Mbowe, Lissu watikisa Ukawa mpya Zanzibar

Rai - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, pamoja na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu majina yao kwa pamoja yametajwa kutawala kikao maalum kilichokutanisha vyama sita vya siasa kilichofanyika Zanzibar mwanzoni mwa wiki hii.

Mbowe ambaye yuko mahabusu, jijini Dar es Salaam na Lissu ambaye yuko kwenye matibabu nchini Ubelgiji, wameibua mjadala mzito kwenye kikao hicho kilichoandaliwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi-CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.

RAI limeelezwa kuwa pamoja na hoja nyingine, lakini tukio la kupigwa risasi kwa Lissu na kuwekwa mahabusu kwa Mbowe, yalichukua nafasi kubwa kwa mijadala ya mkutano huo uliobeba sura ya kuundwa kwa Ukawa mpya na yenye nguvu zaidi.

Ukweli wa madai hayo unahalalishwa na viongozi sita vya vyama hivyo vilivyokutana kwa ajili ya kufanya tathmini ya hatima ya demokrasia nchini katika tamko la Azimio lao la Zanzibar.

Viongozi hao ni Maalim Seif, Mwenyekiti wa NCCRMageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa NLD, Oscar Makaidi, Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar na Salum Mwalimu.

Wengine ni Mwenyekiti wa Chauma, Hashim Rungwe na Kiongozi wa chama cha ACTWazalendo, Zitto Kabwe. TAMKO Tamko hilo ambalo limebeba kurasa tatu limeeleza masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzimia kuwa mwaka ujao utakuwa rasmi kwao kudai haki ya kisiasa, ikiwa ni pamoja na kuwapigania wanasiasa wote waliowaita wafungwa wa kisiasa akiwamo Mbowe.

Baadhi ya maneno ya kwenye tamko hilo yanaeleza kuwa: Sisi viongozi na wanachama waandamizi wa vyama vyetu sita vilivyosaini tamko hili, tumekutana Zanzibar kufanya tafakuri na kujadili juu ya dira yetu kama Taifa.

Mkutano huu maalum wa kihistoria ni taswira juu ya namna hali ya demokrasia yetu ilivyoharibika, na hivyo kututaka kukaa chini kuja na mkakati mpya na wa pamoja wa kupambana na hali husika.

Kwa masikitiko tuliwakosa viongozi wenzetu katika kikao chetu, Kiongozi wa Kambi Upinzani Bungeni, Freeman A. Mbowe, pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu A. Lissu, mmoja akiwa mahabusu, na mwengine akiuguza majeraha ya kupigwa risasi.

Tunafurahi kuwa wote wawili wametoa Baraka zao kwa kikao chetu hiki.

Tunatambua kuwa, Tanzania hivi sasa ina mmomonyoko wa demokrasia kwa ishara zote za utawala usiojali haki za kisiasa, kijamii pamoja na za kiuchumi kwa wananchi; ikiwemo kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2015 ambao CCM walishindwa; kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa kinyume kabisa na Katiba na sheria; kutekwa na kukamatwa kwa wananchi, wakiwemo viongozi wa kisiasa, waandishi wa habari na wafanyabiashara, kuokotwa kwa miili ya watu kwenye fukwe mbalimbali nchini; jaribio la kuuawa kwa Mbunge Lissu na hatua ya vyombo vya Ulinzi na Usalama kukataa kufanya uchunguzi wowote wa maana juu ya tukio hilo; uwepo wa sheria mbaya za Habari na Takwimu, pamoja na uletwaji wa kanuni za uendeshwaji wa Asasi za Kiraia (AZAKI), Kanuni za Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Mswada wa mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa.

Tunatambua kuwa, pamoja na kuwa Katiba inalinda mfumo wetu wa vyama vingi, dola sasa inaendeleza vita dhidi ya vyama vya upinzani pamoja na wote wanaonekana wana mawazo mbadala juu ya namna nchi yetu inavyoendeshwa.

Imekuwa ni kawaida sasa kwa Mkuu wa Nchi yetu, pamoja na wafuasi wake, kuwaita viongozi na wanasiasa wa vyama vya upinzani, pamoja na wakosoaji wa serikali kuwa ni ‘Mawakala wa Nchi za Nje’ na si Wazalendo.

Vita hiyo ya Serikali dhidi ya wote wenye mawazo mbadala imegusa kila kundi la kijamii nchini – Wanahabari, Wamiliki wa Vyombo vya Habari, AZAKI, Wakulima, Wavuvi, Wafugaji, Wafanyabiashara, Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi, Wafanyakazi, Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Wanadiplomasia, Viongozi wa Dini, Wanawake, na hata wanachama wa CCM yenyewe.

Tunashuhudia kuanguka kwa ushumi wa nchi yetu, jambo ambalo linawaumiza zaidi wananchi masikini. Pamoja na juhudi za propaganda za serikali kuonyesha kuwa hali ya uchumi ni nzuri kinyume na hali mbaya iliyoko, tunaona ni muhimu kueleza kwa uwazi kuwa baada mwelekeo mzuri kiasi wa hali ya uchumi wa nchi yetu kwa miaka kumi, hali ya uchumi wetu imeharibika katika kipindi cha miaka hii mitatu tu ya awamu ya tano.

Tunatambua kuwa tunao wajibu kama viongozi na raia wa nchi yetu, wa kushirikiana na wananchi wenzetu kuitoa nchi yetu kutoka katika hali mbaya tuliyonayo sasa, pamoja na kujenga na kupanua zaidi demokrasia yetu, ili ikidhi matakwa na matarajio ya watu wetu. Tunao wajibu wa kutoa dira kwa wananchi. Tunasema sasa basi imetosha.

Tunatangaza kuwa, sasa ni wakati sahihi na muhimu wa kuongeza umoha, mshikamano na kujitoa kwetu katika kuiendea ajenda yetu hii ya kitaifa ya kulinda Demokrasia yetu, jambo hili ni ajenda ya watanzania wote, ni zaidi ya maslahi ya vyama vyetu vya siasa. Jambo hili litahitaji ujasiri pamoja na kupambana na vitisho na madhara yote yatokanayo na dola, ni jambo litahitaji msisitizo juu ya mshikamano wetu hata pale nguvu kubwa ya kutuvunja na kutugawa itakapotumika, ni wakati wa kusisitiza umoja na kila kundi la kijamii.

Tunawatangaza rasmi wenzetu, Freeman Mbowe na Esther Matiko, ambao mpaka sasa wako mahabusu, kuwa ni wafungwa wa kisiasa na tangazo husika halitafutwa mpaka pale watakapoachiwa.

Tutapambana kuhakikisha kuwa wao na wafungwa wenzao wote wa kisiasa, nchi nzima, wanapewa nafasi ya kupata haki katika mfumo ulio huru, mbele ya mahakama na mbele ya macho ya umma.

Mbowe

Lissu

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.