Dk. Bashiru: Wanasiasa wanalinda matumbo yao

Rai - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally amesema wanasiasa wengi wanatumia mapinduzi ya kimtandao ya kijamii kulinda matumbo yao. RAI linaripoti.

Hatua hiyo imekuja kufuatia wimbi la wanasiasa kutumia mitandao ya kijamii ikiwamo Twitter, facebook na Instagram kuandika maoni au mawazo mbalimbali kwa lengo la kuifikia jamii kwa haraka.

Mapinduzi hayo imetafsiriwa na Dk. Bashiru kama moja ya mbinu ya kujishibisha matumbo yao, kufuatia kuibuka kwa taarifa nyingi za uongo zenye lengo la kukishambulia chama hicho, kama ilivyofanyika mwanzoni mwa wiki hii ambapo kulisambazwa taarifa za kuzuiliwa kuingia kwa Steven Wassira kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, mwanzoni mwa wiki hii, jijini Dar es Salaam mara baada ya chama hicho kumaliza vikao vyake, Dk. Bashiru alisema ulimwengu wa sasa unaishi katika kitu kinachoitwa ‘fake news’ (habari za kughushi).

Kauli hiyo ya Dk. Bashiru ilitokana na mojawapo ya maswali aliyoulizwa na waandishi wa habari kuhusu taarifa zilizozagaa mitandaoni kuwa Wassira ametimuliwa kushiriki Kikao cha Halmashauri kuu ya chama.

“Nathibitishia kuwa hizo ni pamoja na mfululizo wa habari ‘fake’ za mitandaoni. Wassira alihudhuria kikao. Amechangia, tumekula naye chakula. Ni mzima buheri wa afya.

“Naomba wanahabari… mimi ni mwalimu, nikiwa na nyie najihisi nipo darasani, taaluma yenu imevamiwa. Hiyo ni fake news. Mimi mwenyewe nakula viporo vya habari hizo. Kila mtu ni mwanahabari nikianza kusikiliza haya mabehewa ninayovuta yatadondoka ndio maana nimejizuia kuingia mitandaoni ila wasaidizi wangu wananisaidia. Sintaingia kwenye mitandao ya kijamii, isipokuwa nachujiwa na kula viporo,” alisema na kuongeza.

“Hali ni mbaya na hasa unapokuwa na jamii ambayo wanasiasa wake hawawajibiki kwa umma kwa walio wengi wanahangaika na kulinda matumbo yao na hali inakuwa mbaya zaidi kwa hiyo mlinzi wa wananchi ni wananchi wenyewe na ninyi wanahabari katika kulinda taaluma yenu dhidi ya habari za upotoshaji.

“Nasikitika na mimi sijui kama tulikuwa tunashambuliwa na ametajwa mtu muhimu sana ambaye amechangia, mtu anazua jambo ambalo halipo, ni uongo mtupu,” alisema.

Kauli hiyo ya Dk. Bashiru ingawa imekaa kiujumla, lakini wafuatiliaji wa mambo wanaamini kuwa imewagusa zaidi wale wanaopenda kutumia muda wao mwingi kurusha taarifa kwenye mitandao bila kujali ni wa chama gani.

Katika siku za karibuni kumekuwa na wimbi la baadhi ya wanasiasa kutumia mitandao ya kijamii kuikejeli au kukosoa utendaji wa chama na serikali iliyopo madarakani.

Pamoja mambo mengine aliendelea kusisitiza kuwa hawezi kukimbia wanahabari kwa kuwa katika mazingira ya sasa CCM kinatakiwa kuwa karibu na wananchi kwa kupitia waandishi wa habari.

“Pia wananchi wanatarajia maswali yenu yatuchokonoe tujibu mambo yanayofanana na shida zao. Ndio changamoto mliyo nayo nyie, kuwajua walaji wa habari zenu, msije kuishia kuwekwa mifukoni na kakundi kadogo ka walaji.

“Changamoto ya pili, taaluma hii imevamiwa, taaluma hii imevamiwa na kazi kubwa mliyonayo kwa haya mapinduzi ya habari, ni suala la fake news yaani ni shida. Tena kwa nchi masikini ambazo kila dakika ni muhimu kwa maendeleo tunajikuta tunajadili masuala ambayo ni mataptap,” alisema.

Hata hivyo, katika mkutano huo Dk. Bashiru alisema kuwa kutokana na muda mchache wa miaka miwili uliobaki kwa Serikali ya awamu ya tano kutimiza ngwe ya miaka mitano, changamoto iliyobaki ni kasi ya utekelezaji wa ilani.

“Changamoto ni kwamba CCM itatekeleza vizuri kipande cha ilani iliyobaki? changamoto ni kasi, namna gani wataendeleza kwa kipindi cha miaka miwili iliyobaki.

“Suala la kutathmini kasi ni suala la ushuhuda, tupo kwenye miaka mitatu, kasi inaridhisha ila changamoto ni namna ya kuiendesha mpaka mwisho bila mtu kuchoka. Tukifika mwisho tujitathmini ni asilimia ngapi. Sasa hivi ni kutamani kasi hii hii iendelee bila kuvuta miguu,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.