasirisha katika mazingira bora na kuishindani.

“Lengo kubwa ni kutoa huduma endelevu kwa kufuata misingi ya biashara bila kuathiri au kukiuka misingi ya ushirika kwa lengo la kuchangia kupunguza umaskini miongoni mwa jamii,” anasema.

Amebainisha kuwa wanachama walikuwa na dira ya kuwa Saccos bora mkoani Kilimanjaro na nchini Tanzania na kufuata misingi ya kitaifa na kimataifa ya uendeshaji wa asasi za kifedha.

Simba alisema pamoja na changamoto mbalimbali za kiuchumi, ushirika umefanikiwa kutoa huduma za kifedha kwa wanachama kama vile ukusanyaji wa hisa, akiba, amana na viingilio.

“Pamoja na hasa iliyopo, lakini tutaendelea na utoaji wa mikopo mbalimbali ili kuwawezesha wanachama kiuchumi na kufanikisha ustawi wa jamii hasa elimu, makazi bora biashara au miradi hatimaye kupunguza umaskini kwa waalimu,” anasema.

Alisema kuwa Saccos hiyo imewasaidia walimu kuwa wajasiriamali, kuwajibika na kuthamini kazi yao kuendelea kulinda ushirika wao kwa nguvu moja na mshikamano.

Saccos hiyo itaendeleza ushirika kwa kupata fursa ya kuwekeza na kuendelea kupata elimu na semina mbalimbali juu ya ujasiriamali, utawala wa mikopo na maisha.

Chama hicho kimeendelea kuwahudumia wanachama walimu waliostaafu kupata huduma za mikopo, elimu na mambo mtambuka katika jamii.

“Kati ya wanachama waliostaafu mwaka 2015-2017 wanachama 71 wanaendelea na Saccos chini ya mpango wa ‘fixed deposit account’ na wamewekeza kiasi cha sh milioni 809.4 amana maalumu kwa riba ya asilimia 7 kwa mwaka,” anasema.

Saccos hiyo pia imewawezesha walimu katika shughuli mbalimbali kama vile elimu, ujenzi na ukarabati wa nyumba, biashara na ufugaji, ununuzi wa vyombo vya usafiri, (magari, pikipiki na baiskeli) na viwanja, pamoja na kusaidia utatuzi matatizo ya kijamii.

“Kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Septemba, mwaka 2018 jumla sh bilioni 2.7, sawa asilimia 68 ya mikopo imetolewa.

“Aina ya mikopo iliyotolewa ni mikopo ya biashara sh bilioni 2.2, mikopo ya elimu sh milioni 78.7, dharura sh milioni 444.1” anasema.

Alisema kuwa tangu chama hicho kianzishwa hadi kufikia Septemba mwaka 2018 jumla ya mikopo iliyotolewa ni sh bilioni 27.1.

Chama hicho kiweka mikakati mbalimbali ili kuhakikusha mikopo yote inayotolewa inazingatia vigezo na pia inakatwa kwa wakati katika mishahara ya wakopaji na kuepuka kutoathiri mzunguko wa fedha kwenye chama.

“Chama kimeendelea kusitisha huduma ya mikopo kwa baadhi ya wanachama ambao wamekuwa ni wadaiwa sugu na hivyo kuingiza chama kwenye mikopo chechefu hali inayowapelekea faida kuwa ndogo na kuathiri kiwago cha gawio, “alisema Simba.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.